Saturday, July 4, 2015

"Bao la mkono" la Nape latua Tume ya Uchaguzi

Dar es Salaam. Kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye bado inawaumiza vichwa wapinzani nchini baada ya viongozi hao jana kuitamkia wazi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kuwa hakuna haja ya kujadili maadili wakati CCM tayari kimesema ‘kitafunga bao la mkono.’
Wakizungumza kwenye mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na viongozi wa vyama vya siasa kuhusu maadili ya Uchaguzi jana, baadhi ya viongozi hao walitaka mkutano huo usitishwe hadi pale CCM itakapomuonya Nape.
Wa kwanza kuibua mada kuhusu Nape, ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi ambaye alisema hakuna haja ya kuendelea na mkutano huo hadi NEC, Msajili wa Vyama vya Siasa na IGP wakemee kauli hiyo.
“Hivi tutayazungumziaje maadili, mbona CCM kimeshaonyesha kuwa hakitafuata maadili, kuna haja gani ya kuzungumzia wakati wameshasema watafunga hata kwa goli la mkono?” alisema Dk Makaidi.
Awali akiwa katika ziara ya Kinana wilayani ya Sengerema, Nape alikaririwa akisema kuwa ana uhakika CCM itashinda baada ya kuona mwitikio mkubwa wa Watanzania katika ziara hizo.
“Rangi inayoenda Ikulu ni hii (anaonyesha shati lake la kijani ambayo hutumiwa na chama hicho). Tuna uhakika na ushindi wa Rais. Kwa namna yoyote ile, CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono... bao ni bao tu ili mradi refa hajaona,” alisema Nape.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva aliwatoa wasiwasi wanasiasa hao akiwaambia kuwa Nec itafanya uchaguzi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu na hivyo kauli ya Nape haiwahusu.
“Maadili tunayoyatengeneza yataanza kutumika kuanzia Agosti 22, wakati wa kampeni, lakini iwapo kuna vurugu zinatokea baina ya vyama sisi wala Nec hatuhusiki,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa akichangia kipengele cha wahusika wa maadili aliitaka Nec kuliweka Jeshi la Polisi kupitia IGP kusaini na kuwa mhusika katika masuala ya maadili ya uchaguzi.
Hiki kipengele cha 1.3 kinawataja wahusika wa maadili kuwa ni vyama vya siasa, wagombea, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Nec pekee.
“Kutokana na uzoefu tulionao katka chaguzi zilizopita, Jeshi la polisi ni washiriki wakubwa katika masuala ya uchaguzi, kama jeshi hilo halitasaini maadili hayo basi kutakuwa na matatizo makubwa katika uchaguzi huo,” alisema.
Awali akifungua mkutano huo Jaji Lubuva alivitaka vyama vya siasa kufuata maadili, sheria na kanuni za uchaguzi, na katika kipindi chote cha kuanza kwa kampeni hadi siku ya uchaguzi.
Alisema kila chama na mgombea kitatakiwa kuheshimu na kutekeleza kanuni na sheria za uchaguzi, siku moja baada ya uteuzi wa mgombea ili kuepesha vurugu zinazotokea kipindi cha uchaguzi.
“Maadili tutakayojadili leo (jana), yatahusisha mambo mbalimbali yasiyotakiwa kufanywa na vyama vya siasa na wagombea wao kipindi cha kampeni hadi uchaguzi,” alisema Jaji Lubuva na kuongeza kuwa;
“Mfano kwa vurugu za aina yoyote katika mkutano wa chama kingine cha saiasa, sanjari na maadili yanatakiwa kufuatwa wakati wa upigaji kura hadi kutangazwa kwa matokeo.
Souce: Mwananchi

HUKUMU YA KESI YA BASIL MRAMBA NA WENZAKE KUTOLEWAJUMATATU


Hukumu ya kesi ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 inayomkabili Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba na wenzake imeahirishwa kwa mara ya pili kwa sababu hakimu anaumwa.
  
Kesi hiyo ilitajwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kusomwa kwa hukumu, baada ya kuahirishwa kwa mara ya kwanza Mei 30 mwaka huu.
  
Hata hivyo, Hakimu Mkazi, Saul Kinemela alisema hawezi kusoma hukumu hiyo kwa sababu Mwenyekiti anayeunda jopo la mahakimu watatu wanaosikiliza kesi hiyo, John Utamwa, hajafika mahakamani kwa kuwa anaumwa na amepewa siku mbili za mapumziko.
  
Hakimu Kinemela aliahirisha hukumu hiyo hadi Jumatatu ya Julai 6, mwaka huu. Hakimu mwingine katika jopo hilo ni Sam Rumanyika.
  
Mbali na Mramba washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.

Wabunge 11 Wa UKAWA Watimuliwa Bungeni Kisa Kupinga Muswada wa Sheria ya Petrol


Dodoma: Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Watanzania limewasimamisha wabunge 11 kwa kudharau mamlaka ya Spika jana.
  
