Saturday, August 1, 2015

KAFULILA AFUTIWA KESI ALIYOFUNGULIWA NA IPTL NA PAP

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali kesi namba 301 iliyofunguliwa
na Kampuni ya kufua Umeme ya IPTL, PAP pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya PAP Bw Harbinder Singh Sethi dhidi ya Mbunge wa Kigoma Kusini, Mhe David Kafulila.

Kesi hiyo illikuwa ikidai kuwa Kafulila alichafua jina kampuni hizo na mhusika wake kwamba walichota zaidi ya shilingi bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta escrow kinyume cha sheria na taratibu.

Katika shauri hilo, Kampuni ya IPTL, PAP na Herbinder Singh Sethi walitaka Mahakama imwamuru Kafulila ailipe fidia ya sh. 310bn kwa kuchafua jina la kampuni na mkurugenzi huyo.

Katika kesi hiyo Kafulila alikuwa akitetewa na taasisi za kisheria za Legal & Human Rights Centre pamoja na kituo cha Human Rights Defenders.

Akitoa uamuzi huo mbele ya mawakili wa Human Rights Defenders na Legal & Human Rights Center wakiongozwa na wakili Mtobesya huku mawakili wa IPTL, PAP na Sethi wakiwa hawakufika mahakamani, Jaji Rosemary Teemba alisema Mahakama Kuu imejiridhisha kwamba kampuni ya IPTL, PAP na Mkurugenzi wao Harbinder Sethi hawakuwa na hoja za msingi kuthibitisha madai yao kama msingi wa kufungua kesi mahakama kuu na hivyo kwa kuzingatia hayo, Mahakama Kuu kanda ya Dar es salaam inatupilia mbali shauri hilo.

No comments :

Post a Comment