Dar es salaam: MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imeshindwa
kumsomea maelezo ya awali Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima
na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya matusi na kushindwa
kuhifadhi silaha.
Kesi hiyo ilitajwa jana kwa ajili ya washitakiwa
kusomewa maelezo ya awali lakini iliahirishwa kwa kuwa Hakimu Mkazi Wilfred
Dyansobera anayesikiliza kesi hiyo hakuwepo mahakamani.
Hakimu Mkazi, Thomas Simba aliahirisha kesi hiyo hiyo
Julai 20, mwaka huu kwa ajili ya washitakiwa hao kusomewa maelezo ya awali mbele
ya Hakimu Dyansobera.
Mbali na Gwajima washitakiwa wengine, ni Mlinzi wake,
George Mzava, Msaidizi wake, Yekonia Bihagaze (39) na Mchungaji Georgey Milulu
(31) wanakabiliwa na shitaka la kukutwa na silaha pamoja na risasi kinyume cha
sheria.
Katika kesi ya kwanza namba 85, Gwajima anadaiwa kati
ya Machi16 na 25, mwaka huu katika Viwanja vya Tanganyika Packers Wilaya ya
Kinondoni Dar es Salaam alitoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu wa Kanisa
Katoliki Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akimueleza Askofu kwamba ni mtoto,
mpuuzi asiye na akili katika namna ya kwamba ingeleta uvunjifu wa
amani.
Katika kesi nyingine namba 84 , Gwajima anakabiliwa na
mashitaka ya kushindwa kuhifadhi silaha na risasi jambo ambalo ni kinyume cha
sheria ya uhifadhi wa silaha za moto.
Anadaiwa kati ya Machi 27 na 29, mwaka huu, ndani ya
Jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, alishindwa kuhifadhi silaha aina ya Beretta namba
CAT 5802, risasi 3 za pisto na risasi 17 za shotgun.
No comments :
Post a Comment