Hatua hiyo ni baada Spika wa Bunge hilo, Anne Makinda, kuwashitaki katika Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, wabunge hao wa Kambi Rasmi ya Upinzani, wakiongozwa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi hiyo, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).
Makinda alichukua hatua hiyo, baada ya wabunge hao kurudia kwa mara ya pili kufanya vurugu na kupiga kelele wakati kikao kikiendelea na kumlazimisha kuahirisha kwa mara ya nyingine shughuli za bunge zilizokuwa zikiendelea bungeni mjini hapa.
“Bunge haliwezi kuendeshwa kwa kelele na vurugu namna hii. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, ninawataja kwa majina vinara wa vurugu ambao walitakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili na kulazimika kuahirisha Bunge hilo hadi jioni."
Hukumu ya Watuhumiwa
Kamati hiyo ilitoa adhabu kwa mafungu matatu ambapo wapo ambao hawakutoa ushirikiano kabisa kwa kamati hiyo wakidai wangefanywa hivyo mbele ya wanasheria wao, hao walifungiwa moja kwa moja, waliotoa ushirikiano kwa kamati wakafungiwa kutohudhuria vikao viwili na wengine waliochelewa kupata wito wanatakiwa kuhojiwa na kama leo asubuhi saa nne wakati mmoja hakuguswa na adhabu hizo kabisa.
Waliosimamishwa moja kwa moja ni Lissu, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Paulina Gekul (Chadema), Mbunge wa Mohambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Kasulu Mjini na Moses Machali (NCCR-Mageuzi).
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), Rashid Ally Abdallah (CUF) na Mbunge wa Gando, Khalifa Khalifa (CUF), hao wanatakiwa kufika katika kamati hiyo ya maadili leo kwa kuwa hawakupata wito wa kuitwa jana mapema huku Mbunge David Silinde hakuguswa kabisa katika adhabu hiyo.
Kundi la pili waliofungiwa vikao viwili, cha leo na Jumatatu ni Mbunge wa Ole, Rajab Mbaruk Mohamed (CUF) na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) ambao waliitikia wito na walitoa ushirikiano kwa Kamati hiyo ambayo Makamu Mwenyekiti wake ni Brigedia Hassan Ngwilizi, ambaye ni Mbunge wa Mlalo (CCM).
Akiwasilisha maamuzi ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa kamati alisema walifikia maamuzi hayo baada ya kuridhika baada ya kuwaita wahusika na kujieleza na hatimaye kufikia maamuzi hayo.
Kamati hiyo ambayo Makamu Mwenyekiti wake ni Kapteni John Chiligati, ambaye ni Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM) ilitoa maamuzi hayo kulingana kanuni za Bunge.
Ilivyokuwa
Vurugu hizo zilianza mara baada ya Lissu kusimama kuomba Mwongozo wa Spika, wakati Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alipokuwa akisoma kwa mara ya pili, muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesi wa mwaka 2015, ambao Kambi ya Upinzani ilikuwa ikiupinga tangu mwanzo.
Wakati wakipiga kelele, Spika alinyamaza na Simbachawene akaendelea kusoma muswada huo, ndipo wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani wote waliokuwepo bungeni wakasimama kumuunga mkono Lissu na kuwalazimu baadhi ya wabunge wa CCM kuanza kuwazomea na wao kurudisha maneno yaliyosababisha hata aliyekuwa akisoma asisikike.
Msimamo wa upinzani
Pamoja na yaliyotokea, kambi hiyo ilijikusanya ndani ya Bunge hilo kupeana misimamo ambapo, walisikika wakisema hata iweje, hawatakubali muswada huo wa Sheria ya Mafuta na Gesi upite.
Katika hatua nyingine, Spika Makinda alikataa kuendekeza malalamiko ya Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata (CCM), aliyeomba mwongozo na kudai kuwa, Mbunge wa NCCRMageuzi, Moses Machali alimdhalilisha kwa kumwambia kuwa, alifumaniwa na wajinga wenzake.
Machali alisema hivyo alipokuwa akitoa maoni ya muswada uliopitishwa wa Ulinzi wa Mtoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi, baada ya kukasirishwa na kitendo cha Mlata kuropoka kuwa Mbunge huyo aliyetaka adhabu iwe kunyongwa ni kichaa.
“Leo wote mmeonesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu, kwa kutoleana maneno yasiyofaa. Wengine mmekuwa mkiingilia hoja za wenzenu wakati wanaziwasilisha, kwa kuwatolea maneno yasiyo na adabu,” alisema.

ACT yailalamikia CHADEMA kuhujumu mikutano yake.


