MAKADA maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamerejesha
fomu na kufafanua mambo kadhaa ambayo yamekuwa yanazungumzwa juu yao kama njia
ya kujiweka sawa kabla ya uteuzi kufanywa na vikao vikuu vya chama
hicho. Waliorudisha fomu ni hawa wafuatao;
Mizengo Pinda
Mmoja wa waliorudisha fomu ni Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda ambaye wakati akirudisha fomu za kuomba kuteuliwa na kusema kuwa
wanaochukulia suala la urais ni la kufa au kupona wana matatizo kwani anayejua
Rais wa Tanzania ajaye ni Mungu.
Alisema safari yake ya kutafuta wadhamini ilikuwa na
misukosuko mingi ikiwemo kutokea ajali tatu lakini hakuna ambaye alikuwa ameumia
sana.
Akiwa ameongozana na mke wake, Tunu Pinda alisema mwana
CCM mkomavu ni yule ambaye yuko tayari kukubali matokeo.
Alisema mpaka sasa ni wanachama wa CCM 42 waliojitokeza
kugombea lakini katika hatua ya kwanza ni majina matano tu yatakayoteuliwa na
kundi kubwa litaondolewa.
“Mimi sitegemei kwenye mchujo wa watu watano watokee
watu wa kunung’unika kwani kila mtu aliyefika kuchukua fomu alikuwa anafahamu
kuwa kutakuwa na mchujo kama tuko wengi wako watano kisha unakwenda ngazi ya
pili, hakuna sababu ya kunung’unika,” alisema.
Alisema baadaye kuna kwenda kwenye Mkutano Mkuu atabaki
mmoja. “Utanung’unikia nini? Kuna kushinda na kushindwa na kuna kupata na
kukosa na ukisema suala la Urais ni kufa au kupona basi una matatizo, ifike
mahali wana CCM wapate mtu ambaye wanadhani anaweza kusaidia kuongoza,”
alisema.
Pia alisema waliojitokeza mwaka huu kuchukua fomu ni
wengi. “Tuliojitokeza tusinuniane, kwa nini haniungi mimi mkono, na wewe
usione jambo hili ni nongwa na usijione mapenzi ya Mungu yako kwako tu,”
alisema.
Pia aliwataka viongozi wenzake washirikiane kumuunga
mkono mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM. “Anayejua rais wa
Tanzania atakuwa nani ni Mungu peke yake,” alisema.
Mwakyembe arudisha fomu
Waziri wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe jana
alirudisha fomu na kusema CCM itapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba mwaka huu kutokana na kutekeleza ilani yake vizuri na
wananchi kuwa na imani kubwa na chama hicho.
Mwakyembe ambaye alirudisha fomu jana mchana alisema
katika safari yake ya kutafuta wadhamini mkoani ameweza kuwaona wanachama wengi
wa CCM ambao wanaonesha imani kubwa na chama chao.
Alisema kila alipokutana na wana CCM waliojitokeza
kumdhamini kwa tathmini aliyofanya tangu kuanza kwa siasa ya vyama vingi nchini
CCM, itashinda ushindi wa kimbunga kwani mtaji upo kutokana na kazi kubwa
iliyofanya serikali ya awamu ya nne katika utekelezaji wa
ilani.
“Tumejipanga kuhakikisha wanaingia kwenye uchaguzi
kifua mbele kutokana na kutekeleza ilani,” alisema.
Pia alisema kwa upande wa pili wana kazi ya kuhakikisha
yote mazuri yaliyofanywa na CCM yanasemwa.
“Tuna kazi ya kuhakikisha kuwakumbusha wananchi
barabara za lami na mafanikio mengi yamepatikana na serikali ya awamu ya nne ya
CCM,” alisema.
Alisema kazi kubwa ni kuhakikisha umma unatambua CCM
imefanya mambo mengi kutokana na upotoshaji unaofanywa na wapinzani kuwa CCM
haijafanya lolote.
Pia alisema CCM kuwa na wagombea wengi waliojitokeza
mwaka huu ni dalili njema za CCM kutoa fursa za kupatikana mmoja ambaye kila
moja atamuunga mkono ili kuweza kukivusha chama.
Dk Mwakyembe alisema yuko tayari kumuunga mkono mgombea
atakayeteuliwa na chama. Awali alisema amezunguka katika mikoa 15 katika
kutafuta wadhamini.
