Sunday, July 19, 2015

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI (NEC) YAIKINGIA KIFUA CCM

Mstaafu Jaji Damian Lubuva (Picha kutoka Maktaba)
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC) Mstaafu Jaji Damian Lubuva amesema mgombea urais mteule wa CCM, Dk John Magufuli hapigi kampeni bali kinachofanyika ni utambulisho wa mgombea wao kwa wananchi.


Kauli ya Lubuva imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Chama
cha ACT-Wazalendo kuandikia barua NEC, ikilalamika kuwa Dk Magufuli ameanza kampeni kabla ya wakati.

Alisema NEC imepokea barua ya malalamiko ya ACT-Wazalendo inayolalamika kuwa Magufuli ameanza kampeni kabla ya muda na pia kulalamika kualikwa kwa mteule huyo wa CCM kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Michuano ya Kombe la Kagame, inayoanza leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Tume ina maadili yake, kwa mfano eti tumzuie asiende kwenye mechi , sisi tumzuie kama nani, huu si wakati wetu, wakati wetu ukifika tutakunjua makucha yetu”

alisema.



Alisema NEC haihusiki hata na yale yanayotokea Dodoma, bali itaanza kazi yake ifikapo Agosti 21 mara baada ya uteuzi rasmi wa wagombea.

Akizungumzia zaidi ziara hizo, Jaji Lubuva alisema tume hiyo haina kauli juu ya ziara ya Magufuli, bali akifanyacho ni mchakato tu wa ratiba ya chama chake.

Jaji Lubuva alisema kwa upande wa Sheria na Katiba, Nec itaanza kuchukua hatua kwa wale watakaokiuka kanuni kuanzia Agosti 22, pindi kipyenga cha kampeni kitakapoanza hadi Oktoba 24 kitakapomalizika.

“Katika kipindi hicho, tume inakuwa na nguvu ya kuwashughulikia wagombea, kwa sasa kinachotokea ni mambo ya vyama, sisi kwenye tume hatuna msingi wa kushughulikia hayo,” 

alisema.



Wakati Jaji Lubuva akisema hayo, Chama Cha Kijamii (CCK) wameamua kutumia wanasheria ili kuandaa mipango ya kumwekea pingamizi Dk Magufuli, kuwa anakiuka Sheria ya Uchaguzi kwa kufanya kampeni kabla ya wakati.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa CCK Renatus Muhabi, alisema Tume ya Uchaguzi (NEC) huenda nayo ikashtakiwa kwa kushindwa kuwajibika licha ya kuwa ndiyo msimamizi wa Sheria ya Uchaguzi.

“Tumeshampa kazi mwanasheria, Aloys Rugaziya kuandaa pingamizi baada ya kutoridhishwa na majibu ya Jaji Lubuva.“ Majibu yake Jaji Lubuva ni wazi yanaonyesha kuwa anaiogopa CCM, maana ndiyo iliyompa hiyo nafasi, hapo unaweza kuona kwa nini tumekuwa tunalilia tume huru, yeye anapodai hahusiki na kufuatilia mambo anayofanya mgombea huyo, eti hadi pale atakapochukua fomu ya NEC, huu siyo utawala bora ni ukiukwaji mkubwa,” 


alisema.



Muhabi alisema CCK imeamua kujitolea kulifuatilia jambo hilo kwa karibu licha ya kwamba wapinzani wenzao wakiwamo UKAWA wapo kimya, wanaamini kwamba ukimya huo unatokana na kutingwa kusaka mgombea wao wa urais, hivyo wao watajitahidi hadi dakika ya mwisho kutetea haki na demokrasia ndani ya vyama. 

Wakili anayeshughulikia utaratibu wa kufungua kesi hiyo, Rugaziya, alikiri kuwapo kwenye mchakato wa kufungua kesi, lakini hatua hiyo itafuata pale watakapojiridhisha kuwa kuna makosa ya kisheria kwenye matendo ya Dk Magufuli na mikutano anayofanya.

“Wanasiasa wana utazamaji wao wa mambo nasi kama wanasheria tuna utazamaji wetu, hivyo tunachofanya sasa ni kwamba tupo kwenye hatua za kujiridhisha kwanza kuangalia vipengele vya sheria ya uchaguzi kwa ujumla, ikiwamo masuala ya kampeni baada ya hapo ndiyo tutajua mwelekeo mzuri wa jambo hili,” 
alisema Wakili Rugaziya.

No comments :

Post a Comment