Thursday, July 2, 2015

BEI YA PETROLI YAPAA KWA SASA NI Sh2,200 KWA LITA


Dar es Salaam.


Serikali imepandisha bei ya mafuta kuanzia leo baada ya jiji la Dar es Salaam kukumbwa na uhaba wa muda wa nishati hiyo kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kusitisha mauzo kusubiri kunufaika na bei mpya.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza jana kuwa kuanzia leo bei ya petroli imepanda kwa Sh232 kutoka bei ya sasa ya Sh1,966. Bei ya kikomo ya petroli sasa itakuwa Sh2,198, ikiwa ni ongezeko la asilimia 11.82.
Bei ya dizeli imepanda kwa Sh261, ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.65 na hivyo bei mpya itakuwa Sh2,043 badala ya Sh1,782, wakati mafuta ya taa yamepanda kwa Sh369 sawa na asilimia 22.75.
Tangu bei ya mafuta ghafi ishuke hadi chini ya Dola 50 za Marekani kwa pipa mapema mwaka huu na kusababisha bei ya petroli kushuka hadi Sh1,652 mwezi Machi, mwenendo wa bidhaa hiyo imekuwa ni kupanda.
Hadi jana, mafuta ghafi duniani yalikuwa yanauzwa chini ya Dola 60 za Marekani kwa pipa katika soko la dunia, lakini nishati hiyo nchini imerejea kwenye bei ambayo mafuta ghafi yalikuwa yakiuzwa Dola 100 kwa pipa.
Mkurugenzi mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi aliwaambia waandishi jana kuwa mabadiliko aliyotangaza yanatokana na bei ya mafuta katika soko la dunia, pia kuendelea kudhoofika kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani pamoja na mabadiliko ya tozo za Serikali katika mafuta kuanzia Julai Mosi, 2015.
Alisema thamani ya shilingi kwa machapisho ya bei za Juni na Julai 2015, imepungua kwa Sh 175.11 dhidi ya dola ya Marekani sawa na anguko la asilimia 8.65.
“Juni mwaka huu bei za jumla petroli ziliongezeka kwa Sh232.35 kwa lita sawa na asilimia 12.49, dizeli Sh261.15 kwa lita sawa na asilimia 15.57 na mafuta ya taa Sh369.41 kwa lita sawa na asilimia 24.32,” alisema Ngamlagosi.
Pamoja na naibu waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage kutoa tamko kali bungeni kuonya wafanyabiashara dhidi ya vitendo vya kutouza mafuta, baadhi ya vituo vilikuwa havitoi huduma jana na juzi.
Ewura ilisema jana inamfuatilia mtu aliyesambaza ujumbe kwa njia ya mitandao ya kijamii kutaarifu kuwapo kwa njama za wafanyabiashara kutouza mafuta kwa siku mbili kusubiri bei mpya.
Ngamlagosi alisema Ewura imeiandikia barua Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi kutaka wachunguze kujua ujumbe huo ili muhusika achukuliwe hatua.
“Upungufu wa mafuta uliojitokeza mkoani Musoma na kuwasababishia usumbufu wananchi tunafuatilia na tukibaini watapewa adhabu ya kulipa faini ya Sh20 milioni au kwenda jela au kufutiwa leseni ya biashara ya mafuta,” alisema Ngamlagosi.
 
Source: Mwananchi

No comments :

Post a Comment