WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira (pichani), ameshinda kura za
maoni za CCM, baada ya kupata kura 6,429 na kumshinda mpinzani wake wa karibu ambaye ni mjasiriamali, Robert Maboto aliyepata kura 6,206.
Akitangaza matokeo hayo jana katika ofisi ya CCM ya Wilaya ya Bunda, Mkurugenzi wa uchaguzi katika wilaya hiyo, Magreth Mtatiro, alisema Wassira alimzidi mwenzake kwa kupata kura 6429.
Mtatiro alimtangaza mshindi wa tatu kuwa ni Mwenyekiti wa CCM mkoani Mara, Christopher Sanya aliyepata kura 1,140, ambapo wengine ni pamoja na Exavery Lugina aliyepata kura 846, Simon Odunga (547), Magesa Mugeta (446), Peres Magiri (385) na Burian Bitaa (263).
Kutokana na matokeo hayo, Mtatiro alimtangaza Waziri Wasira ambaye anatetea tena nafasi hiyo, kuwa mshindi katika kinyang’anyiro hicho cha kura za maoni. Wakati huohuo, mbunge aliyemaliza muda wake katika jimbo la Mwibara Kangi Lugola (pichani kulia), ameshinda uchaguzi katika kura za maoni za chama hicho na kumshinda kwa kura nyingi mpinzani wake wa karibu, Charles Kajege aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo.
No comments :
Post a Comment