Dodoma. Historia inaelekea kujirudia, kama ilivyokuwa wakati Rais Jakaya Kikwete akizindua Bunge la 10 na wabunge wa Chadema kususia hotuba yake, ndivyo itakavyokuwa atakapolihutubia Bunge kwa mara ya mwisho Alhamisi bila kuwapo wabunge hao na wenzao kutoka NCCR – Mageuzi na CUF wanaounda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB).
Wabunge wa Chadema wakati huo wakiunda KUB peke yao, walisusia hotuba ya Rais Kikwete Novemba 30, 2010 wakipinga matokeo ya uchaguzi uliomweka madarakani.
Kiongozi wa KUB, Freeman Mbowe alisema jana kwamba wabunge wanaounda kambi hiyo hawatahudhuria vikao vilivyosalia kwa sababu ya Serikali kupitisha miswada mitatu ya petroli na gesi kinyume cha kanuni na sheria.
“Miswada hii inahitaji umakini mkubwa kabla ya kuigeuza kuwa sheria,” alisema Mbowe na kufafanua kuwa utaratibu uliotumika utazaa sheria mbaya.
Alisema KUB na viongozi wote wa vyama vinavyounda Ukawa walikubaliana kuishauri Serikali, uongozi wa Bunge na wabunge wa CCM wasiwe na haraka katika kuipitisha miswada hiyo lakini hawakusikilizwa.
Mbowe alisema walikubaliana kuiacha miswada hiyo ipitishwe na Bunge la 11 litakaloanza Novemba ili kufanya uchambuzi wa kina kwa kuzingatia masilahi mapana ya Taifa.
“Tunatambua kuwa pamoja na maudhui mengine katika miswada hii, kuna kipengele muhimu ambacho kinalazimisha mikataba yote iliyosainiwa awali, ya gesi na mafuta, isibatilishwe.
“Mikataba ambayo leo hii ipo katika utekelezaji imekuwa ikilalamikiwa na watu wengi kuwa ina mapungufu makubwa na hivyo inalikosesha Taifa mapato mengi,” alisema Mbowe katika mkutano uliohudhuriwa pia na baadhi ya wabunge wa CUF na Chadema.
Alisema kwa sababu uongozi wa Bunge umewadhalilisha kwa kuwatoa wabunge 43 bungeni kinyume cha taratibu, ni dhahiri ulikusudia kuipitisha miswada yote bila kujali ushauri.
Mbowe alisema uongozi unaomaliza muda wake una agenda ya siri inayoufanya kulazimisha sheria hizo kupitishwa katika utaratibu huo.
“Sisi wabunge wa Ukawa tumeshauriana na viongozi wengine wa vyama vyetu, tumeona hatuna sababu ya kuendelea kuwapo ndani ya Bunge, kushiriki katika kutunga sheria ambazo zitakuwa na athari kwa Taifa. Ni kwa misingi hiyo, sisi wabunge wa Ukawa leo (jana) ndiyo mwisho katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Vyama kukutana leo
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema alisema chama hicho kimeitisha Kamati Kuu leo na vyama vingine vimeita vikao kwenye vyama vyao kujadili suala hilo kabla ya kesho kufanya mkutano wa wabunge wote wa Ukawa na viongozi wakuu wa vyama hivyo.
Alisema lengo la kikao hicho ni kupeana taarifa ya nini kinaendelea ili azma yao ya kulipeleka suala hilo kwa wananchi iweze kuwekewa utaratibu wa utekelezaji.
Kanuni zilizovunjwa
Waziri Kivuli na Katiba na Sheria, Tundu Lissu alisema jambo la kwanza lililokiukwa katika kupitisha miswada hiyo ni utaratibu wa kanuni za kuitangaza katika Gazeti la Serikali.
Alisema Kanuni ya 80 inasema kila mswada wa sheria wa Serikali utatangazwa katika gazeti angalau katika matoleo mawili kukiwa na muda usiopungua siku saba kati ya toleo la kwanza na la pili lakini miswada hiyo ilitangazwa Mei 29 na mara ya pili Juni Mosi, ikiwa ni tofauti ya siku tano tu.
Alisema pia kuwa mswada unatakiwa uwasilishwe, ujadiliwe na kupitishwa kabla miswada mwingine, lakini kilichofanyika ni kusoma yote na kuijadili kwa pamoja.
Alitaja pia Ibara ya 98 ya Katiba kuwa imekiukwa kwa kuwa inataka mswada wa sheria unaohusu Muungano kuungwa mkono na theluthi mbili ya kila upande, jambo ambalo halikutakiwa.
Lissu alisema wanapinga sehemu ya miswada hiyo inayosema kuwa masuala yanayohusu fedha (mikataba) hayatabadilishwa na Bunge kwa kipindi kisichopungua miaka mitano tangu kupitishwa kwa sheria hiyo.
“Kifungu kingine tunachokipinga ni cha 261(3) ambacho kinasema mikataba ya mafuta na gesi itaendelea kuwa halali chini ya sheria hii hadi muda wa mikataba hii itakapoisha,” alisema.
Waziri Kivuli, Sera, Uratibu na Bunge, Rajab Mbarouk Mohamed, alisema neno Zanzibar katika miswada hiyo limetajwa mara moja tu na kuwa sehemu hiyo ya Muungano haijashirikishwa kwenye kipengele cha ukusanyaji wa mapato yanayotokana na gesi na mafuta.
Ulinzi mkali bungeni
Jana, Polisi waliimarisha ulinzi bungeni kwa kuongeza idadi ya askari na pia kufunga kipande cha barabara kuanzia kwenye mzunguko wa kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani kupitia eneo la Bunge hadi mwanzo wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Tawi la Dodoma.
Kulikuwa na idadi kubwa ya polisi wa usalama barabarani, utepe mweupe uliofungwa katika barabara hiyo huku kukiwekwa kibao kilichoandikwa kwa maandishi mekundu, “barabara hii imefungwa.”
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema kufungwa kwa barabara hiyo ni miongoni mwa shughuli za usalama.
Source: Mwananchi
No comments :
Post a Comment