Zikiwa zimebakia siku sita kwa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) kumpata mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka
huu, kura ya maoni iliyoendeshwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia
(REDET) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inamweka kileleni Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa, kuwa changuo la kwanza la wengi kwa kujipatia asilimia
27.0 ndani ya chama hicho.
Wakati Lowassa akiwafunika watia nia wenzake ndani ya
CCM, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, anawafunika wenzake kwenye Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akiwa changuo la wengi kwa asilimia
23.1.
REDET wamesema kuwa matokeo ya utafiti huo yanaweza
kuchukuliwa kwa ujumla wake kama maoni ya Watanzania endapo masuala yaliyoulizwa
uchaguzi ungefanyika katika kipindi cha utafiti.
“Sampuli iliyotumika katika utafiti huu kwa kiwango cha
kutosha ni wakilishi na ina akisi hali halisi ya Watanzania,” imesisitiza
ripoti hiyo iliyojatwa kuwa ni maoni ya wananchi kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao wa
Oktoba 2015, mwaka huu.
Katika utitiri wa watia nia ndani ya CCM, kati ya
wahojiwa 1,250 waliohojiwa, Lowassa alipigiwa kura na watu 338, wakati Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akipata asilimia 8.2
akichaguliwa na watu 103.
Utafiti wa REDET ulifanyika katika wilaya moja moja
kwenye mikoa 25 ya Tanzania Bara baada ya wahojaji kukataliwa ruhusa ya kufanya
utafiti wao katika mikoa mitano ya Zanzibar.
Utafiti huo uliokuwa umedhaminiwa na kampuni ya
Business Times Limited, ulifanyika kati ya Juni 23-26, mwaka huu na kila wilaya
ilikuwa na wahojiwa 50.
Kwa upande wa CCM watia nia wengine ni Mizengo Pinda
nafasi ya tatu akiwa na asilimia 7.2 akichaguliwa na watu 90; John Magufuli
nafasi ya nne akipata asilimia 6.6 akipigiwa kura na watu 83 na Charles
Makongoro Nyerere nafasi ya tano akipigiwa kura na watu 54.
Wengine ni Mark Mwandosya nafasi ya sita akipata
asilimia 3.1 akichaguliwa na watu 39; Dk. Harrison Mwakyembe nafasi ya saba
akiwa na asilimia 1.4 akichanguliwa na watu 18; Frederick Sumaye nafasi ya nane
akipata asilimia 1.4 akichaguliwa na watu 17; nafasi ya tisa imekamatwa na Jaji
Augustino Ramadhani akiwa na asilimia 1.2 akichaguliwa na watu 15 na nafasi ya
10 amekamata Mwigulu Nchemba akiwa na asilimia 1.0 akichaguliwa na watu
13.
Wengine na idadi ya waliowachagua na asilimia zao
kwenye mabano ni January Makamba nafasi ya 11 (asilimia 0.8, watu 10); Dk.
Asha-Rose Migiro nafasi ya 12 (asilimia 0.7, watu tisa); Samuel Sitta nafasi 13
(asilimia 0.6. watu wanane); Lazaro Nyalandu nafasi ya 14 (asilimia 0.4, watu
watano).
Pia wamo Prof. Sospeter Muhongo nafasi ya 15 (asilimia
0.4, watu watano); Balozi Amina Salum Ali nafasi ya 16 (asilimia 0.2, watu
wawili); Dk. Mohammed Gharib Bilal nafasi ya 17 (asilimia 0.2, watu watatu);
Stephen Wasira nafasi ya 18 (asilimia 0.2, watu 3) na William Ngeleja nafasi ya
19 (asilimia 0.2, watu wawili).
Wengine ni Balozi Ally Karume nafasi ya 20 (asilimia
0.1, mtu mmoja); Amos Siyantemi nafasi ya 21 (asilimia 0.1, mtu mmoja); Joseph
Chagama nafasi ya 22 (asilimia 0.1, mtu mmoja); na Mwele Malecela nafasi ya 23
(asilimia 0.1, mtu mmoja).
Katika kura hiyo, watia nia 14 ambao wamejitosa kwenye
urais kupitia CCM hawakutajwa kabisa na watoa maoni ambao ni Balozi Augustine
Mahiga; Boniphace Ndengo; Eldophonce Bihelo; Godwin Mwaipopo; Dk. Hamis
Kigwangalla; Dk. Hans Kitine; Joseph Chagana; Leons Mulenda; Luaga Mpina; Maliki
Marupu; Mathias Chikawe; Monica Mbega; Titus Kamani na Balozi Patrick
Chokala.
Kwenye kundi la Ukawa, namba mbili amechukua Prof.
Ibrahim Lipumba akiwa na asilimia 13.6 akichaguliwa na watu 170; Freeman Mbowe
ameshika nafasi ya tatu akiwa na asilimia 7.2 akichaguliwa na watu 90; James
Mbatia amekamata nafasi ya nne akiwa na asilimia 3.2 akichaguliwa na watu 40;
Emmanuel Makaidi akishikilia nafasi ya tano kwa asilimia 0.6 akichaguliwa na
watu 8, huku George Kahangwa akishika nafasi ya sita kwa asilimia 0.2
akichaguliwa na watu wawili.
