Dar es salaam: Mahakama ya hakimu mkazi kisutu jijini Dar es Salaam imewahukumu kwenda jela miaka mitatu aliyekuwa waziri wa zamani wa fedha Basil Mramba,na aliyekuwa Waziri wa zamani wa Nishati na Madini,Daniel Yona baada ya kukutwa na hatia ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7.
Akizungumzia hukumu hiyo, Wakili wa washtakiwa hao, Peter Swai, amesema kwamba hukumu hiyo imetolewa na jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Samu Rumanyika, Jaji John Utamwa, pamoja na Hakimu Saul Kinemela, ambapo mtuhumiwa wa tatu wa kesi hiyo ambaye ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, amekutwa hana hatia huku mawakili wa washtakiwa wakiazimia kukata rufaa.
“Hatujaridhika na hukumu ila shauri limesikilizwa na
Mahakimu wa tatu. Na kwa mujibu wa sheria tukikata rufaa aidha watakubali wote
watatu au mmoja wao atakataa, kwahiyo iwapo mmoja wao atakataa na wawili
wakikubaliana hiyo ndiyo hukumu ya Mahakama, na hicho ndicho Mahakama
ilichofanya leo, hili ni jambo la kisheria kama tunaamini kwamba uamuzi
uliotolewa hauendani na sheria tutakata rufaa kwenye Mahakama ya juu na
itatafsiri sheria upya na sisi tutapata majibu” amesema
Swai.
Kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, kosa la
matumizi mabaya ya madaraka adhabu zake ni kulipa faini ya Sh. milioni 2 au
kifungo cha kati ya mwaka mmoja au miaka mitatu jela baada ya mshtakiwa
kupatikana na hatia.
Novemba 25, mwaka 2008, washtakiwa hao, walifikishwa
katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hezron Mwankenja, na
kusomewa mashitaka 13, likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka. Kesi hiyo
ilipangiwa jopo hilo na kuanza kuisikilizwa mapema mwaka
2009.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba katika mashitaka yaliyokuwa yanawakabili washtakiwa ni pamoja na kudaiwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 Jijini Dar es Salaam, washitakiwa wakiwa watumishi wa umma kama Mawaziri walitumia vibaya madaraka. Mramba na Yona wanadaiwa kuwa kati ya Juni 2003 na Mei 2005, wakiwa na nyadhifa hizo za uwaziri kwa makusudi na kutowajibika waliruhusu mkataba wa kuzuia kulipa kodi na kuipendelea kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya Alex Stewart (ASSAYERS) na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 11,752,350,148.00 kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
No comments :
Post a Comment