Thursday, August 6, 2015

TAARIFA KAMILI: LIPUMBA AJIUZULU

Hali ya Umoja wa Vyama vya UKAWA inazidi kuwa tete baada ya Mwenyekiti wa Chama
Cha CUF, Prof. Ibrahim Lipumba kutangaza kujiuzulu nafasi yake ya Uenyekiti kwenye chama hicho. Hii ni mfululizo kwa yele yanayoendelea baada ya Mbunge wa Monduli kukaribishwa CHADEMA.

Tamko hilo la Prof. Lipumba linahitimisha siku mbili za minong’ono na tetesi zilizogubika medani ya kisiasa nchini kuwa kiongozi huyo anaondoka katika chama hicho hali iliyolazimu wananchama, wapenzi na mashabiki wa kiongozi huyo kufurika makao makuu ya chama hicho Buguruni Dar es Salaam jana ili kujua hatma ya kiongozi wao huyo.

Akizungumzia sababu za kujiuzulu kwake, Profesa Lipumba amesema amekerwa na hatua ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao CUF ni chama shiriki kushindwa kusimamia makubaliano yaliyopelekea kuundwa kwa umoja huo.

Amesema Ukawa ulianzishwa kulinda maslahi ya wananchi yaliyoainishwa kwenye Katiba iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba, na kwamba nafsi yake inamsuta hivi sasa kuendelea na uongozi huku waliokuwa wanaipinga Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba wakikaribishwa kuwania uongozi wa nchi kupitia umoja huo.

Prof. Lipumba amesema baada ya kujiuzulu atajikita kufanya shughuli za kitaaluma kwa kujihusisha zaidi na ushauri wa masuala ya uchumi na maendeleo.

No comments :

Post a Comment