SWALI LA MSINGI
Swali la msingi lililokuwa linaulizwa lilisema: “Kama
wewe leo ungeshirikishwa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi
ya CCM, kati ya wanachama wake 37 waliokwishajitokeza, ungemchagua nani
apeperushe bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Oktoba 2015?”
Pia swali kwa Ukawa lilikuwa: “Kama wewe leo
ungeshirikishwa katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kati ya wanachama wake
waliokwishakutangaza nia na wanaotarajia kutangaza nia ungemchagua nani
apeperushe bendera ya Ukawa katika uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Oktoba 2015?”
Ripoti ya REDET imesema kuwa kwa maswali yote, mhoji
alitakiwa kutomtajia majina mhojiwa, bali mhojiwa aliombwa ataje jina alilonalo
kichwani mwake.
REDET imesema kuwa katika utafiti wake ilikusudia
kupata maoni ya wananchi katika maeneo matatu; mosi, kupata maoni ya wahojiwa
kuhusu wanachama wa CCM wanaoomba kuteuliwa kuwania nafasi ya urais kwa tiketi
ya chama hicho; mbili, kupata maoni ya wananchi kuhusu wanachama wa vyama
vinavyounda Ukawa ambao wamejitokeza au wanafikiriwa kuwania nafasi ya urais
chini ya mwavuli wa Ukawa na tatu, kupata maoni ya wahojiwa kuhusu wanachama wa
vyama vingine vya upinzani vilivyo nje ya Ukawa wanaofikiriwa kwania nafasi ya
urais.
Katika kundi la vyama ambavyo havipo Ukawa, Zitto Kabwe
ameongoza kwa asilimia 8.5 akichaguliwa na watu 106, Chama cha Demokrasia Makini
kimepata asilimia moja kilichaguliwa na watu 13, John Cheyo ameibuka nafasi ya
tatu akiwa na asilimia 0.9 akichaguliwa na watu 12 na Augustine Mrema nafasi ya
nne akiwa na asilimia 0.7 akichaguliwa na watu wanane.
Wengine ni Chama cha ADC nafasi ya tano kikiwa na
asilimia 0.5 kikichaguliwa na watu sita na nafasi ya sita yupo Christopher
Mtikila akiwa na asilimia 0.5 akichaguliwa na watu sita pia.
WILAYA ZA KURA YA MAONI
Wilaya ambazo kura ya maoni iliendeshwa ni Longido,
Temeke, Dodoma Manispaa, Mbogwe, Kilolo, Muleba, Mlele, Ujiji Kigoma, Moshi
Manispaa, Lindi, Hanang, Bunda, Rungwe, Morogoro Manispaa, na
Msasi.
Nyingine ni Ilemela Manispaa, Ludewa, Kisarawe,
Kalambo, Namtumbo, Kahama, Itilima, Singida, Tabora Manispaa na
Muheza.
Ambako ruhusa haikupatikana ni Micheweni, Kaskazini B,
Mkoani, Kusini na Mjini A.
VIJANA ZAIDI WAJITOKEZA
Katika utafiti huo ambao ulitumia mfumo wa sampuli
nasibu (random sampling), vijana wengi zaidi walitoa maoni yao. Wahojiwa 334
sawa na asilimia 26.7 walikuwa kati ya umri wa miaka 36 – 45 na wengine 201 kati
ya miaka 18 – 25 wakiwa ni asilimia 16.1. Wahojiwa wachache yaani zaidi miaka 66
walikuwa ni 70 sawa na asilimia 5.6.
Wanawake katika wahojiwa walikuwa 626 sawa na asilimia
501, huku wanaume wakiwa ni 624 sawa na asilimia 49.9.
Asilimia 30 ya wahojiwa wote walitoka mijini, huku
asilimia 70 wakitoka maeneo ya vijijini.
VIPAUMBE SERIKALI AWAMU YA TANO
REDET wanasema kuwa wahojiwa walitakiwa kutaja
kipaumbele kimoja tu na mlolongo uliopatikana ni elimu asilimia 23.8 iliyotajwa
na watu 298; kilimo asilimia 14 watu 175, ajira asilimia 12 watu 150, afya
asilimia 9.9 watu 124, kupambana na rushwa asilimia 6.4 watu 80 na maji asilimia
5.4 watu 68.
Nyingine ni barabara iliyoshika nafasi ya saba
iliyopata asilimia 3.4 ikitajwa na watu 43, viwanda asilimia 3.3 ikitajwa na
watu 41 na mikopo na mitaji asilimia 2.6 ikitajwa na watu
33.
Vipaumbelea vingine na asilimia na idadi ya waliotaja
kwenye mabano ni umeme (asilimia 2.2, watu 28), kukomesha migogoro ya ardhi
(asilimia 1.5, watu 19), ujenzi wa makazi/ nyumba bora (asilimia 0.6, watu 7),
demokrasia (asilimia 0.6, watu 8), katiba inayopendekezwa (asilimia 0.3, watu
watu 4) na muungano (asilimia 0.1, mtu mmoja).
No comments :
Post a Comment