Dk Mwele Malecela
Mwanachama mwingine wa CCM aliyerudisha fomu jana ni Dk
Mwele Malecela ambaye alisema pamoja na kazi kubwa iliyofanywa katika uongozi wa
awamu nne bado kuna watu wanaoishi kwenye umasikini
uliokithiri.
Alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wake na waandishi
wa habari. Alisema alifanikiwa kupata wadhamini katika mikoa 20 ikiwemo 17 ya
Tanzania bara na mitatu ya Zanzibar.
Alisema wananchi wameonekana kufarijika kuona
wanafuatwa kwenye maeneo ya kata walipo. Alisema ameweza kuzunguka mikoa tisa
kwa siku nne hali inayoonesha kuwa kazi kubwa imefanyika katika ujenzi wa
barabara za lami kuunganisha mikoa.
‘Pamoja na maendeleo na kazi kubwa ya awamu zote bado
kuna umasikini uliokithiri lazima kuliangalia suala hilo kama kiongozi na
kulitafutia ufumbuzi,” alisema.
Alisema aliguswa sana na wanawake waliojitokeza
wakiwemo wazee ambao walikuwa wakitaka kumuona ni mwanamke wa aina gani ambaye
anataka kugombea Urais.
“Wanawake wamefurahi sana kuona wanawake tunajitokeza
hii ni fursa nzuri ya kuwapa moyo akinamama kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi katika nchi,” alisema.
Membe Ayakana Mabilioni ya
Libya
Membe kwa upande wake wakati anarudisha fomu akijibu
swali aliloulizwa kuhusu madai ya kuwa anahusika na ufisadi wa fedha za Libya na
kama inavyosambazwa na wapinzani wake, alisema akigundulika kuwa alikula hata
dola moja yuko tayari kujiuzulu.
“Uvumi kuwa nahusika na mabilioni ya Libya hauna
mashiko kabisa baadhi ya wanasiasa wenzangu wanajua ukweli wote huu lakini kwa
makusudi wameamua kuniunganisha na kampuni hiyo na kuwaaminisha watu ni yangu au
nina hisa maneno hayo ni ya uongo,” alisema.
Alifafanua kuwa Libya ni moja kati ya nchi wafadhili wa
Tanzania ambapo, kama ilivyo wafadhili wengine imekuwa ikiipa Tanzania misaada
na mikopo yenye masharti nafuu.
Alisema katika utaratibu huo, Tanzania na Libya zilitia
sahihi mkataba wa kubadili madeni na kuyaingiza katika miradi ambao uliweka
utaratibu wa matumizi na urejeshaji wa fedha za deni la
Libya.
Alisema kumbukumbu alizonazo zinabainisha kuwa kabla ya
Serikali ya Libya kuweka saini katika mkataba wa nyongeza iliyotaka fedha hizo
zikopeshwe kwa kampuni ya Meis, upembuzi yakinifu wa mradi husika ulifanywa
kupitia vyombo vyake, na wao wenyewe kujiridhisha juu ya ubora wa mradi
huo.
Sumaye na mahakama ya rushwa
Naye Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye naye
alirejesha fomu alisema akichagulia kuwa Rais wa nchi ataanzisha mahakama
maalumu ya wala rushwa.
Mbali na rushwa pia vipaumbele vyake ni pamoja na
ufisadi, uhujumu uchumi na kwamba ataunda chombo cha uchunguzi katika masuala
hayo.
Pia alisema wakati akiwa Waziri Mkuu wa Tanzania
alifanya mambo makubwa na atahakikisha anaunda serikali inayofahamu kutimiza
wajibu wake.
‘Uchumi ninaouzungumzia si wa takwimu ni wa hali
halisi, nitaangalia pia maeneo kama viwanda vikubwa na vidogo ili watu wengi
waweze kujiajiri na kulinda viwanda vya ndani,” alisema.
Alisema atahakikisha uzalishaji wa viwanda vya ndani
unaongezeka na kunakuwa na ongezeko la mauzo ya nje ya nchi. Pia alisema
ataimarisha huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya upatikanaji wa maji na huduma
nyingine muhimu.
Alipohojiwa kama maeneo aliyokwenda kutafuta wadhamini
aliombwa rushwa, Sumaye alisema, tangu aanze kazi ya siasa hajawahi kutoa
rushwa.
