Mmoja wa majeruhi waliyopigwa risasi ,Ramadhani Hija Hassan akiwa katika kituo cha afya cha AL-Rahma kwa ajili ya kupatiwa matibabu .Alipigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura cha Shehia ya Nganani Mjini Magharibi, Unguja jana.Picha na Talbu Ussi. |
Zanzibar. Wakati watu watano wakijeruhiwa, wawili kwa kupigwa risasi, kwenye uandikishaji wa wapigakura eneo la Makunduchi, mkutano baina ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar na wadau umevunjika kutokana na mzozo wa mgwanyo wa majimbo.
Vurugu hizo zimetokea baada ya watu waliokuwa wamekusanyika katika Msikiti wa Kubini kwa madhumuni ya kupinga kazi hiyo ya uboreshaji wa Daftari la Wapigakura wakituhumu kuwapo kwa mamluki waliokuwa wakiandikishwa, lakini wakajikuta wakivamiwa na kundi la askari wasiokuwa na sare ambao walikuwa na silaha za moto.
Waliojeruhiwa kwa risasi ni Kheri Makame Hassan (42) na Ramadhani Hija Hassan (29) wote wakazi wa Makunduchi wakati Ali Seif Issa (38), Ali Hassa Hassan (70) kutoka Paje akiwa amepigwa kwa magongo na nondo na kuumia vibaya miguuni, na Hassan Ali Ameir (43).
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti hospitalini hapo, majeruhi wao walisema walikuwa katika kituo cha Nganani, Shehia ya Nganani Kusini Unguja ndipo walipokuja watu waliovaa vinyago na kuwaamuru waondoke eneo hilo wakati uandikishaji ukiendelea.
“Ilikuja gari na watu waliojifunika nyuso zao wakatuambia tuondoke na sisi tukakataa kwa sababu tulikuwa tunazuia kuandikishwa mamluki katika eneo letu. Baada ya kubishana pale wakaenda kuchukua gari nyingine wakaanza kutupiga,” alisema Kheri ambaye amepigwa risasi ya pajani.
“Watu waliojifunika nyuso walikuja mara mbili na kuondoka kabla ya kufanya shambulio na kufanikiwa kuondoka katika eneo la tukio la Nganani kwa kutumia magari mawili,’ alisema Faki huku akilalamika kusikia maumivu.
Shuhuda wa tukio hilo, Ameir Mussa, mkazi wa Makunduchi, alisema kwamba waliamua kukusanyika eneo la msikiti wakitafakari jinsi ya kuzuia uandikishaji wa wapigakura mamluki, ambao ni pamoja na walio na umri mdogo.
“Lilikuja kundi la watu mara mbili na kuondoka. Walikiwa wamefunika nyuso zao na waliporudi kwa mara ya mwisho walitushambulia kwa kutumia silaha za kienyeji na baadaye kufyatua risasi za moto na kujeruhi watu wawili,” alisema Mzee Ameir.
Daktari wa zamu wa Hospitali ya Al Rahma, Seif Suleiman alithibitisha kupokea majeruhi na kusema kwamba katika hatua za awali wanazuia damu kuvuja kutoka kwenye majeraha.
Alisema wanaendelea na vipimo ili kujua majeraha hayo yamesababishwa na nini. “Tumewafanyia x-ray ili kujua majeraha yao yanatokana na nini lakini yanaonesha wazi kuwa ni majeraha kama ya risasi kwa kuwa risasi jeraha lake linakuwa ni kitobo kidogo inapoingia lakini kitobo kikubwa inapotokea risasi.” Dk Suleiman alisema majeruhi hao wanaendelea vizuri baada ya kutibiwa na wengine wataruhusiwa watakapopata nafuu.
“Wapo walioumia sana hao wataendelea kuwepo hospitali kwa sababu wametokwa damu nyingi sana na kutoka Makunduchi hadi Mjini ni mbali kwa hivyo wanahitaji kupumzishwa kwanza hadi hapo watakapopata nafuu,” aliongeza Dk Suleiman.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Saadi alisema kuwa katika mkoa wake kuna uandikishaji wananchi kuwaingiza kwenye Daftari la Wapigakura, lakini hana taarifa za watu kupigwa risasi na kwamba anachojua ni risasi hizo kupigwa hewani na hivyo hazijajeruhi mtu.
