Friday, July 10, 2015

Vurugu Bagamoyo: Kituo cha Polisi Bunju chachomwa moto

Jengo la polisi likiteketea kwa moto
JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuchoma kituo kidogo cha Polisi kilichopo Bunju ‘A’ jijini Dar es Salam.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Camillus Wambura alisema tukio hilo lilitokea saa 3:00 asubuhi wakati Tanroads pamoja na Jeshi la Polisi walipokuwa katika mazungumzo ya kuweka matuta katika barabara hiyo.

Alisema kabla ya kuchomwa kituo hicho dereva aliyetambulika kwa



jina la Yohana John aliyekuwa akiendesha gari aina ya Coaster alisababisha ajali katika eneo hilo na kumgonga mwanafunzi mmoja wa shule ya Bunjua ‘A’ Radhia Omary na kusababisha kifo chake.

Alisema baada ya mwanafunzi huyo kupoteza maisha wanafunzi wa shule hiyo pamoja na wananchi wa eneo hilo walikusanyika na kulala barabarani hali iliyosababaisha magari kutoendelea na safari zake.

Alisema wananchi hao pamoja na wanafunzi walifunga barabara hiyo kwa muda wa saa tatu wakidai kuwa wanataka matuta yawekwe katika eneo hilo lililopo karibu na shule hiyo ili liweze kuwasaidia wanafunzi wakati wa kuvuka barabara.

Hali hiyo ilileta usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo kwa kufungwa na kushindwa kuendelea na shughuli zao hali iliyosababisha polisi kutumia nguvu kuwatawanya watu.
“Baada ya tukio hilo polisi na Tanroads tulikaa kikao cha dharura kilichokuwa kikielekeza utengenezwaji wa matuta ya haraka katika eneo hilo.
“Wakati tukiendelea na mazungumzo hayo wananchi walipata mwanya wa kukivamia kituo hicho na kukichoma moto.
“Sababu ya wananchi hao kuchoma kituo hicho hakuna, na wamefanya jambo ambalo si la busara na wamesahau kuwa kituo hicho kinawasaidia watu wote wa eneo hilo,” 
alisema Kamanda Wambura.

Alisema mbali na kuchoma kituo hicho pia wamechoma magari mamne ya watu binafsi yaliyokuwa yameegeshwa pembezoni mwa kituo hicho.

Pia alisema wanamshikilia dereva wa Coaster aliyesababisha ajali pamoja na gari hilo.

“Kwa sasa tupo katika zoezi la kuwasaka na kuwakamata watu wote waliosababisha vurugu hizo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake,” 
alisema Kamanda Wambura.

Shuhuda wa tukio hilo, Moshi Sultan, alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 3:00 asubuhi baada ya gari kumgonga mwanafunzi huyo aliyekuwa anakwenda shule.

Alisema baada ya tukio hilo wananchi wa eneo hilo walikusanyika na kufunga barabara hali iliyosababisha polisi kuingilia kati na kuanza mvutano kati yao na hatimaye wananchi hao kuvamia kituo hicho na kukichoma moto.

Alisema wananchi hao waliwasha moto kituoni hapo pamoja na tairi za gari na kudai kuwa askari waliopo hawafanyi kazi kwa umakini.

“Kutokuwapo kwa askari wa kutosha katika kituo hicho kumechangia wananchi hao kuvamia kwa urahisi na kuchoma moto kituo hicho,”
alisema.

Katika tukio jingine, moto mkubwa umezuka na kuteketeza nyumba yote inayomilikiwa na Hamisi Katori iliyopo katika mtaa wa Mabanda Marefu Ukonga Mombasa jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Lucas Mkondya, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.

Alisema wakati moto huo ukiendelea kuwaka alikuwepo mtoto mdogo mwenye umri wa miaka miwili aliyetambulika kwa jina la Mohamed Shabani ambaye alikuwa amelala ndani lakini msamaria mwema alifanikiwa kumuokoa.

Mkondya alisema moto huo uliteketeza nyumba yote, mali na thamani zilizoteketea kwa moto bado hazijafahamika.

Alisema hakuna madhara kwa binadamu, moto ulizimwa na kikosi cha Zimamoto Uokoaji cha Jiji kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.

Polisi wa wakijaribu kuwatawanya watu katika eneo la kituo cha Polisi Bunju baada ya wanachi kukichoma moto baada ya mwanafunzi wa shule kugongwa na gari na kufa papo hapo.



Moja ya Gari iliyokuwepo kituoni hapo ikiwa imenyofolewa vifaa vyake wakati wa vurugu hizo


Kituo cha Polisi cha Bunju kinavyoonekana baada ya kuchomwa moto.

Kituo cha Polisi cha Bunju A kikiteketea kwa moto.

Polisi akikagua uharibu katika moja ya gari lililokuwa kituoni hapo.
Imevunjwa kioo chote cha nyuma

Baadhi ya polisi wakiangalia uharibifu uliofaywa na baadhi ya watu waliovamia kituo hicho cha polisi Bunju,kufuatia tukio la kudaiwa kugongwa na gari mwanafunzi mmoja na kufa papo hapo.



Baadhi ya Polisi wakiwatawanya watu (hawapo pichani) kwa mabomu ya machozi mara baada ya tukio la kuchomwa moto kituo cha polisi Bunju, tukio hilo limetokea.Kituo cha polisi Bunju kilichopo nje kidogo ya jiji la Dar kimechomwa moto na baadhi ya Wananchi kufuatia tukio la kudaiwa kwa Mwanafunzi mmoja kugongwa na gari na kufa papo hapo.

No comments :

Post a Comment