“Hata maeneo ambayo nimekwenda kutafuta wadhamini
sijatoa fedha hata zilizodaiwa kwa lugha laini nilikataa kwani nilitaka
nidhaminiwe na wale walio na imani na mimi,” alisema.
Alisema wakati akiwa Waziri Mkuu alipambana na wala
rushwa ambapo aliweza kuwafukuza kazi watu 3,360 huku wengine 400 walipelekwa
mahakamani.
Balozi Mahiga
Balozi Mahiga naye wakati anarejesha fomu alisema
ameenda mikoa 15 kwa gari na akawashukuru wana CCM kumlaki na kwamba
wamehamasika na wanasubiri kwa hamu uchaguzi.
Alisema kama CCM ikimpitisha kuwa mgombea atahakikisha
kuwa anajenga maadili ya uongozi ili kuondokana na vitendo vya rushwa na
ufisadi.
Alisema uongozi mzuri ni ule unaojengwa katika misingi
ya maadili na atapambana na rushwa ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimekuwa
vikirudisha nyuma wananchi.
“Nitahakikisha ninaimarisha misingi ya umoja na
mshikamano katika nchi ikiwa ni pamoja na kudumisha muungano wa Tanzania na
Zanzibar,” alisema.
Joseph Chaggama
Mwanachama mwingine wa CCM aliyerudisha fomu jana ni
Joseph Chaggama ambaye alisema amezunguka katika mikoa 17 wakati wa kutafuta
wadhamini. Alisema anaijua CCM vizuri na jinsi Serikali
inavyoendeshwa.
Aliongeza na kusema yeye ni mmoja wa watu wasiofahamika na sababu
ya kuchukua fomu ni nia ya dhati kutoka moyoni kuwa anaweza kuongoza
nchi.
Pia alisema uwezekano wa yeye kuchaguliwa lazima
kutokee muujiza. Alisema yuko tayari kuwatumikia Watanzania ikiwa atapewa ridhaa
ya kuwa mgombea wa CCM na akashinda uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka
huu na kuwa yuko tayari kumuunga mkono mgombea ambaye
atateuliwa na chama.
Monica Mbega
Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Monica Mbega naye
alirudisha fomu na kusema kuwa chama kiliweka utaratibu mzuri wakati wakienda
mkoani kupata wadhamini katika mikoa 15 ikiwemo mitatu ya
Zanzibar.
Alisema amekamilisha kazi yake kwa ukamilifu bila
matatizo na kuwashukuru wanawake wengi waliojitokeza kumuunga
mkono.
Aliongezea pia na kusema suala la rushwa linategemea jinsi mtu
alivyokwenda wakati akitafuta wadhamini
Amos akemea matumizi makubwa ya
fedha
Mwingine aliyerudisha fomu hizo jana ni Amosi Siyantemi
ambaye ni mtumishi wa CCM wakati ambaye alisema kuwa kwenye mchakato wa kutafuta
wadhamini baadhi ya wagombea wameonesha matumizi makubwa ya
fedha.
“Ni jambo la kujiuliza fedha hizo wamepata wapi na ni
kiasi gani ni lazima wachunguzwe na kuchukuliwa hatua,” alisema
Siyantemi.
Pia alisema rushwa ni ugonjwa mbaya unaoiangamiza jamii
ni lazima zichukuliwe hatua za haraka na makusudi ili kuweza kukomesha suala
hilo kabla nchi haijatumbukia kwenye shimo la machafuko.
Alisema CCM ya sasa si kama ile ya Mwalimu Nyerere.
“Tunahitaji kurejesha haraka heshima ya CCM machoni mwa Watanzania na kwenye
macho ya Jumuiya ya Kimataifa,” alisema.
Alisema akichaguliwa kuwa Rais atahakikisha kunakuwa na
huduma bora za matibabu sanjari na bima ya afya kwa kila Mtanzania, kufanya
mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa elimu kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo
kupunguza idadi ya masomo.
Pia alisema atapiga marufuku mauzo na manunuzi
yanayofanyika nchini kwa malipo ya dola ambapo malipo ya dola yatafanyika kwa
kibali maalumu.
Pia alisema atakuwa na jukumu la kuleta mageuzi makubwa
katika sekta ya sanaa, michezo na burudani yatakayolenga kuwanufaisha kiuchumi
wananchi.
No comments :
Post a Comment