“Taarifa nilizonazo ni kwamba polisi wamerusha risasi juu kwa bahati mbaya wakati wakijitayarisha kuweka sawa vifaa vyao,” alisema Kamanda Saad.
Hata hivyo, Kamanda Saad aliahidi polisi kufanya upelelezi wa kina ili kujua ni kina nani wanahusika na urushaji wa risasi hizo ambazo zimewajeruhi wananchi waliokuwepo katika eneo hilo la uandikishaji wapigakura.
Majeruhi wao walipelekwa Hospitali ya Al Rahma na kupatiwa matibabu na habari zinasema hali ya mmoja wao si nzuri na amehamishiwa Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa matibabu zaidi.
Wakati huohuo, kikao baina ya ZEC, vyama vya siasa na wadau kilichokuwa kinafanyika jana kisiwani hapa, kilivunjika jana baada ya tume kushindwa kuwasilisha ripoti ya mgawanyo mpya wa majimbo ya uchaguzi.
Uchaguzi Mkuu umepangwa kufanyika Oktoba 25, lakini hadi sasa ZEC haijaweza kutangaza majimbo mapya, jambo lililozua mzozo kwenye kikao hicho kilichofanyika Hoteli ya Bwawani. Kikao hicho kilivujika baada ya mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha kumaliza kutoa utangulizi kuhusu hatua zilizofikiwa katika kazi ya kutayarisha mipaka ya majimbo. Alisema kimsingi ZEC tayari imeshamaliza kazi ya kufanya mapitio ya mipaka ya majimbo ya Zanzibar na kwamba wanatarajia kutoa taarifa rasmi wiki ijayo na kuwataka wadau wa uchaguzi kuendelea kuwa na subira wakati wakikamilisha kazi hiyo.
Jecha alisema kwamba kazi ya kupitia mipaka ya majimbo ilianza kufanyika Juni 9 mwaka jana na kuwapa nafasi wadau wa uchaguzi kutoa maoni yao na hatua iliyobakia ni kutangaza mipaka ya majimbo.
Hata hivyo, mwenyekiti wa chama cha AFP, Said Soud alisema kwamba anashangazwa na ZEC kushindwa kukamilisha kwa wakati mwafaka kazi hiyo na badala yake kuendelea kutoa ahadi.
“Wakati umefika wa kumshauri Rais wa Zanzibar kuvunja uongozi wa ZEC kwa sababu wanaonekana bado wanavutana na ndiyo maana wanapiga danadana katika kutoa taarifa ya ugawaji wa mipaka ya majimbo ya uchaguzi ya Zanzibar,” alisema Soud
Mwakilishi wa CCM, Rashid Ali alisema kitendo cha ZEC kuendelea kuchechemea kutoa taarifa ya mabadiliko ya mipaka kimeendelea kuathiri vyama vya siasa kwa wagombea kushindwa kuanza kufanya matayarisho ya wagombea ubunge na uwakilishi katika majimbo ya Unguja na Pemba.
“Kama majimbo ya uchaguzi ni ya wananchi, kwa nini ZEC mnashindwa kufanya kazi ya kupitia majimbo kwa muda muafaka wakati nyie ndiyo wasimamizi wa uchaguzi?” alihoji.
Mkurugenzi wa uenezi na mawasiliano ya umma wa CUF, Ismail Jussa Ladhu alisema wameshachoshwa kudanganywa na ZEC kuhusu taarifa ya mapitio ya mipaka ya majimbo ya uchaguzi, akielezea kuwa kitendo hicho ni usanii.
Alisema kwamba ZEC walitoa ahadi ya kutoa taarifa ya mipaka ya majimbo ifikapo Machi mwaka Huu, lakini walishindwa na kuendelea kutoa ahadi nyigine bila ya utekelezaji wake kuonekana, jambo ambalo halionyeshi umakini wa utendaji kazi wa tume hiyo.
Akizungumzia mkasa huo katibu mkuu wa Tadea alisema kwamba inasikitisha muda wa uchaguzi umekaribia lakini hadi sasa hawajui mgawanyo wa majimbo.
Miongoni mwa wadau waliyoshiriki Kikao hicho ni vyama vya siasa, na asasi za kiraia, vikosi vya ulinzi na taasisi za Serikali
No comments :
Post a Comment