Tuesday, July 28, 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU HABARI ILIYOANDIKWA KWENYE GAZETI LA MWANANCHI


THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
STATE HOUSE,
1 BARACK OBAMA ROAD,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Gazeti la Mwananchi la leo, Jumatatu, Julai 27, 2015, kwenye ukurasa wake wa 26 limechapisha habari yenye kichwa cha habari, “Marais watano wanaotajwa kuongoza kwa mishahara minono barani Afrika ni hawa hapa”.

Katika habari hiyo ambayo gazeti hilo linadai chanzo chake ni “uchambuzi wa mtandao wa African Review” inadaiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, anashilikia nafasi ya tano miongoni mwa viongozi 38 wa nchi za Afrika wanaolipwa mshahara mnono zaidi.

Gazeti hilo linadai kuwa Rais Kikwete analipwa Dola za Marekani 192,000 kwa mwaka, ikiwa ni malipo ya Dola za Marekani 16,000 kwa mwezi.

Habari hizi siyo za kweli. Ni uongo na uzandiki. Ni uzushi mtupu na ni uzushi wa hatari.

Mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwezi ama kwa mwaka haufikii na hata wala kukaribia kabisa kiwango kinachotajwa na Gazeti la Mwananchi.

Tangu Uhuru, mwaka 1961, Rais wa Tanganyika na baadaye tangu mwaka 1964 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa miongoni mwa viongozi wanaolipwa mishahara ya chini kabisa duniani.

Mshahara wa Rais wa Tanzania kwa mwezi ni wa chini kiasi cha kwamba mshahara wake unazidiwa, tena kwa mbali, na mishahara wanayolipwa baadhi ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma nchini.

Aidha, ni jambo la kushangaza kwamba Gazeti la Mwananchi, linalochapishwa hapa nchini, linaweza kupata kiasi cha uongo anacholipwa Rais wa Tanzania katika mitandao ya nje badala ya kuuliza rasmi na kupewa majibu sahihi.

Kwa kujiingiza katika uzushi wa kupindua kiasi hiki, Gazeti la Mwananchi haliwezi kuwa na nia nyingine yoyote isipokuwa nia ya kuwachochea wananchi na kuwajengea chuki dhidi ya Serikali yao na Kiongozi wao Mkuu.

Ni matarajio yetu, kuwa Gazeti la Mwananchi litafanya jitihada za makusudi, kama taaluma ya uandishi wa habari inavyoelekeza, kutafuta usahihi wa jambo hili na kuwaambia Watanzania ukweli.

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
27 Julai, 2015

No comments :

Post a Comment