Kama kuna msamiati mgumu kwangu, ni huu ninaousikia na kuusoma mara kwa mara kuwa kuna nyumba za bei nafuu hapa nchini.
Tena wakati mwingine tunaaminishwa kuwa nyumba hizi ni maalumu kwa watu wa kipato cha chini.
Kwa maneno mengine, watu wa kipato cha chini wa Tanzania aina ya nyumba zao ni hizi zinazoitwa za bei nafuu ambazo hivi sasa zinajengwa kwa wingi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hata hivyo, kila ninapofuatilia bei za nyumba hizi utakuta zinauzwa kuanzia Sh40 milioni na kuendelea juu.
Kwa hakika tangu nianze kusikia msamiati huu sijawahi kusikia benki, taasisi au shirika au kampuni inayojenga nyumba hizo kwa bei chini ya Sh20 milioni.
Mimi si mchumi ila kwa sura hii napata kujua kumbe mtu wa kipato cha chini hapa Tanzania ninayemjua si huyu anayekusudiwa katika miradi ya nyumba hizi.
Kama kweli wanaokusudiwa ni hawa wenye uwezo wa kununua nyumba za Sh40 milioni, Sh50 milioni na kuendelea, nashangaa iweje Tanzania iendelee kuwa katika kundi la nchi zenye wananchi wengi wa kipato cha chini.
Mimi binafsi kila ninapotamani kufuatilia angalau nami nibahatike kununua ‘mjengo’ wangu, navutwa shati na kima cha bei, nitazitoa wapi Sh40 milioni au zaidi?
Naamini siko peke yangu, msamiati huu unawatatiza wengi, na nimeshawasikia watu wakihoji mantiki ya kuziita nyumba hizi za bei ya chini.
Watanzania tuwe wakweli, hata kama mashirika yanayojenga nyumba hizi yanadai kutupa mkopo wa miaka 10 na zaidi, Sh40 milioni si kima anachoweza kumudu mtu wa kipato cha chini ambaye wengi tunamjua kwa viwango vya Kitanzania.
Shuleni sikuwa mzuri wa hesabu lakini sidhani kama nitashindwa kujua kiasi gani kwa mwezi anapaswa kulipa mtu wa kipato cha chini anayekopa tuseme nyumba ya ‘kimasikini’ ya Sh40 milioni.
Tuchukue mkopo huo ni wa miaka 10, tuachane na riba tubaki katika kima cha msingi. Miaka 10 ni sawa na miezi 120, ili masikini alipe mkopo huu atalazimika kulipa Sh333,333 kwa mwezi. Loh! mtu gani wa kipato cha chini hapa nchini mwenye uwezo wa kulipa kiasi hiki kwa kila mwezi?
Kwa mtazamo wangu, huyu katu hawezi kuwa mtu wa kipato cha chini, atakuwa mtu mwingine sijui jina lake.
Ni kwa sababu hii napata ugumu kuamini kama nyumba hizi zinawalenga kina ‘yakhe’ ambao ndiyo wengi Tanzania.
Nilitarajia kuona nyumba zinazojengwa wanakopeshwa watu kama mamantilie, machinga na wengineo, ila kwa nyumba hizi za sasa watu hawa watazisikia tu katika ‘bomba.’ Jambo la ajabu zaidi watu hawa si tu hawawezi kuzinunua lakini hata uwezo wa kupanga hawana kwa zile zinazopangishwa.
Tuwe wakweli, nyumba hizi si za watu wenye kipato kidogo, tubadilishe ukakasi uliopo katika msamiati huu kwa kuubadiilsha maana.
Pengine kwangu jina mwafaka hizi tungeziita nyumba za watu wa kipato cha juu, maana ndiyo wenye uwezo wa kulipa zaidi ya Sh300,000 kwa mwezi.
Kwa mazingira ya Kitanzania, hata tunaowaita wananchi wa kipato cha kati, wengi wao ni muhali sio tu kumudu kununua nyumba ya Sh40 milioni lakini hata kwa utaratibu wa kukopa.
Nasisitiza kuwa anayeweza kulipa mkopo wa nyumba wa zaidi ya Sh300,000 kwa mwezi si mtu wa kipato cha chini.
Pengine nitoe rai kwa waungwana hawa wanaojenga nyumba hizi, wakimaliza waanze basi kujenga japo vibanda kwa watu wa makundi ya kipato cha chini, kwani hata muuza mahindi ya kuchoma barabarani naye anahitaji kupata stara ya makazi.
CHANZO: Mwananchi
No comments :
Post a Comment