Lile Sakata la walimu wa Shule ya Msingi Nambaza, katika
Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, kufanyiwa vitendo vya kishirikina na kutishiwa
maisha, limeendelea kuumiza vichwa vya viongozi wilayani
humo.
Viongozi hao, leo wanatarajia kukutana katika kikao
ambacho kitamshirikisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Ofisa Utumishi na
Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo ili kujadili hatima ya walimu wa shule hiyo ambao
wote wamefungasha mizigo yao na kutoweka kijijini hapo wakihofia kuuawa na
baadhi ya ndugu wa watuhumiwa.
Kaimu Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo, Bw. Ruben Kaswamila,
amesema kuwa kikao hicho pamoja na mambo mengine, pia kitajadili tukio zima la
Nambaza ambalo ni la aibu na kushangaza ili kuangalia uwezekano wa kuwahamisha
walimu wote wageni na kuwapangia vituo vingine.
"Kesho (leo) tutakuwa na kikao ambacho kitamhusisha
Mkurugenzi, Ofisa Utumishi na mimi Kaimu Ofisa Elimu ili kujadili suala zima la
Nambaza na hatima ya walimu wa shule hiyo
waliodhalilishwa.
"Mwelekeo wa kikao ni kuwahamisha walimu wote wageni
na kuwapangia vituo vingine vipya vya kazi kwani kuendelea kuwaacha hapo ni
kuwahatarishia maisha maana hata kisaikolojia hawawezi kufundisha shuleni hapo
kwa ufanisi," alisema.
Alisema uhamisho huo hautawahusu walimu watatu wa shule
hiyo, Bw. Sospeter Mafuru ambaye ni Mwalimu Mkuu, Bw. Medard Munaku anayestaafu
Juni, 2016 na Bw. Renatus Molla ambaye naye anastaafu Februari, 2016 ambao ni
wazaliwa wa kijiji hicho ambao watabaki hapo shuleni kuwafundisha
watoto.
Aliongeza kuwa, Serikali ya kijiji na wanakijiji kwa
ujumla watatafuta wenyewe walimu ili waongeze nguvu shuleni
hapo.
"Kwakuwa wanakijiji ndio waliosababisha hayo,
watafute wenyewe walimu wa kuwafundishia watoto wao kama ni wanafunzi
waliomaliza kidato cha nne na cha sita wakubaliane, mshahara wawalipe wao kwa
sababu walimu walioletwa na Serikali, hawahitajiki kijijini,"
alisema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walimu wazawa
kijijini hapo ambao inadaiwa ndio watabaki kufundisha watoto, walisema hawako
tayari kurudi kufundisha shuleni hapo na kama mwajiri alikuwa na mpango wa
kuwafukuza kazi afanye hivyo si kurudi Nambaza.
Bw. Mafuru alisema jana alifuatwa na watu ambao
walimtukana, kumtemea mate na kutishia kumuua tukio ambalo ameliripoti polisi
sasa kwanini aendelee kukaa kijijini hapo.
"Mimi ni mzawa wa kijiji hiki lakini ni mtumishi wa
Serikali kama walivyo watumishi wengine, utumishi wangu ndio umesababisha
nitendwe vibaya, nitishiwe kuuawa na kuonekana sifai na adui miongoni mwa
wanakijiji, natishiwa sasa iweje niendelee kuwepo
kijijini.
"Nambaza sitakiwi tena nitauawa, uhai wa maisha
yangu ni bora kuliko kazi, kama mwajiri anataka kunifukuza kazi afanye hivyo
lakini siwezi kurudi Nambaza kufundisha," alisema.
Kwa upande wake, Molla alisema, hawezi kurudi
kufundisha Nambaza kwani amevumilia mengi pamoja na kumpoteza mtoto wake katika
mazingira ya kishirikina lakini bado anatishiwa kuuawa hivyo ni bora afukuzwe
kazi akafanye shughuli nyingine kama mwajiri anaona kumbakiza kijijini hapo
atakuwa amemtendea haki kwa sheria za utumishi.
"Sitarudi Nambaza, nipo tayari kufukuzwa kazi,
mizigo na familia yangu nimeitoa Nambaza baada ya kutendwa vibaya na wanakijiji,
nimetishiwa kifo na hao hao wanakijiji, kurudi hapo ni kwenda kufa, siwezi
kufuata kifo ninachokiona hadi Mwenyezi Mungu atakapoamua,"
alisema.
Aliongeza kuwa, mwaka 2014 mwanaye alikufa katika
mazingira ya kutatanisha kishirikina kwani hakuugua bali alianguka njiani
akitembea na kufa papo hapo.
Mwalimu Munaku, ambaye tayari amekwishajiondosha
kijijini hapo akihofia kuuawa kutokana na vitisho kutoka kwa wanakijiji,
hakuweza kupatikana ili kuzungumza kama yuko tayari kuendelea kufundisha shuleni
hapo ama la.
No comments :
Post a Comment