|
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba; picha kutoka maktaba |
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba amesema CCM inakabiliwa na kazi ngumu ya kupata mgombea wa urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa mwaka huu, akionya kuwa makundi ya urais yasipomalizwa yanaweza kufika hadi ngazi ya kata.
Makada 38 wamejitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho tawala ya kugombea urais katika kipindi ambacho kuna ongezeko kubwa la nguvu ya vyama vya upinzani, huku vyama vinne vikiwa vimeamua kusimamisha mgombea mmoja.
Tayari vikao vya kujadili jinsi ya kumpata mteule wa kupeperusha bendera ya chama hicho vimeshaanza kwa wenyekiti na makamu wao kukutana na jana Kamati Kuu ilikuwa inakutana mjini Dodoma.
Akiangalia hali hiyo, Jaji Warioba aliiambia Mwananchi jana kuwa chama hicho tawala kinatakiwa kuwa makini katika mchakato huo, kwa maelezo kuwa unaweza kuacha majeraha makubwa kutokana na makundi yaliyoibuka.
“CCM inakabiliwa na wakati mgumu wa kupitisha jina la mgombea urais kutokana na waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kufikia 38, na mpaka sasa imekuwa ni vigumu kutabiri atakayepitishwa, jambo ambalo halikujitokeza wakati wa upitishwaji wa mgombea urais wa chama hicho mwaka 1995 na 2005,” alisema Jaji Warioba, ambaye alikuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kila unapofika Uchaguzi Mkuu kunakuwa na changamoto zake, lakini mwaka huu CCM inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kwa sababu uchaguzi huo utamleta rais mpya na mwenyekiti mpya wa chama hicho.
Alisema jambo la kwanza lililotokea katika mchakato wa kumpata mgombea urais litakalokifanya chama hicho kuwa na wakati mgumu ni kitendo cha baadhi ya wagombea kueleza sera zao, wakati wakijua wazi kuwa sera za CCM ziko kwenye ilani yake ya uchaguzi.
“Waliotangaza nia wamekuwa wakieleza sera zao na ukiwasikiliza unaona kama walikuwa wagombea binafsi hivi kwa sababu CCM ina sera, wanayo ilani ambayo ipo tayari na yeyote atakayepeperusha bendera ya CCM lazima ajikite kwenye ilani ya chama,” alisema jaji Warioba.
“Kama mtu ametangaza sera na vipaumbele vyake na havifanani na vipaumbele vya ilani ya chama unafanyaje? Ni mtihani mwingine huo.”
Alisema jambo la pili ni kukiukwa kwa utaratibu uliowekwa na chama hicho kwamba yeyote anayehusika kwenye ngazi ya maamuzi, asimdhamini mgombea yeyote wa urais, huku akiwatolea mfano wajumbe wote wa mkutano mkuu wa chama hicho ambao ndio humchagua mgombea urais wa chama hicho.
“Nimeambiwa kwamba wajumbe wa mkutano mkuu walikatazwa kudhamini wagombea, lakini tulivyoona ni kwamba viongozi wengi wameonyesha waziwazi wapo kundi gani, wapo waliojitokeza na kusema na wengine hawakusema lakini wanajulikana wanamuunga mkono mgombea gani,” alisema.
“Hawa ndio watakwenda kuchuja, sasa hapa itakuwa kazi ngumu na inawezekana kukawa na mgongano wa maslahi na hilo lisipoangaliwa linaweza kufanya mchujo ukaonekana kuwa haukuwa wa haki. Jambo hili linatakiwa kuangaliwa na hasa kwa kuwa kuna makundi.
Alisema makundi yaliyoibuka ndani ya chama hicho yanaweza kuifanya CCM ikalegalega na hasa kama wengine watafikiri utaratibu uliotumika wa kumpata mgombea haukuwa wa haki.
