Monday, July 13, 2015

UKAWA WASEMA HAWAMUOGOPI MAGUFULI

UKAWA Wasema Magufuli Hawatishi na Hawamuogopi!!

Dakika chache baada ya CCM kumpitisha Dk John Magufuli kuwa mgombea wake wa urais, viongozi wa vyama vya upinzani wamesema hawatishwi na Dk Magufuli na wanamuona kama kada wa kawaida miongoni mwa wengi waliopo CCM na kwamba hawezi kuleta mabadiliko yoyote.

Wamesema vita yao ni kuondoa mfumo wa uongozi uliopo na si ya mtu mmojammoja.

Wakizungumza jana viongozi hao, hasa wanaounda Ukawa, walisema wanajipanga kumtambulisha mgombea wao kesho na kila Mtanzania atapata fursa ya kumfahamu.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema CCM inakabiliwa na tatizo la mfumo mbovu, hivyo vita iliyopo inaelekezwa katika kukiondoa madarakani ili kuruhusu kitu kipya kuchukua nafasi na kuwapa Watanzania uzoefu mwingine.

Alisema Ukawa haimhofii mgombea huyo kwa kuwa hata sifa zilizotumika kumpata ni za chama chake na kwamba suala linalozingatiwa ni hoja zenye mashiko mbele ya wananchi ambao wamechoshwa na taratibu za siku zote kushughulikia kero zao.

“Ajenda na hoja tulizonazo ndizo zitakazotubeba mbele ya wananchi… tutawapelekea ili waamue wakiwa na taarifa sahihi. Kama ni kutowajibika au ufisadi ndani ya CCM, suala hilo linaanzia ngazi ya juu mpaka kwa mwanachama wa kawaida,” alisema na kuongeza:

“Hatutegemei kashfa kama kigezo kikuu cha kumshinda mgombea wa CCM kwa kuwa hilo ni tatizo la mfumo wa chama kizima,” alisema.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi alisema endapo wananchi wataachana na dhana ya kufuata itikadi na wakaelekeza fikra na akili zao katika hoja za kampeni, watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kumchagua kiongozi bora.

“Hatustushwi na (Dk John) Magufuli kwa lolote na mashambulizi yetu yatakuwa makubwa. Lengo letu la kuiondoa CCM madarakani liko palepale,” alisema Dk Makaidi ambaye pia ni Mwenyekiti wa NLD.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema mabadiliko ya mfumo mbovu wa utawala hayawezi kufanywa na mteule yeyote wa CCM kwa kuwa chama hicho kimeahidi kufanya mambo yaleyale.

Alisema baada ya chama hicho kumaliza harakati zake za kumpata mgombea urais, kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kumteua Samia Suluhu Hassan aliyeshiriki uongozi wa kuichakachua Katiba Mpya.

“Hii inadhihirisha kuwa nchi itaongozwa na watu walio nyuma ya pazia kuendeleza uchakachuaji badala ya kuheshimu matakwa ya wananchi. Ufisadi utaendelea iwapo CCM itaendelea kutawala,” alisema Mnyika.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema alimpongeza Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete pamoja na kamati ya maadili ya chama hicho kwa kuwaondoa watu wenye kashfa za rushwa na ufisadi na kutaka wembe huo uendelee hata kwa ngazi za ubunge na udiwani.

“Chama kimejivua gamba na wafanye hivyo kwa ngazi zote zilizosalia,” alisema Mrema na kuongeza kuwa:
 
“Nitafanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Dk Magufuli kwani ameshafanya kazi kubwa hapa Vunjo. Namtakia mafanikio katika safari yake.”

No comments :

Post a Comment