CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema hakitajitoa katika
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na kuwapo kwa vikwazo vya ugawaji wa
madaraka ndani ya umoja huo.
Akizungumza katika kikao cha Kamati Kuu cha chama hicho
kilichoketi jana katika Hoteli ya Travertine jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa
chama hicho, James Mbatia, alisema lengo la umoja huo lilikuwa ni kuunganisha
nguvu ili kuwa na sauti moja ya ushirikiano.
“Yapo maneno mengi yamesemwa na waandishi, wachochezi
wanasema NCCR inataka kuvunja Ukawa, tangu lini mama akakata mkono wa mtoto
wake?
“Kama kuna wenye wazo la sisi kujitoa kwenye umoja
huu ni vizuri watambue kuwa hatuna mpango huo, na hili ni azimio lililotolewa
na wajumbe wa Halmashauri Kuu. Pia itambulike kuwa chama hiki ni zao la Ukawa,
hivyo si jambo rahisi kujitoa,” alisema Mbatia.
Alisema Ukawa si sehemu ya kugawana madaraka na kudai
kuwa umoja huo unaangalia zaidi masilahi ya wananchi.
Mbatia alisisitiza pamoja na uchochezi uliopo na
changamoto ya ugawaji majimbo, wanaamini watavuka kwa kuwa lengo ni kusaidia
wananchi na si vyama husika.
Alisema umoja huo umejipanga vizuri, hivyo wananchi
wasiwe na wasiwasi kwakuwa wana uwezo wa kutoa rais pamoja na viongozi wengine
watakaounda Serikali.
Ajitosa Sakata la Zanzibar
Aidha Mbatia alishagazwa na hatua ya Rais wa Zanzibar,
Dk. Ali Mohamed Shein kuvunja Baraza la Wawakilishi juzi bila tukio hilo
kuhudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad baada ya
wabunge na wawakilishi kumkatalia kuhudhuria.
“Nimeshangaa sana rais wa Zanzibar anavunja Bunge
yupo mwenyewe bila Maalim Seif. Nini maana ya Serikali ya Umoja wa Kitafa?”
alihoji Mbatia.
Alisema wanachama wa vyama vya CCM na CUF wanapaswa kutambua kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni makubaliano na mali ya Wazanzibari wote na si wanasiasa pekee.
Akizungumzia kuhusu mwenendo wa uandikishaji wa daftari
la wapigakura unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kutumia mfumo
wa kielektroniki (BVR), alisema hakuna dalili za daftari hilo kukamilika kwa
wakati kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji.
Alisema kutokana na hali hiyo, kuna viashiria
vinavyoonyesha uchaguzi utakaofanyika Oktoba hautakuwa huru na wa
haki.
“Uchaguzi hautakuwa huru na haki kwa sababu wameshindwa
uandikishaji, kama leo wanasema kuna zaidi ya watu 5,000 wamejiandikisha mara
mbili, wanamaanisha nini kwa wananchi?
“Tulishauri tangu mwaka jana kuhusu utaratibu wa
uandikishaji na muda wa kuanza, lakini wenzetu wakawa wanabisha. Kwa hapa
tulipofikia lolote likitokea wa kulaumiwa ni Serikali ya CCM,” alisema
Mbatia.
Alisema hadi sasa kuna baadhi ya mikoa ikiwamo Dar es
Salaam na Pwani bado hawajaandikishwa. Pia NEC inapaswa kuwa na muda wa
kuhakiki majina ambako kutafanywa na wananchi.
Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya nne tangu
ilipoingia madarakani mwaka 2005 imekuwa ikipoteza mvuto siku hadi siku
kutokana na kutowajibika kwa ufasaha.
Alisema hadi sasa kuna mazingira ambayo mtu yeyote
makini ni rahisi kuona jinsi Serikali ya CCM ilivyopoteza utashi, mvuto na
mwelekeo wa kuongoza Watanzania.
No comments :
Post a Comment