CHAMA cha Alliance for Change and Transparency(ACT), kimebaini kuwepo kwa mipango inayoratibiwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya kuhusika kuhujumu mikutano yake mbalimbali.
Hujuma hizo zimebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Mipango na Mikakati Taifa  wa ACT Habibu Mchange, aliyesema kuwa chama hicho kimekuwa kikihangaikia ACT na kusahau kushughulikia matatizo ya watanzania.
“Chadema wamekuwa wakitufuatilia kila mahali tunapofanya mkutano na hilo wamekuwa wakifanya kwa sababu ya kutuhofia. Kwa mfano tulipokuwa na mkutano Mwanza na wao wakatangaza kufanya tukawashinda, kesho tumetangaza kufanya mkutano na wao wametangaza kufanya Kawe.
“Chadema tunawaonea huruma kwa kuwa tutawafanya kitu ambacho hawatasahau katika historia ya siasa za tanzania kwa sababu njia nyingi wanazotumia ni zile tulizoziratibu wakati tukiwa huko,”alisema Mchange.
Katika hatua nyingine Mchage alisema baada mbalimbali mikoani hivi sasa ACT kupitia viongozi wake  wa kitaifa wameandaa kufanya mkutano mkubwa kesho jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mwembe Yanga.
“Mkutano huo utatoa fursa ya kuzindua Ilani ya jiji la Dar es salaam, itakayotokana na ilani Kuu  ya chama ili kukabiliana na kero mbalimbali za jiji.
“mkutano huo utatoa fursa ya ACT kuwataka watanzania kuishi katika misingi ya haki, undugu, umoja na mshikamano kwa kutumia azimio la Tabora lilozinduliwa na chama hicho likiwa limewisha azimio la Arusha,”alisema.
Chama hicho kinatarajia kusimamisha madiwani, wabunge na nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Akizungumzia tuhuma hizo msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alisema chama hicho hakina muda wa kuzungumzia tuhuma ambazo hazina mashiko.

Friday, July 3, 2015

Wanne hawakurejesha fomu za CCM kuwania Urais Tanzania 2015

 
Watu wanne waliochukua fomu za kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wagombea wa kiti cha urais wametoka rasmi katika mchakato huo, baada ya kushindwa kurudisha fomu hadi muda wa mwisho ulipofika saa 10.00 alasiri ya jana.
Watu hao ni 
  1. Peter Nyalali
  2. Helen Elinewinga
  3. Anthony Chalamila
  4. Dk Muzamil Kalokola
Jumla ya wanachama 42 walijitokeza kuchukua fomu hizo.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Rajab Luhwavi alisema zoezi la kuchukua fomu lilianza Juni 3, mwaka huu na lilitarajia kumalizika Julai 2, 2015.
“Mmoja wa wachukua fomu, Helena Elinawinga alitelekeza fomu hizo kwa mmoja wa maofisa wa CCM baada ya kufika kuomba ushauri huku akitaka kupewa kwanza elimu ya siasa kabla ya kuanza kutafuta wadhamini” 
Luhwavi alisema hatua itakayofuata ni mchakato wa vikao vya chama kuanzia Jumanne wiki ijayo.

 

Bunge Laahirishwa Ghafla Tena leo, baada ya Wapinzani kugomea Muswada wa Mafuta na Gesi Asilia

 
 
Dodoma: Waziri wa Nishati na madini George Simbachawene alipoanza kusoma kwa mara ya pili Muswada wa mafuta na gesi asilia (Muswada juu ya Petroli, 2015 The Petroleum Act, 2015), Tundu Lissu alisimama na kuomba Kuhusu utaratibu, Spika hakumpa nafasi, ndipo wabunge wote wa UKAWA Waliposimama na kuanza kupiga kelele wakisema Muongozo muongozo..!!.

Spika Kamuomba Waziri aliyekuwa anasoma Hotuba akakae kisha akawataja baadhi ya wabunge kwamba ndio wanaoleta fujo bungeni kwa kosa kutokana na kanuni ya kuleta fujo bungeni ambao ni:

1.John Mnyika Mbunge wa CHADEMA jimbo la Ubungo

2.Tundu Lissu Mbunge wa CHADEMA jimbo la Singida Mashariki

3.Ernest Silinde Mbunge wa CHAEMA jimbo la Mbozi Magharibi

4.Rashid Ali Abdalla mbunge wa CUF jimbo la Tumbe Zanzibar

5.Paulina Gekul Mbunge wa Viti Maalumu wa CHADEMA wa Mkoa wa Manyara

6.Moses Joseph Machali Mbunge wa NCCR-Mageuzi Jimbo la Kasulu Mjini

7.Rajab Mbarouk Mbunge wa CUF Jimbo la Ole Zanzibar

8.Felix Francis Mkosamali Mbunge wa NCCR Mageuzi jimbo la Muhambwe

9.Rev. Simon Peter Msigwa Mbunge wa CHADEMA jimbo la Iringa Mjini

10.Joseph Roman Selasini Mbunge wa CHADEMA jimbo la Rombo

11.Khalifa Suleiman Khalifa Mbunge wa CUF Jimbo la Gando Zanzibar

Bunge limesitishwa hadi watakapoitwa tena na Spika, vilevile kamati ya Maadili imeitwa kujadili hili Swala.