SERIKALI imewataka wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya
juu ambao bado hawajapata ajira kutoa taarifa kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu
(HESLB).
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Kazi
na Ajira, Gaudentia Kabaka, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kasulu
Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi).
Katika swali lake, Machali alitaka kujua Serikali
inawasaidia vipi Watanzania wanaodaiwa mkopo na Bodi ya Mikopo lakini hawana
ajira mpaka sasa.
Kabaka alisema mwanafunzi anapomaliza elimu ya juu
hupewa mwaka mmoja wa kujipanga na kutafuta kazi kabla ya kuanza kulipa deni
lake.
“Baada ya hapo kama anakuwa bado hajapata ajira
atatakiwa kwenda kutoa taarifa Bodi ya Mikopo kwa kuwa asipofanya hivyo akianza
kulipa atalipa pamoja na riba ya asilimia 10,” alisema.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti
Maalumu, Christowaja Mtinda (Chadema), Naibu Waziri wa Kazi, Dk. Makongoro
Mahanga, alisema jumla ya mikopo iliyotolewa kuanzia mwaka 1994/95 hadi 2013/14
ni Sh trilioni 1.8 kwa wanufaika 291,582.
Hadi kufikia Aprili 30, 2015 mikopo ya Sh bilioni 70.83
ilikuwa imerejeshwa kwa wanufaika 136,803 kati ya wanufaika 177,017 ambao mikopo
yao imeiva.
“Jumla ya wanufaika 40,214 ambao wanadaiwa Sh bilioni
94.12 hawajaanza kurejesha mikopo, jumla ya wanufaika 114,565 waliokopeshwa Sh
bilioni 973.7 mikopo yao haijaiva hivyo haijaanza kurejeshwa kwa sababu
wanufaika ama bado wanaendelea na masomo vyuoni na wengine wako kwenye kipindi
cha matazamio,” alisema.
Katika swali lake, Mtinda alitaka kujua mpaka sasa Bodi
ya Mikopo imeshakusanya kiasi gani na bado inadai kiasi
gani.
No comments :
Post a Comment