Monday, July 13, 2015

UKAWA WASEMA HAWAMUOGOPI MAGUFULI

UKAWA Wasema Magufuli Hawatishi na Hawamuogopi!!

Dakika chache baada ya CCM kumpitisha Dk John Magufuli kuwa mgombea wake wa urais, viongozi wa vyama vya upinzani wamesema hawatishwi na Dk Magufuli na wanamuona kama kada wa kawaida miongoni mwa wengi waliopo CCM na kwamba hawezi kuleta mabadiliko yoyote.

Wamesema vita yao ni kuondoa mfumo wa uongozi uliopo na si ya mtu mmojammoja.

Wakizungumza jana viongozi hao, hasa wanaounda Ukawa, walisema wanajipanga kumtambulisha mgombea wao kesho na kila Mtanzania atapata fursa ya kumfahamu.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema CCM inakabiliwa na tatizo la mfumo mbovu, hivyo vita iliyopo inaelekezwa katika kukiondoa madarakani ili kuruhusu kitu kipya kuchukua nafasi na kuwapa Watanzania uzoefu mwingine.

Alisema Ukawa haimhofii mgombea huyo kwa kuwa hata sifa zilizotumika kumpata ni za chama chake na kwamba suala linalozingatiwa ni hoja zenye mashiko mbele ya wananchi ambao wamechoshwa na taratibu za siku zote kushughulikia kero zao.

“Ajenda na hoja tulizonazo ndizo zitakazotubeba mbele ya wananchi… tutawapelekea ili waamue wakiwa na taarifa sahihi. Kama ni kutowajibika au ufisadi ndani ya CCM, suala hilo linaanzia ngazi ya juu mpaka kwa mwanachama wa kawaida,” alisema na kuongeza:

“Hatutegemei kashfa kama kigezo kikuu cha kumshinda mgombea wa CCM kwa kuwa hilo ni tatizo la mfumo wa chama kizima,” alisema.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi alisema endapo wananchi wataachana na dhana ya kufuata itikadi na wakaelekeza fikra na akili zao katika hoja za kampeni, watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kumchagua kiongozi bora.

“Hatustushwi na (Dk John) Magufuli kwa lolote na mashambulizi yetu yatakuwa makubwa. Lengo letu la kuiondoa CCM madarakani liko palepale,” alisema Dk Makaidi ambaye pia ni Mwenyekiti wa NLD.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema mabadiliko ya mfumo mbovu wa utawala hayawezi kufanywa na mteule yeyote wa CCM kwa kuwa chama hicho kimeahidi kufanya mambo yaleyale.

Alisema baada ya chama hicho kumaliza harakati zake za kumpata mgombea urais, kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kumteua Samia Suluhu Hassan aliyeshiriki uongozi wa kuichakachua Katiba Mpya.

“Hii inadhihirisha kuwa nchi itaongozwa na watu walio nyuma ya pazia kuendeleza uchakachuaji badala ya kuheshimu matakwa ya wananchi. Ufisadi utaendelea iwapo CCM itaendelea kutawala,” alisema Mnyika.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema alimpongeza Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete pamoja na kamati ya maadili ya chama hicho kwa kuwaondoa watu wenye kashfa za rushwa na ufisadi na kutaka wembe huo uendelee hata kwa ngazi za ubunge na udiwani.

“Chama kimejivua gamba na wafanye hivyo kwa ngazi zote zilizosalia,” alisema Mrema na kuongeza kuwa:
 
“Nitafanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Dk Magufuli kwani ameshafanya kazi kubwa hapa Vunjo. Namtakia mafanikio katika safari yake.”

TAARIFA KAMILI KUHUSU TUKIO LA UJAMBAZI LILILOTOKEA USIKU WA JANA

WATU wanaodhaniwa kuwa majambazi wamevamia Kituo cha Polisi Stakishari kilichopo Ukonga jijini Dar es Salaam, jana usiku na kuua askari na raia kisha kupora silaha.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa watu hao walifika kituoni hapo wakiwa katika pikipiki wakidai kwamba walikuwa wamembeba mtu aliyepata ajali wakihitaji msaada wa polisi kabla ya kuwabadilikia ghafla na kuanza kuwashambulia kwa risasi.

Inadaiwa kuwa askari wanne wamepoteza maisha katika tukio hilo, wananchi wawili na mmoja wa magaidi hao.

Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema atakuwa na mkutano na wanahabari kati ya saa 5 au 6 leo kwa ajili ya kutoa taarifa rasmi juu ya tukio hilo la kigaidi.

UJAMBAZI: KITUO CHA POLISI SITAKI SHARI UKONGA CHAVAMIWA NA MAJAMBAZI

Kuna habari zmetufikia zinazosema kwamba kituo cha polisi cha Sitaki-Shari kikichopo Ukonga kimevamiwa na majambazi ambapo takribani watu sita wanakadiriwa kuuwawa.
Bado tunafuatilia kwa undani habari hii

MAGUFULI AWATANGAZIA KIAMA MAFISADI

Mgombea wa Uraisi kupitia CCM Mh. John Pombe Magufuli amewatangazia kiama mafisadi, wezi na walarushwa.

Magufuli aliyaongea hayo Jana katika viwanja vya Jamhuri Manispaa ya Dodoma alipokua anakijitambulisha kwa  wananchi waliokua wamefurika katika viwanja hivyo.

Akiwa mwenye kujiamini na mwenye bashasha na akishangiliwa na umati huo Wa wananchi Mh. Magufuli alisema kwamba atawashughulikia mafisadi wezi na walarushwa na hatowangusha wananchi.

Wengi wa wananchi waliosikiliza hotuba yake waliipongeza na kusema kwamba hotuba hiyo inatoa mwanga mpya hasa kutokana na kutokubagua wananchi kutokana na vyama vyao.

Mh. Magufuli alisisitiza kwamba hatowangusha wana CCM na Wapinzani (CHADEMA, CUF, NCCR n.k) na kuwaomba wamuamini na wampe ridhaa ya kuwaongoza.

MEMBE , KIGWANGALA WANYOOSHA MIKONO

Waziri wa Mambo ya nje na  Ushirikiano wa  Kimataifa Mh. Bernard Membe  pamoja na  Mbunge wa Nzega  Dkt. Hamisi Kigwangalla wamekubali kushindwa katika kinyang’iro cha kuomba ridhaa ya kuteuliwa ndani ya chama cha Mapinduzi CCM zoezi lililohitimishwa leo.

Akizungumza na Mwandishi wetu mara baada ya Magufuli kutangazwa mshindi  , Mh. Bernad Membe amesema angechaguliwa mtu mwingine pasinge tosha leo katika ukumbi mpya wa chama cha Mapinduzi CCM, lakini kuteuliwa kwa Dkt Magufuri ameridhika kabisa kutoka ndani ya moyo wake huku akimmwagia  sifa Magufuli na kusisitiza kuwa  watanzania wamepata mtendaji shupavu.

Naye Kigwangalla amesema  hakika Magufuli ni chaguo la Mungu kwa  kuwa ni mmoja kati ya wanasiasa ambao hawajatoa hata shilingi kumi kuwapa wadhamini ili adhaminiwe kama ilivyo kwa wanasiasa wengine.

Kwa mujibu wa Nape Nnauye katibu wa Itikadi na Uenezi CCM  mara baada ya kumpata mwanasiasa atakaye peperusha bendera ya chama cha Mapinduzi amesema wanatarajia kufanya mkutano jijini Dar es salaam siku ya jumanne.