MBUNGE wa Jimbo la Mpanda Mjini, Bw. Said Amour Alfi (CHADEMA) ni miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao wamechukua na kurejesha fomu za kuomba kugombea ubunge katika Jimbo jipya la Nsimbo, Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi kwa tiketi ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM mkoani Katavi, Averin Mushi amethibitisha Bw. Arfi kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo hilo.
Alisema makada 23 wamejitokeza kuwania ubunge katika majimbo yote ya uchaguzi mkoani humo ambapo katika Jimbo la Nsimbo, makada ambao wamerejesha fomu ni Bw. Arfi, Shabir Hasanali 'Dallah', Richard Mbogo, Manamba David na Mapesa Frank.
Katika Jimbo la Katavi ni Isaack Kamwelwe, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoani humo, Shafi Mpenda, Maganga Kampala na Osca Albano.
Kwa upande wa Jimbo jipya la Kavuu, yupo Zumba Emmanuel, Mselem Abdalah Said na Prudenciana Kikwembe ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu.
Jimbo la Mpanda Mjini yuko Sebastian Kapufi, Galus Mgawe na Gabriel Mnyele na Mpanda Vijijini ni Moshi Kakoso, Abdalah Sumry, Willy Makufe, Elizabeth Sultan, Godfrey Nkuba, Rock Mgeju na Chifu Charles Malaki.
Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Abdallah Mselem aliwaasa wanachama wa chama hicho kujiepusha na wagombea wanaotumia ukabila, udini na hali yoyote ya ubaguzi ili kupata uongozi.
"Wapo wagombea wanaotumia misingi ya udini na ukabila kuwabagua wagombea wenzao na kuwashawishi wanachama wasiwachague, kama mgombea yeyote atabainika kufanya hivyo hatutamvumilia bali atashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za chama," alisema.
No comments :
Post a Comment