MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru Kada
wa CCM Rajabu Maranda na wenzake waliokuwa wanakabiliwa na kesi wizi wa Sh
milioni 207 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kutoka Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
Jopo la mahakimu watatu likiongozwa na Hakimu John
Utamwa, Ignas Kitusi na Eva Nkya liliwaachia washitakiwa hao baada ya upande wa
Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya washitakiwa
hao.
Mbali na Maranda washitakiwa wengine walioachiwa huru
ni Farijala Hussein na waliokuwa wafanyakazi wa BoT, Ester Komu, Bosco Kimera na
Imani Mwakosya.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Utamwa alisema washitakiwa
waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka manne kula njama, kughushi, kuwasilisha
nyaraka za uongo BoT na wiziwa Sh milioni 207.2 wako huru kutokana na upande wa
Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka hayo bila kuacha shaka kama
inavyotakiwa kisheria.
Alisema upande wa Jamhuri umeshindwa kuithibitishia
mahakama jinsi Maranda na Farijala walighushi makubaliano ya kukusanya deni kati
ya Kampuni ya General Marketing ya India kwenda Kampuni ya Rashas (T) ya
Tanzania.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa bila Mwakosya kuwepo
mahakamani, Hakimu Utamwa alisema upande wa Jamhuri wameshindwa kumleta
mpelelezi wa kesi hiyo ili aweze kuithibitishia Mahakama saini ambazo zinadaiwa
kuwepo katika makubaliano hayo hivyo udhaifu huo hauwezi kuwatia washitakiwa
hatiani.
Aliongeza kuwa, upande wa Jamhuri ulishindwa
kuthibitisha shitaka la kughushi, kwa hiyo shitaka la kuwasilisha nyaraka za
uongo litakuwa limekufa,kwa sababu wameshindwa kuonesha kweli nyaraka ni za
kughushi.
Aidha alisemwa wameshindwa kuonesha ni jinsi gani fedha
hizo zilihamishwa kama wanavyodai kuwa mchakato huo ulifanikiwa kwa sababu
Maranda na Farijala walitumia nyaraka za kughushi.
“Hakuna shahidi aliyeweza kutoa ushahidi ukaenda sawa
na hati ya mashitaka iliyofunguliwa mahakamani hapo dhidi ya washitakiwa,”
alisema Hakimu Utamwa.
Nyaraka zinazodaiwa kughushiwa ni hati za makubaliano
ya kuhamishiwa deni kutoka Kampuni ya General Marketing ya India kwenda Kampuni
ya Rashas (T) ya nchini Tanzania, ambazo walizutumia na kuiba fedha
hizo.
Baada ya Hukumu hiyo, Farijala alirudishwa rumande kwa
sababu anatumikia kifungo cha miaka miwili jela alichohukumiwa katika kesi
nyingine na Maranda aliachiwa lakini bado ataendelea kwenda mahakamani kwa kuwa
anakabiliwa na kesi nyingine.
Ndugu na marafiki waliokuwepo katika eneo hilo la
mahakama walishukuru mahakama kutoa uamuzi wa haki na kusema kweli Mungu
ametenda miujiza.
No comments :
Post a Comment