MBUNGE wa Mpanda Mjini, Said Arfi, jana
aliwaaga wapiga kura wake akiwaeleza kuwa uanachama wake Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) utakoma mara baada ya kuvunjwa kwa Bunge la 10 mjini
Dodoma.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Shule ya Msingi Kashato mjini hapa jana, Arfi,
aliyekiwakilisha chama hicho kwa miaka 10 mfululizo, aliwaambia wananchi kuwa
jimbo hilo litakuwa wazi wakati wowote wiki ijayo.
“Kama Chadema wana ubavu, waje
walikomboe jimbo hili. Mimi ninaifahamu Chadema kuliko mtu yeyote mkoani Katavi
kwani nilikuwa Makamu Mwenyekiti (Bara), na sasa nitamuunga mkono yeyote
anayefaa kuwa mrithi wangu,” alisema Arfi na
kushangiliwa.
Mkutano huo uliohudhuriwa na umati
mkubwa, ulikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi kutokana na kuzagaa kwa taarifa
za kutaka kufanyiwa fujo kwa Mbunge huyo na watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa
Chadema.
Arfi alisema hatogombea tena Mpanda
Mjini; “Lakini nipo tayari kuvaa shati la kijani au la zambarau kumpigia debe
mgombea yeyote katika jimbo hili. Ninawajua Chadema na kama wakiendelea
kunifuatafuata, nitasema yote.”
Kauli hiyo ilitafsiriwa kuwa Arfi sasa
atafanya kampeni akiwa CCM au ACT Wazalendo dhidi ya Chadema katika Jimbo la
Mpanda Mjini, ambalo kabla yake halikuwahi kutawala na Mbunge mmoja kwa miaka 10
mfululizo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Arfi kuweka
hadharani mustakabali wake kisiasa, lakini kauli yake ya kuwa tayari kuvaa shati
la kijana inakwenda tofauti na fununu zilizozagaa mjini hapa kuwa huenda
akajiunga na ACT Wazalendo, chama kinachoongozwa na swahiba wake, Zitto
Kabwe.
Ikumbukwe kuwa mara baada ya Chadema
kutangaza kumvua nyadhifa zote Zitto takriban miaka miwili iliyopita, mara moja
Arfi alitangaza kuajiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema.
No comments :
Post a Comment