Thursday, August 6, 2015

TAARIFA YA WIZARA KUHUSU KUNYANYASWA OFISINI KWA KUVAA HIJAB

AMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA


WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO


Gazeti la kila wiki la Imaan la Agosti 3-9, 2015 Toleo Na.022, lilichapisha habari katika ukurasa wake wa pili yenye kichwa cha habari: “Watatu wasimulia walivyonyanyaswa kwa hijab Serikalini.”

Katika habari hiyo mwandishi alieleza kuwa baadhi ya watumishi wa umma ambao wanavaa mavazi kulingana na imani za kidini wananyanyapaliwa na kunyimwa safari. Ilieleza kuwa baadhi ya taasisi za Serikali (alizitaja) ikiwemo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo zinawanyanyapaa wafanyakazi wa kike wanaovaa mavazi aina ya hijab ambayo ni maarufu zaidi kuvaliwa na wanawake waumini wa dini ya Kiislamu.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haina dini hivyo siyo kweli kwamba Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imekuwa ikiwakataza wanawake wa Kiislamu kuvaa hijab kama ambavyo mwandishi alieleza katika habari hiyo.

Kimsingi habari hiyo ni ya kizusha na yenye lengo la kupandikiza chuki baina ya jamii yenye imani ya dini ya Kiislam dhidi ya Serikali yao. Hata hivyo, mwandishi ameandika habari hiyo bila kupata maoni au maelezo upande wa pili unaotuhumiwa kwa maana ya uongozi wa taasisi alizozitaja kwamba zinawazuia wanawake kuvaa hijab badala yake ametumia maelezo ya upande mmoja unaolalamika.

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inafuata mwongozo wa Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 3 wa mwaka 2007 kuhusu mavazi kwa watumishi wa Umma. Waraka huo umeainisha mavazi ambayo hayafai kuvaliwa katika ofisi za umma kwa wanawake na wanaume; aidha umeelekeza aina za mitindo ya nywele isiyofaa pamoja na aina za viatu visivyofaa.

Mifano ya mavazi yasiyokubalika kwa watumishi wa umma wanawake ni kama vile nguo zinazobana, nguo fupi ambazo zinaacha magoti wazi, nguo ambazo zinaacha sehemu ya mwili wazi kama vile kitovu na kifua, nguo ambazo zina picha, michoro, na maandishi ambayo hayaendani na shughuli za Serikali, kaptura aina yoyote ile kama vile pedo na pensi, nguo zinazoonyesha maungo ya mwili (transparent), suruali za ‘Jeans’, na nguo zingine zote zenye kukinzana na maadili ya utumishi wa umma na jamii kwa ujumla.

Aidha, kwa upande wa wanaume mavazi yasiyokubalika ni pamoja na nguo ambazo ni za kazi maalum kama vile michezo (hizi zivaliwe wakati wa shughuli hiyo tu), nguo ambazo zina michoro, maandishi na picha ambazo haziendani na shughuli za Serikali, nguo zinazobana, kaptura ya aina yoyote, suruali yoyote inayoachwa bila kupindwa, suruali za “Jeans” na Fulana “T-shirts” (Hizi zivaliwe tu wakati wa shughuli maalum inayotambulika), Kikoi au msuli, nguo zenye maandishi ya chama chochote cha siasa na yenye kuonyesha ushabiki wa kitu fulani.

Pamoja na kuwepo kwa miongozo ya mavazi yanayostahili kwa watumishi wa umma, tafsiri ya mavazi ya heshima hutegemea mila na desturi ya jamii husika. Katika utumishi wa umma mavazi ya heshima kwa mtumishi wa umma ni yale ambayo yanazingatia mila na desturi za taifa letu.

Kwa kutambua kuwa kila mmoja wetu ana imani yake na anao uhuru wa kuamini katika dini yoyote ni vyema sisi wenye dhamana ya kuhabarisha umma tukaepuka kueneza habari za chuki dhidi ya imani nyingine au Serikali kwani kufanya hivyo kutasababisha utengano miongoni mwa jamii, badala ya kuleta umoja na mshikamano kwa ustawi wa Taifa letu.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

No comments :

Post a Comment