Monday, July 20, 2015

JOTO LA UCHAGUZI: CHADEMA YATANGAZA RATIBA YA KURA YA MAONI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza ratiba ya kuanza kura ya maoni ndani ya chama hicho kuwa itaanza leo (Julai 20) na kumalizika Julai 25 mwaka huu.

Kura hiyo inakuja baada ya kukamilika kwa kazi ya uchukuaji fomu za kuomba kuwania ubunge na udiwani, ndani ya chama hicho.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Chadema, Tumaini Makene, alisema jana kuwa katika hatua hiyo, kila uongozi wa kanda umepanga ratiba yake ya kura za maoni katika majimbo mbalimbali.

Makene alisema kupitia mchakato huo wa kura ya maoni, wana wa Chadema  watapata wagombea ubunge makini ambao watakihakikishia chama ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu, utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Alisema ili kufanikisha mchakato huo, Waratibu wa Kanda za Chama, Makatibu wa Mikoa na Makatibu wa Majimbo watoe ushirikiano kwa vyombo vya habari ili viweze kufuatilia nchi nzima na kuuhabarisha umma wa Watanzania.

Mnyika achukua fomu ya Ubunge
Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (pichani), jana alichukuliwa fomu na Wazee wa chama hicho wa jimbo hilo wakimshinikiza kuwania tena nafasi hiyo.
 
 Wazee hao ambao walifika kwenye ofisi za jimbo maeneo ya Kimara Kona, majira ya mchana walimtaka kuwania nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Akizungumza na mtandao huu, Katibu wa jimbo hilo, Justine Mollel, alisema katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Ubunge kwenye jimbo hilo hadi jana aliyechukua fomu ni Mnyika pekee.

Alieleza kuwa, kwenye jimbo jipya la Kibamba jumla ya makada saba wa Chadema, walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo.

“Ni kweli Mnyika leo amechukuliwa fomu na Wazee wa Chadema Jimbo la Ubungo kwa ajili ya kuwania nafasi ya Ubunge na mipaka sasa hakuna aliyechukua fomu ya kuwania nafasi hiyo na anatarajia kuirudisha leo jioni (jana),” alisema Mollel.

No comments :

Post a Comment