Matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yanayokwenda sambamba na kupora silaha, kuua askari na kujeruhi imebainika kuwa yanasukwa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu waliopo ndani ya Jeshi la Polisi au waliofukuzwa kwa makosa mbalimbali ukiwa ni mkakati wa kumdhoofisha kiutendaji Mkuu wa Jeshi hilo IGP, Ernest Mangu.
Uchunguzi wa kina ambao umefanywa na NIPASHE kwa takribani wiki tatu sasa umebaini kuwa hatua ya baadhi ya askari polisi kuasi ndani ya jeshi hilo kunatokana na kuchukizwa na mambo kadhaa yaliyofanywa na IGP Mangu tangu alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo.
Baadhi ya watumishi wa serikali waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema mambo ambayo yamechukizwa baadhi ya watu ndani ya jeshi hilo ni kutokana na kufukuzwa kazi askari wengi na wengine kubadilishwa vituo vyao vya kazi kwa sababu mbalimbali, mambo ambayo yamefanyika kipindi cha IGP Mangu.
“Unakumbuka wakati Sanya (Laurance Sanya) alipokuwa RPC Mbeya kulitokea tukio moja la uvamizi wa Kituo cha Polisi Tunduma lakini kipindi cha utawala wa IGP Mangu yamejitokeza mengi hapa kuna sababu,” alisema.
Alisema IGP Mangu amekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi ambaye ameongoza kufukuza askari hususani wanaokula rushwa ambao hakuwavumilia na ndiyo hao hao wamegeuka kuwa adui wa jeshi hilo kwa kushirikiana na jamaa na ndugu zao ambao bado wapo ndani ya utumishi wa jeshi hilo.
Jambo la pili lililojenga hasira kwa askari hao ni hatua ya IGP Mangu kutoa tishio kwamba askari wote ambao wana vyeti vya kughushi wajisalimishe.
“Taarifa za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaonyesha kuwa zaidi ya watumishi 10,000 wa Jeshi la Polisi wana vyeti vya kughushi lakini kwa bahati mbaya katika awamu zote za utawala wahusika wamekuwa wakiachwa bila kuchukuliwa hatua na sasa IGP Mangu amekuja kuyavumbua,” kilisema chanzo kutoka ndani ya serikali.
Chanzo hicho kilieleza kuwa baada ya IGP Mangu kutoa tamko la kutaka watumishi ndani ya jeshi hilo wenye vyeti vya kughushi wajisalimishe ndipo matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yalipoibuka kwa kasi ili mkuu huyo wa Jeshi la Polisi aonekane ameshindwa kazi na kufukuzwa.
Anaeleza kuwa kuhusisha matukio ya uvamizi huo na suala la ugaidi inaweza kuwa siyo kweli kwa asilimia kubwa kwa sababu mara nyingi magaidi wanaofanya matukio makubwa mfano nchi jirani wanakuwa na silaha kubwa kama AK-47 sasa inawezekanaje kama kweli ni magaidi hapa kwetu wawe wanapora bunduki ndogo za SMG.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijobisimba, alisema matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yameanza kujitengeneza pole pole na sasa yamekuwa makubwa.
“Matuki ya vituo kuvamiwa yalianza kwa wananchi wenye hasira kutaka kutoa watu waliokamtwa na baadaye wakaona kama kumbe ni rahisi kuvamia kuiba silaha, kujeruhi askari na kuua,” alisema.
Alisema wakati hali ya kiuslama ikibadilika, Jeshi la Polisi kwa upande wake bado halijabadilika ili kukabiliana na matukio hayo.
“Zamani usingeweza kuona askari anayetembea barabara ananyang’anywa silaha hata kama huyo askari yukoje, lakini hivi sasa polisi wapo kwenye doria wanavamia na kunyanng’anywa silaha, wanaenda kama vile nyumbani kwao na bahati mbaya polisi wenyewe hawajashtuka,” alisema.
Kijobisimba alisema polisi wangekuwa wamebadilika kiutendaji matukio hayo yasingetokea.
Alisema sababu nyingine ya kuibuka kwa matukio hayo ni ndani ya Jeshi la Polisi lenyewe kuna tatizo ambalo inabidi litafutiwe ufumbuzi.
“Ukiangalia tukio la uvamizi wa Kituo cha Polisi Stakishari ni utata, mimi nilikuwa jeshini, utunzaji wa silaha unakuwa very secure (usalama mkubwa), sasa wale Stakishari utunzani wao wa silaha unakuwaje kiasi kwamba wavamizi waliingia mara moja na kuchukua silaha kama kweli hakukuwa na inside job (kazi ya ndani),” alisema na kuongeza:
“Katika tukio hilo pengine inawezekana hata mfungaji wa mlango wa kutunzia ofisi akawa alisahau kufunga kwani wavamizi wasingeweza kufika kirahisi na kupora.”
Bikijobisimba alisema mambo hayo yanaweza sehemu ambayo kuna askari ambao siyo waadilifu kutokana na jinsi wanavyopewa mafunzo.
“Zamani kulikuwa na utaratibu mtu akitaka kuajiriwa polisi wanaangalia urefu ndiyo wanachukuliwa, lakini leo hii hata wafupi wapo wengine na inawezekana wanapelekwa na ndugu zao na pia mafunzo yanatolewa kwa miezi sita wakati zamani ilikuwa miezi tisa,” alisema.
Alisema mafunzo ya miezi sita kimsingi hayawezi kutosha kumfundisha askari kuwa katika maadili mazuri na mkakamavu kiasi cha kuaminiwa kuwa mlinzi wa taifa.