“Hali hiyo ikitokea itakuwa ngumu kuyarudisha makundi hayo ili kuwa kitu kimoja,” alionya Jaji Warioba ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Katika siasa chama ndiyo muhimu na kisipokuwa imara, mgombea yeyote wa chama husika hataweza kuwa na nguvu sana. Nadhani itasababisha matatizo na si katika urais tu, haya makundi yasipopatana yakaendelea na uhasama itakwenda mpaka kwenye majimbo na kata,” alisema.
Alisema mwaka huu ni wa ushindani na kama CCM isipochukua tahadhari katika kumpata mgombea, chama hicho kitakumbana na wakati mgumu.
Kamati Kuu ya CCM itakutana Julai 9 kufanya mchujo na Julai 10 Halmashauri Kuu itakutana kupanga ajenda za Mkutano Mkuu ambao utafanyika Julai 11-12 kwa ajili ya kumchagua mgombea urais.
Kamati Kuu, ambayo ndiyo msingi wa maamuzi yote, inaundwa na mwenyekiti, ambaye ni Rais Jakaya Kikwete; mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein; Makamu mwenyekiti, Philip Mangula; katibu mkuu, Abdulrahman Kinana; makamu wa Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Spika Anne Makinda na Balozi Seif Ali Iddi.
Wengine ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Amir Kificho; Rajab Luhwavi, Vuai Ali Vuai, Nape Nnauye, Mohamed Seif Khatibu, Zakhia Meghji, Asha Rose- Migiro, Sophia Simba, Sadifa Juma Khamis, Abdallah Bulembo, Jenister Mhagama, William Lukuvi.
Wengine ni Steven Wasira, Dk Emmanuel Nchimbi, Pindi Chana, Jerry Silaa, Adam Kimbisa, Shamsi Vuai Nahodha, Dk Hussein Mwinyi, Maua Daftari, Samia Suluhu, Dk Salim Ahmed Salim, Makame Mbarawa na Hadija Abood.
Msekwa anena
Wakati Jaji Warioba akitafakari mustakabali wa CCM, makamu mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Pius Msekwa amesema ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi itakuwa ni moja ya mambo mawili makubwa yatakayoangaliwa kwenye mchujo wa wagombea.
Mbali na ukiukwaji huo wa taratibu, watatumia vigezo 13 vilivyowekwa na chama hicho kumpata Rais wa Serikali ya Awamu ya tano na mwenyekiti wa chama hicho.
Tayari baraza hilo linaloongozwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi limeripotiwa kuanza kazi ya uchambuzi na litawasilisha taarifa yake kwa Kamati Kuu .
Wajumbe wengine wa baraza hilo la wazee ni Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, marais wa zamani wa Zanzibar Aman Abeid Karume na Dk Salmin Amour.
Jana, Msekwa ambaye amewahi kuwa makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, alisema kazi hiyo itafanywa kwa umakini mkubwa kwa kuzingatia mambo hayo mawili.
“Sifa zimeandikwa kwenye kanuni zetu za chama na zipo 13. Hizo ndizo zitakuwa kipimo cha wagombea katika vikao na watachujwa kwa kuzingatia hilo. Ni lazima kutazama kama mgombea ana sifa hizo,” alisema.
“Pili, tunatazama kama mgombea amekiuka masharti yoyote ya kanuni zetu maana unaweza kuwa na sifa lakini ukawa umekiuka masharti.”
Alisema mambo hayo mawili ndiyo yatakayotumika na hakuna kigezo kingine chochote kitakachomfanya mtu kupata au kukosa nafasi.
Msekwa alikumbushia makada wa chama hicho waliowahi kukumbana na adhabu baada ya kukiuka masharti ya kanuni akisema: “Nadhani unakumbuka wapo waliowahi kusimamishwa kutokana na kukiuka masharti ya kanuni baada ya kuanza kampeni mapema. Kwa sasa wameshafunguliwa.”
Makada waliopewa ‘adhabu ya kifungo’ cha mwaka mmoja kutokana na kujihusisha na kampeni za urais kabla ya wakati ni mawaziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Kilimo na Ushirika, Steven Wasira.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Source: Mwananchi