Saturday, August 1, 2015

MASWALI YAZIDI MAJIBU KUHUSU DR. SLAA NA MNYIKA


Hofu imetanda ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wananchi kwa ujumla kutokana na kutoonekana kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, katika matukio mawili makubwa ya kisiasa yanayohusu mustakabali wa chama hicho.

Dk. Slaa hakuonekana siku ya kihistoria Jumanne wiki hii, iliyokuwa maalum kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kutangaza kujivua uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga CHADEMA.

Kadhalika, Dk. Slaa hakuonekana jana makao makuu ya chama wakati Lowassa alipofika kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia chama hicho akitarajiwa kuwakilisha Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), katika hafla iliyotikisa jiji la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa juu wa CHADEMA.

Hata hivyo, Dk. Slaa alihudhuria kikao cha dharura cha kamati kuu ya CHADEMA Jumapili iliyopita ambacho kiliendelea hadi usiku wa manene na hoja kuu ikiwa ni kujadiliana na Lowassa na kumpokea katika chama hicho.

Dk. Slaa alionekana katika baadhi ya picha zilizovuja kutoka katika kikao hicho akiwa na viongozi waandamizi wa CHADEMA huku akijadili jambo na Lowassa, ambaye katika siku za hivi karibuni ambekuwa gumzo kubwa baada ya kubadili upepo wa siasa za Tanzania. 

Tangu juzi kumekuwa na mijadala mirefu ndani ya mitandao ya kijamii, juu ya aliko Dk. Slaa, wengine wakibashiri kuwa ameamua kuacha siasa.

Hata hivyo, Dk. Slaa mwenyewe hajawa radhi ama kupokea simu yake au kujitokeza hadharani kujibu maswali ya umma juu ya kinachomsibu.

Mbali na kutokuonekana CHADEMA, Dk. Slaa pia hakuonekana kwenye mkutano wa UKAWA, uliofanyika Jumatatu wiki hii makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), ambao wenyeviti wenza wa umoja huo walimkaribisha Lowassa kujiunga nao.

Wakati wa Dk. Slaa akiadimika kwenye hadhara, viongozi waandamizi wa CHADEMA kwa nyakati tofauti wameithibitishia NIPASHE kuwa kila kitu “kimedhibitiwa” kuhusu tetesi kwamba kiongozi huyo amesusa.

“Sikiliza brother, Dokta yuko freshi. Kila kitu kinakwenda kama tulivyopanga. Hakuna ukweli wa lolote juu ya madai eti Dokta anakwenda CCM,” 
kilisema chanzo chetu kilichoomba kutotajwa kwa sasa.

Wakati hali ikiwa hivyo, kuna taarifa kwamba Dk. Slaa anashinikizwa sana na watu wa ndani ya familia yake ambao wanadaiwa kusumbuliwa zaidi na ubinafsi, hasa baada ya mabadiliko ya kisiasa ambayo yamekikumba chama hicho kufuatia kujiunga kwa Lowassa.

Watu hao wa ndani wa familia ya Dk. Slaa wanadaiwa kuwa walikuwa wamejiandaa kuwa sehemu ya harakati za katibu mkuu huyo kuwania tena urais mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka 2010.
“Sisi tunawaza jinsi ya kuivunjavunja CCM, lakini wapo watu wanawaza jinsi ya kuwa sijui nini sijui nani?
Hapa tunatafuta njia ya kuing’oa CCM hata kama ni kwa kutumia nguvu ya shetani,”
 alisema kiongozi mmoja wa CHADEMA.

Lowassa aliamua kujiunga CHADEMA baada ya kuchoshwa na siasa zilizojaa chuki za kumzuia kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya kuwania urais kupitia CCM.

Katika hatua nyingine, Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu, aliliambia NIPASHE kwamba, Dk. Slaa alishiriki vikao vyote muhimu vilivyoafiki, Lowassa kujiunga na chama hicho.
“Jana (juzi) usiku nilikuwa naye na wiki hii alishirika kikao cha kamati kuu ambacho mliona picha kwenye mitandao,” 
alisema.

Alipoulizwa alipo, Dk. Slaa, Lissu hakutoa majibu ya moja kwa moja zaidi ya kusema kwamba akiwapo mwenyekiti kwenye kikao chochote inatosha na siyo lazima, viongozi wote wa kitaifa wawepo.

Kuhusu Naibu Katibu wa CHADEMA, Tanzania Bara, John Mnyika na yeye kutoonekana katika mikutano hiyo, alijibu kwa kifupi kwamba anaumwa.

Licha ya kutafutwa mara kadhaa kupitia simu yake ya mkononi juzi na jana, Dk. Slaa hakupatikana badala yake mtu mmoja mwanamke alipokea na kusema mpigaji amekosea namba.

Alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno ili aeleze kilichomsibu kushindwa kuhudhuria matukio muhimu ya kumkaribisha Lowassa pia hakujibu.
  • Taarifa hii imenukuliwa kutoka NIPASHE

No comments :

Post a Comment