Dodoma. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime amewataka wageni wasiokuwa na shughuli muhimu ya kufanya mkoani hapa kutokuja katika kipindi cha juma hili ili kuepusha usumbufu utakaojitokeza.
Misime alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu wiki hii ambayo inatarajiwa kuwa na ugeni mkubwa wa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM ambao amesema kuwa unakadiriwa kuwakusanya watu takribani 10,000.
Alisema ili kuepusha usumbufu utakaojitokeza kama vile kukosa mahali pa kulala, ni vyema kama mtu hana shughuli ya muhimu ya kufanya mjini hapa asije mpaka mkutano huo utakapokwisha.
“Kuna wengine wanataka kuja kwa ajili ya ushabiki tu au kuja kushuhudia tukio zima na hata kama hawatakuja haitawaathiri kitu hivyo ni vyema wasije ili kuepusha usumbufu,” alisema Misime.
Alisema Jeshi la Polisi limejipanga kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi wote watakaofika katika mkutano huo na kuwataka wananchi kutoa taarifa za viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
Aliwataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni kuhakikisha kuwa vitu vyote vyenye thamani vya wateja wao vinatunzwa vizuri ili kuepusha usumbufu au kupotea kwenye mikono yao.
Ulinzi mkali bungeni
Jana, Polisi waliimarisha ulinzi bungeni kwa kuongeza idadi ya askari na pia kufunga kipande cha barabara kuanzia kwenye mzunguko wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani kupitia eneo la Bunge hadi mwanzo wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Tawi la Dodoma.
Kulikuwa na idadi kubwa ya polisi wa usalama barabarani, utepe mweupe uliofungwa katika barabara hiyo huku kukiwekwa kibao kilichoandikwa kwa maandishi mekundu, “barabara hii imefungwa.”
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime (pichani) alisema kufungwa kwa barabara hiyo ni miongoni mwa shughuli za usalama.
No comments :
Post a Comment