Dodoma. Wabunge 33 jana walipitisha Muswada wa Benki ya Posta Tanzania (kufuta sheria iliyoanzisha Sheria ya Benki ya Posta na kuweka masharti ya mpito).
Idadi ya wabunge wote ni 356 na nusu yake ni 178 wanaotakiwa kupitisha jambo lolote lenye uamuzi ikiwamo miswada.
Tangu asubuhi jana, kulionekana kuwa na idadi ndogo ya wabunge huku baadhi yao wakiingia na kutoka kila walipomaliza kusaini mahudhurio.
Mara baada ya kupitishwa kwa muswada huo ambao uliwasilishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, idadi ya wabunge ilipungua zaidi na kubaki wabunge 29 huku Muswada mwingine wa Sheria ya Masoko ya Bidhaa wa 2015 ulipokuwa ukiwasilishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima.
Wakati hali ikiwa hivyo ndani ya Ukumbi wa Bunge, kulikuwa na idadi ndogo ya wabunge walioonekana nje ya ukumbi wakizungumza kwa vikundi na wengine wakiwa ‘bize’ na simu zao za mikononi.
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa alilalamikia kitendo hicho akisema ni uvunjaji wa kanuni na Katiba ya nchi.
Mnyaa alisema kuwa wabunge wa Tanzania wengi ni wapole na wasiopenda makuu kwani kama ingetokea mtu yeyote akasimama na kuamua kushtaki, lazima angeshinda na kupata umaarufu mkubwa.
“Hapa tunachokifanya siyo jambo jema hata kidogo, unajua mambo mengi tunayopitisha hapa yanakuwa sheria. Si sahihi na tunaanza kuvunja sheria sisi wenyewe humu ndani,” alisema Mnyaa.
Alisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 94 (1) ambayo inaeleza kuwa upitishwaji wa jambo lolote linalohusu uamuzi wa wabunge ni lazima akidi iwe ni nusu ya wabunge wote kama ilivyo Kanuni ya 77 ya Bunge.
“Kila tukisema sisi tunapingwa na kuambiwa kaa chini, tena sisi wapinzani ndiyo shida kweli na hasa hawa wanaokalia viti (anawataja) wanatubana sana ni afadhali na Ndugai (Job, Naibu Spika),” alisema.
Mbunge huyo alibainisha kuwa wakati wowote kama ataibuka mtu wa kutaka kuliburuza Bunge mahakamani, atashinda kesi hiyo mchana kweupe na sheria nyingi zitapaswa kufutwa.