Butiku (pichani) alisema chimbuko hilo lilianzia mwaka 1995 lilipoundwa kundi la mtandao ndani ya chama hicho, wakati huo Kamati Kuu ikiwa kwenye mchakato wa kupitisha jina la mgombea urais wa chama hicho kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu.
“Mtandao huo iliamua kufanya kazi nje ya CCM kwa sababu itikadi zao na sisi zilitofautiana. Eti wanasema CCM ni chama cha mizengwe kinawachelewesha kutajirika. Sasa hao watu ndiyo wameendelea kuwapo na kusababisha haya matatizo yaendelee,” alisema Butiku.
Alisema hata wakati huu ambao Kamati Kuu ipo kwenye mchakato wa kumtafuta mgombea wa urais, kuna baadhi wa wajumbe waliotakiwa kushiriki kwenye kazi hiyo muhimu, lakini wapo nje, jambo ambalo alisema si sahihi.
“Kama baadhi wa watu muhimu wapo nje, sasa mwenyekiti wetu (Rais Jakaya Kikwete) amekwenda kufanya nini huko? Kama viongozi wa CCM wameshampata mtu wanayemtaka (kugombea urais) wanakwenda Dodoma kufanya nini. Huku si kumkejeli Rais Kikwete?” alihoji.
Akizungumzia rushwa, Butiku alisema sasa rushwa imetawala kila kona hata kwa viongozi wa juu.
Alisema viongozi hawafuati utaratibu, kila kitu lazima hela. “Sasa tunatoka kwenye utaratibu wetu wa vyama tunashiriki katika kufanya uovu. Kama haki inauzwa, hatuwezi kupata amani. Viongozi wanatoa rushwa hata kabla ya kupewa nchi. Je, wakipewa nchi itakuwaje?” alihoji.
Alisema kwa hali ambayo imefikia sasa ndani ya CCM, mtu kama hana fedha hawezi kuwa kiongozi.
Alisema vitendo vya watu kukiuka Katiba ya nchi na za vyama vyao vya siasa, ni ishara ya kutoweka kwa amani.
Butiku alivitaka vyama vya siasa nchini kupitisha wagombea waadilfu na kuwataka Watanzania kukikataa chama kitakachopitisha mgombea mla rushwa.
Warioba
Wakati Butiku akizungumzia kukithiri kwa ukiukwaji wa sheria na taratibu, Jaji Joseph Warioba aliangalia kazi atakayokuwa nayo Rais wa Awamu ya Tano.
Waziri huyo mkuu wa zamani alisema viongozi watakaochaguliwa wanakabiliwa na kazi nzito ya kulinda amani ya nchi kutokana kuanza kuibuka kwa matukio yanayoashiria kuvunjika kwa amani, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Alisema viongozi hao lazima wahakikishe kuwa wanawaunganisha Watanzania na kuwa kitu kimoja kama alivyofanya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na wenzake walipowaunganisha wananchi waliokuwa wamegawanyika baada ya nchi kupata uhuru 1961.
Alisema kwa sasa Taifa linakabiliwa na ukabilia, udini na ukanda.
“Tunaposema udini, ukabila na ukanda tutazame hali iliyopo sasa. Tuna vyama vya siasa ambavyo ni kama vya ukabila hivi,” alisema Jaji Warioba.
“Mtu aliyevaa gwanda (sare zinazotumiwa na Chadema) akionekana katika mkutano wa wanaovaa sare za kijani (rangi inayotumiwa na CCM) ni balaa. Na hata wa sare za kijani akionekana katika mkutano wa wanaovaa gwanda ni hatari pia,” alisema.
Alisema jambo hilo linaondoa umoja na kuwafanya watu kuanza kubaguana.
“Mambo hayo yanatakiwa kusimamiwa na viongozi,” alisema akielezea jinsi Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo alikuwa mwenyekiti wake, ilivyopendekeza Tunu za Taifa na kuziingiza katika Rasimu ya Katiba kwa ajili ya kudumisha mshikamano na umoja wa Watanzania.
“Katika nchi yetu kila mtu anamlalamikia mwenzake. Vyama vya siasa vinailalamikia serikali, mahakama, chama tawala na serikali nayo inavilalamikia vyama vya siasa. Kila kundi linasema likichukua madaraka litakomesha rushwa,” alisema akirejea ahadi za wagombea uongozi.
“Tunakwenda katika uchaguzi lakini huku tukiwa na viashiria vya uvunjifu wa amani. Hivi nani hajui kuwa kuna rushwa kubwa katika uchaguzi, “ alisema na kusisitiza kuwa Mwalimu Nyerere alijenga umoja kwa kuondoa matabaka, ukabila na udini, mambo ambayo alisema yananza kurejea hivi sasa.
Profesa Baregu
Wasiwasi wa kuvunjika kwa amani pia alikuwa nao Profesa Mwesiga Baregu ambaye pia alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kama umakini utakosekana kipindi cha uchaguzi, kuna uwezekano mkubwa kukatokea machafuko kama ilivyokuwa kwa nchi jirani ya Kenya,” alisema Profesa Baregu.
“Mwaka 2008 Kenya kulitokea machafuko na idadi kubwa watu walipoteza maisha kwa sababu viongozi walichakachua Rasimu ya Katiba waliyopelekewa na tume yao ya katiba.”
Aliongeza kwamba ikiwa viongozi wa nchi hawatasimama imara suala la amani litakuwa ni ndoto kwa sababu wananchi wanapigakura huku kukiwa hakuna Katiba Mpya.
Polepole
Mjumbe mwingine wa Tume ya Warioba, Humphrey Polepole alizungumzia tatizo la ajira akisema uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano upo njia panda kwani uchumi unayumba na hakuna mambo ya msingi yanayoendelea.
Alisema nchi inakabiliwa na tatizo la ajira kwa vijana ambalo kwa kiasi kikubwa linatokana na ukosefu wa maadili kwa viongozi.
Source: Mwananchi
No comments :
Post a Comment