Dodoma: Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Watanzania limewasimamisha wabunge 11 kwa kudharau mamlaka ya Spika jana.
Hatua hiyo ni baada Spika wa Bunge hilo, Anne Makinda, kuwashitaki katika Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, wabunge hao wa Kambi Rasmi ya Upinzani, wakiongozwa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi hiyo, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).
Makinda alichukua hatua hiyo, baada ya wabunge hao kurudia kwa mara ya pili kufanya vurugu na kupiga kelele wakati kikao kikiendelea na kumlazimisha kuahirisha kwa mara ya nyingine shughuli za bunge zilizokuwa zikiendelea bungeni mjini hapa.
“Bunge haliwezi kuendeshwa kwa kelele na vurugu namna hii. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, ninawataja kwa majina vinara wa vurugu ambao walitakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili na kulazimika kuahirisha Bunge hilo hadi jioni."
Hukumu ya Watuhumiwa
Kamati hiyo ilitoa adhabu kwa mafungu matatu ambapo wapo ambao hawakutoa ushirikiano kabisa kwa kamati hiyo wakidai wangefanywa hivyo mbele ya wanasheria wao, hao walifungiwa moja kwa moja, waliotoa ushirikiano kwa kamati wakafungiwa kutohudhuria vikao viwili na wengine waliochelewa kupata wito wanatakiwa kuhojiwa na kama leo asubuhi saa nne wakati mmoja hakuguswa na adhabu hizo kabisa.
Waliosimamishwa moja kwa moja ni Lissu, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Paulina Gekul (Chadema), Mbunge wa Mohambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Kasulu Mjini na Moses Machali (NCCR-Mageuzi).
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), Rashid Ally Abdallah (CUF) na Mbunge wa Gando, Khalifa Khalifa (CUF), hao wanatakiwa kufika katika kamati hiyo ya maadili leo kwa kuwa hawakupata wito wa kuitwa jana mapema huku Mbunge David Silinde hakuguswa kabisa katika adhabu hiyo.
Kundi la pili waliofungiwa vikao viwili, cha leo na Jumatatu ni Mbunge wa Ole, Rajab Mbaruk Mohamed (CUF) na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) ambao waliitikia wito na walitoa ushirikiano kwa Kamati hiyo ambayo Makamu Mwenyekiti wake ni Brigedia Hassan Ngwilizi, ambaye ni Mbunge wa Mlalo (CCM).
Akiwasilisha maamuzi ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa kamati alisema walifikia maamuzi hayo baada ya kuridhika baada ya kuwaita wahusika na kujieleza na hatimaye kufikia maamuzi hayo.
Kamati hiyo ambayo Makamu Mwenyekiti wake ni Kapteni John Chiligati, ambaye ni Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM) ilitoa maamuzi hayo kulingana kanuni za Bunge.
Ilivyokuwa
Vurugu hizo zilianza mara baada ya Lissu kusimama kuomba Mwongozo wa Spika, wakati Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alipokuwa akisoma kwa mara ya pili, muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesi wa mwaka 2015, ambao Kambi ya Upinzani ilikuwa ikiupinga tangu mwanzo.
Wakati wakipiga kelele, Spika alinyamaza na Simbachawene akaendelea kusoma muswada huo, ndipo wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani wote waliokuwepo bungeni wakasimama kumuunga mkono Lissu na kuwalazimu baadhi ya wabunge wa CCM kuanza kuwazomea na wao kurudisha maneno yaliyosababisha hata aliyekuwa akisoma asisikike.
Msimamo wa upinzani
Pamoja na yaliyotokea, kambi hiyo ilijikusanya ndani ya Bunge hilo kupeana misimamo ambapo, walisikika wakisema hata iweje, hawatakubali muswada huo wa Sheria ya Mafuta na Gesi upite.
Katika hatua nyingine, Spika Makinda alikataa kuendekeza malalamiko ya Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata (CCM), aliyeomba mwongozo na kudai kuwa, Mbunge wa NCCRMageuzi, Moses Machali alimdhalilisha kwa kumwambia kuwa, alifumaniwa na wajinga wenzake.
Machali alisema hivyo alipokuwa akitoa maoni ya muswada uliopitishwa wa Ulinzi wa Mtoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi, baada ya kukasirishwa na kitendo cha Mlata kuropoka kuwa Mbunge huyo aliyetaka adhabu iwe kunyongwa ni kichaa.
“Leo wote mmeonesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu, kwa kutoleana maneno yasiyofaa. Wengine mmekuwa mkiingilia hoja za wenzenu wakati wanaziwasilisha, kwa kuwatolea maneno yasiyo na adabu,” alisema.
No comments :
Post a Comment