Friday, August 7, 2015

NEC: MARUFUKU KUPIGA KAMPENI NYUMBA ZA IBADA

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jji Mstaafu, Damian Lubuva akizungumza na wanahabari juu ya mambo yahusuyo tume hiyo.
WAKATI joto la uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu likizidi kupanda, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeviagiza vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa kisheria, kutoendesha kampeni zao katika nyumba za ibada.

Rai hiyo imetolewa na Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega alipozungumza na waandishi wa habari jana katika Ofisi ya Tume hiyo mjini hapa. Alivitaka vyama hivyo kuzingatia maadili kama ilivyokubaliwa na vyama vyote 22 na ambayo viongozi wake waliridhia na kusaini mbele ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Mbali na nyumba za ibada, NEC pia imeviagiza vyama hivyo vya siasa, kutoendesha kampeni zao katika taasisi za umma kama vile vyuo vikuu. Kwitega alisema NEC ni chombo huru, ambacho hakifungamani na chama chochote cha siasa na kwamba jukumu lake ni kusimamia kwa uadilifu wa hali ya juu masuala ya Sheria za Uchaguzi nchini.

Mbali na nyumba za ibada na taasisi za Serikali, pia alivitaka vyama vya siasa kuepuka kutumia lugha za matusi kejeli na kashfa wakati wa kampeni, huku akivihimiza kunadi sera zake mbele ya wananchi pamoja na yale ambayo chama husika kimetekeleza ama kinatarajia kutekeleza.

Alisema NEC itasimamia maadili ambayo yamekubaliwa na vyama vyote vya kisiasa vyenye usajili wa kudumu. Aidha, Kwitega alivitaka vyama vya siasa kutowatumia viongozi wa madhehebu ya dini, kuendesha kampeni zao katika madhehebu yao.

Alisema kwamba maeneo ya ibada ni kwa ajili ya kuabudu, sio kuendesha kampeni za kisiasa. Pazia la kampeni kwa vyama vyote, zinazotarajiwa kufanyika kwa miezi miwili, linatarajiwa kufunguliwa Agosti 22.

No comments :

Post a Comment