Friday, July 3, 2015

SHINYANGA: Polisi yakamata mashine ya BVR kwa kiongozi wa CHADEMA

Jeshi la polisi wilayani Kahama mkoani Shinyanga limekamata mashine moja ya BVR ikitumika kuandikisha wapiga kura saa tatu usiku nyumbani kwa mwenyekiti wa mtaa wa Nyakato wilayani humo Mayunga Alphonce (CHEDEMA), huku wakiwalipa shilingi 5,000/= kila mmoja.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya amesema tukio hilo limetokea jana majira ya saa 3 usiku katika mtaa wa Nyakato ambapo mashine hiyo ilikutwa ikiwa inafanya kazi ya kuandikisha wapiga kura.

Mpesya amesema kuwa vyombo vya usalama wilayani humo vilipata taarifa kutoka kwa raia wema ambazo zimewezesha kukamatwa kwa mashine hiyo pamoja na vitambulisho vitano ambavyo tayari vilikuwa vimeshakamilika kuandikishwa.

Ameongeza katika harakati za kukamata mashine hiyo pia wameweza kumkamata mhamiaji haramu mmoja raia wa Burundi ambaye tayari alikuwa ameshaandikishwa na mashine hiyo akiwa ndani ya nyumba ya mwenyekiti huyo.

Mpesya amesema jeshi la Polisi wilayani humo linamshikilia Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Nyasubi, Lugina Misango ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusimamia mashine hizo kwa kosa la kuruhusu mashine hiyo kutumika nyumbani kwa Mwenyekiti wa Mtaa.

Katika hatua nyingine, Mpesya amewataka waandishi wa habari wanaotumiwa kukanusha taarifa hiyo, kutambua kuwa ofisi yake ina mamlaka kamili ya serikali na kwamba wasubiri hatua za kisheria kwani ushahidi wa kukamatwa kwa mashine hiyo upo katika kituo cha polisi.

Source: Habari hii nimeinukuu kutoka Malunde 1 Blog

No comments :

Post a Comment