Kijobisimba alisema ili kukabiliana na matukio hayo kuna umuhimu wa Jeshi la Polisi kutafuta chimbuko la matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi kwani lazima kutakuwa kuna tatizo.
Naye mwanaharakati wa haki za binadamu, Julius Niselia, alisema matukio hayo yanaonyesha kuwa mabadiliko ya uongozi ndani ya Jeshi la Polisi yaliyomwingiza IGP Mangu hayakupokelewa vizuri ndani ya jeshi hilo na baadhi ya askari waliokuwa watii kwa uongozi uliondoka ambao wamekumbana na fagio la chuma la uongozi mpya na ndiyo wanaofanya njama hizo.
“Mangu ni mkali sana hapendi askari wanaofanya uovu hivyo amekuwa akichukua hatua haraka na kusababisha malalamiko kwa askari ambao walilelewa vibaya ndani ya jeshi hilo na viongozi wapole wasiochukua hatua,” alisema.
“Askari wanaofukuzwa kwa utovu wa nidhamu ndiyo wanaounda magenge ya kihalifu ili kumdhoofisha IGP Mangu aonekani hafai kiutendaji,” alisema.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Pentekoste World Mission International, Samson Mwalyego, alisema chanzo cha matukio hayo ni kuporomoka kwa maadili ndani ya Jeshi la Polisi.
Alisema ndani ya jeshi hilo watumishi wanajali zaidi rushwa na wamekuwa siyo wa siri wanapopewa taarifa jambo ambalo limewakatisha tamaa wananchi kushirikiana nalo.
Wakati hayo yakiendelea baadhi ya askari polisi wamelalamikia kitendo cha serikali kupuuza malalamiko yao mbalimbali ikiwamo ubaguzi katika upandishaji wa madaraja na nyongeza ya kima cha mshahara tangu miongoni mwao walipopandishwa vyeo Agosti, mwaka jana.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya jeshi hilo zinaeleza kwamba, kutokana na hali hiyo kiwango cha utendaji kazi kwa polisi hao kimeshuka kutokana na uongozi wa juu kukaa kimya.
Hata hivyo, imefahamika kwamba tatizo hilo limefanywa kuwa siri na hakuna askari anayeruhusiwa kuzungumzia kwa uwazi.
Askari wachache ambao walikuwa mstari wa mbele kufuatilia suala hilo, imedaiwa sasa wamenyamazishwa baada ya kupewa stahiki zao kinyemela.
“Tumevumilia vya kutosha jambo hili, hivi vyeo tulivyopewa ni kama hewa, tukiuliza ngazi za juu hawatupatii majibu ya kuturidhisha,” kilisema chanzo kimoja.
Mmoja wa askari hao ambaye alitaka jina lake lisitajwe, alisema malalamiko hayo yanawahusu askari wengi nchi nzima ambao walikwenda katika mafunzo mwaka jana.
Alisema licha ya kufanya vizuri na kupandishwa vyeo mbalimbali vya kijeshi, mishahara yao imebaki kama mwanzo jambo ambalo limewarudisha nyuma kiutendaji.
“Huwezi kufanya kazi nzuri katika hali hii, tunachoomba serikali isikilize kilio chetu na kututatulia,” alisema askari huyo.
Askari mwingine alisema huko nyuma waliunda kamati maalum ya kufuatilia suala hilo ngazi za juu za jeshi hilo, lakini walikatishwa tamaa baada ya kuona kuna tatizo katika mchakato wa kuwaongezea maslahi.
“Jambo la kusikitisha watu wachache walionekana wasemaji waliingiziwa pesa za nyongeza, tuliobaki hatujui tutafikiwa lini na hakuna anayethubutu kusema kwa uwazi ili kulinda kibarua chake,” alisema.
TUME YAUNDWA
Askari hao walidai mwanzo wa mwaka huu serikali ilifanya uhakiki wa watu wanaotakiwa kuongezewa mishahara kulingana na nafasi zao za kazi.
Alisema licha ya kupewa ushirikiano na askari hao katika vituo vyote walivyotembelea, hadi sasa hakuna jibu lolote walilopewa, badala yake walitakiwa kuukaa kimya.
“Tunajua IGP anajua tatizo hili vizuri, tunamuomba atusikilize malalamiko yetu na kuyafanyia kazi kwa haraka,” alisema.
VITUO VILIVYOVAMIWA
Katika kipindi cha kuanzia Juni, 2014 mpaka Julai 13, mwaka huu, bunduki 53 zimeporwa katika matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi na askari 11 kuuawa.
Vituo vya polisi vilivyovamiwa ni Newala mkoani Mtwara, ambako bunduki tatu ziliporwa, mkoani Pwani katika wilaya ya Ikwiriri (bunduki saba), Kimanzichana, wilaya ya Mkuranga (bunduki tano) mbili zikiwa za polisi na tatu za raia zilizokuwa zimezihifadhiwa.
Vingine ni Kituo cha Polisi Ushirombo wilaya ya Bukombe, mkoani Shinyanga bunduki 18 ziliporwa, ingawa baadaye zilipatikana zote.
Kituo cha Polisi Pugu Machinjioni, mkoani Dar es Salaam na Tanga, askari waliokuwa katika shughuli za ulinzi na doria walishambuliwa na kuporwa silaha tatu na Kituo cha Polisi Stakishari, Dar es Salaam ambako bunduki 20 ziliporwa na askari wanne na raia watatu kuuawa.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment