Sunday, August 2, 2015

Mtikila achukua fomu ya urais kwa shingo upande

Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila  akisaini nyaraka za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) za kuthibitisha kupokea fomu za kugombea Urais  zilizokabidhiwa na Ofisa Mwandamizi wa Tume  hiyo George Kashura jijini Dar es Salaam jana
Dar es Salaam. Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP),
Christopher Mtikila akigoma kusaini fomu za kugombea urais akitaka ufafanuzi wa mgombea binafsi, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa alikwama kwenye lifti za jengo lililopo katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi (NEC) kutokana na kukatika umeme.
Mchungaji Mtikila ambaye aliambatana na mgombea mwenza Juma Metu Juma, alitaka ufafanuzi wa kutokuruhusiwa kuwania urais akiwa mgombea binafsi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (AfCHPR) imeruhusu.
“Siondoki hapa na wala sitaweza kuchukua hizi fomu hadi mniambie ni wapi nitapata jibu la tume la kukiuka maagizo ya mahakama ya Afrika.
“Waandishi embu subirini kwanza mkurugenzi wa uchaguzi aje hapa ilia atoe ufafanuzi na nyie msikilize mkaandike ukweli kwa sababu hii siyo haki ni sawa na kudharau mahakama,” alisema.
Baada ya kuzozana na maofisa waliokuwa wakimkabidhi fomu hizo, walilazimika kumuita mkurugenzi wa uchaguzi Kailima Ramadhani, ambaye alimwambia kwamba sheria hairuhusu.
“Sisi tunafuata sheria mwenyekiti kama hicho kipengele kingekuwapo tungekuruhusu uchukue fomu hizo, lakini hapa tunabanwa na sheria tunaruhusu kutoa fomu kwa watu wanaotoka kwenye vyama vyao,” alisema Ramadhani
Alisema ni vizuri Mtikila angefuatilia kwa makini suala hilo ili sheria ipitishwe kwani NEC wanachokifanya ni kufuata sheria zilizopo tu na si vinginevyo.
Baada ya kumaliza maongezi Mtikila aliamua kuweka sahihi na kuchukua fomu hizo kwa shingo upande huku akisema atakiwakilisha vyema chama chake hicho.
Juni 13,2013 Mtikila alishinda kesi aliyofungua AfCHPR, mjini Arusha akidai Tanzania inakiuka demokrasia inapozuia wagombea binafsi.
Mchungaji Mtikila, ambaye ana historia ndefu ya kukwaruzana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), alifungua shauri mahakama ya Afrika mwaka 2011 baada ya jitihada zake za kupindua mabadiliko ya kikatiba yaliyofuta ugombea binafsi kugonga mwamba kwenye mahakama za kitaifa.
Dovutwa
Mwenyekiti wa UPDP Fahmi Dovutwa alikwamba kwenye lifti kwa dakika kumi baada ya jana kuchukua fomu za kuwania urais.
Dovutwa ambaye alikuwa wa kwanza kufika kuchukua fomu saa tatu asubuhi, akiwa ameambatana na mgombea mwenza, alisema kwamba kukwama kwake kwenye lifti ni hujuma iliyofanywa na baadhi ya wagombea wenzake wa urais.
Wakati huohuo; Mgombea urais kwa tiketi ya TLP Maxmilian Lyimo, ambaye hakuwa na mgombea mwenza alikuwa wa pili kufika katika ofisi hizo kwa ajili ya kuchukua fomu.
Mgombea huyo alifika saa 5:33 asubuhi baada ya kuchukua fomu alisema kuwa upepo wa Uchaguzi Mkuu unaovuma mwaka huu, haukuwahi kuvuma wakati mwingine wowote, hivyo inaashiria kuwa nchi itapata kiongozi asiyetarajiwa na wengi.
“TLP ni chama kisichochafua amani tangu kuasisiwa kwake, hivyo wananchi waangalie amani ya nchi kwani ni bora kuliko kitu kingine,”alisema na kuongeza:
“TLP bado kuna nafasi za uongozi kuanzia kata hadi za ubunge, wanaoshindwa huko waliko tunawakaribisha kwa ajili ya kuja kugombea nafasi hizo.”

No comments :

Post a Comment