Dar es salaam: Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura kwa teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) lililoahirishwa katika jiji la Dar es salaam na mkoa wa Pwani hivi karibuni sasa litafanyika kuanzia Julai 7-20 kwa mkoa wa Pwani na Julai 16- 25 kwa jiji la Dar es salaam.
Uboreshaji wa Daftari hilo kwa jiji la Dar es salaam na
Mkoa wa Pwani uliahirishwa kutokana na kuchelewa kwa vifaa vya uboreshaji kutoka
mikoani ambavyo vilipelekwa ili kuongeza ufanisi kutokana na maeneo hayo kuwa na
idadi kubwa ya watu wenye sifa ya kuandikishwa kuwa Wapiga
Kura.
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Julius Mallaba
amewataka wananchi wote wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya
uandikishaji vitakavyokuwa kwenye Vijiji, Vitongoji na Mitaa ili kujiandikisha
waweze kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu Mwezi
Oktoba Mwaka huu.
Amewataja watakaohusika na zoezi hili kuwa ni watu wote
waliotimiza umri wa Miaka 18 na kuendelea na wale watakaotimiza Miaka 18 ifikapo
mwezi Oktoba Mwaka huu.
Wengine ni waliojiandikisha awali kwenye Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura la zamani ili kuhuisha taarifa zao na kupata kadi mpya za
kupigia kura. Aidha Mallaba amewataja wengine wenye sifa ya kujiandikisha kuwa
ni wale wote wenye sifa za kujiandikisha lakini hawajawahi kujiandikisha kwenye
Daftari hilo.
Amesema wale wote wenye Kadi za kupigia Kura za zamani
wanatakiwa kwenda na Kadi zao ili kurahisisha uchukuaji wa taarifa zao na kadi
hizo zitarudishwa NEC na watapata vitambulisho vipya. Wananchi wanatakiwa
kujiandikisha katika Vituo vilivyopo ndani ya Kata zao ili kuweza kupata fursa
ya kumchagua Diwani, Mbunge na Rais.
Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa wananchi wa mikoa hiyo
kuhakikisha wanajiandikisha kwani bila kufanya hivyo hawataweza kupiga Kura
wakati wa Uchaguzi Mkuu. Vituo vya kujiandikisha vitafunguliwa kila siku kuanzia
saa 2:00 asubuhi na kufungwa ifikapo saa 12:00 jioni
No comments :
Post a Comment