Monday, August 3, 2015

TAKUKURU YAMSAFISHA NAPE


Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) mkoa wa Lindi, Steven Chami akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo wakati akikanusha tuhuma za rushwa dhidi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi (NEC-CCM), Nape Nnauye jana. (Na Mpigapicha Wetu).

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Lindi, imekanusha tuhuma za rushwa zilizoelezwa na baadhi ya vyombo vya habari dhidi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM), Nape Nnauye.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi yake siku ya Jmosi, Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Steven Chami alisema, taasisi hiyo haikumkamata Nape kwa sababu ya kuhusika na rushwa, bali ilitaka kujiridhisha na kiwango cha fedha kilichokuwa kikitolewa kwa mawakala.

Alisema, “Uhakiki ulifanywa kwa watu wote walioomba ridhaa ya kugombea nafasi mbalimbali mkoani humu, ikiwa ni pamoja na ubunge, ambao Nnauye na wengine waliomba."

Kutokana na maelezo yake, Nape alikuwa miongoni mwa wanasiasa walioomba ridhaa ya CCM kugombea ubunge katika jimbo la Mtama, na alikuwa pia miongoni mwa watangaza nia walioingia kuchukua fedha katika Benki ya NMB ya mjini hapa, iliyotajwa na vyombo vya habari.

Alifafanua kuwa, kitendo cha maofisa wa Takukuru kumfuata Nnauye ili wajiridhishe na kiwango cha fedha alichokitoa kwa ajili ya mawakala, kilichukuliwa kuwa ni kumkamata kwa rushwa jambo ambalo si kweli.

“Vijana wangu walimuomba Nnauye aongozane nao hadi ofisini ili wahakiki kiasi cha fedha alichokuwa amekitoa benki. Alifanya hivyo na kutumia dakika kati ya 30 na 45 kutoa maelezo yaliyowaridhisha maofisa wa Takukuru waliomwachia baada ya mahojiano mafupi. “...Ninapenda kuwathibitishia kuwa, Nnauye alikuwa na kiwango cha kawaida cha fedha ambacho kinaruhusiwa kutolewa kwa mawakala. Haikuwa rushwa kama ilivyopotoshwa na baadhi ya wanahabari walioandika na kutangaza habari hiyo,” Chami alisema na kuongeza kuwa alikutwa na Sh milioni tatu tu.

Alisema, Nnauye aliieleza Takukuru kuwa fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya kuwalipa mawakala wake 156, aliowaandaa kusimamia uchaguzi katika vituo vyote jimboni humo.

Kutokana na kadhia hiyo, Chami alivionya vyombo vya habari kuwa makini kuepuka kupotosha jamii kwa sababu, kufanya hivyo kunaweza kukaribisha uvunjifu wa amani.

No comments :

Post a Comment