Monday, June 29, 2015

Lipumba asema CCM hakiwezi kutoa rais mwadilifu

Mara. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema CCM hakina kiongozi mwadilifu atakayeweza kupeperusha bendera ya nchi, kutokana na viongozi wake kugubikwa na ufisadi.
Profesa Lipumba alitoa kauli hiyo jana kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Mkendo mjini Musoma alipokuwa akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara.
Alisema lengo la mkutano huo ni kuwaelimisha wananchi kuchagua viongozi wenye uadilifu na wanaojali rasilimali za nchi na watu wake badala ya kuchagua viongozi ambao ni mafisadi na wasio na uchungu wa kuinua pato la Tanzania.
Alisema anaunga mkono kauli ya mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Makongoro kuwa CCM kimekamatwa na kimekumbatiwa na vibaka ambao hawataki kuondoka ndani ya chama kwani wamekwishaweka mizizi.
“Nyerere atambue kuwa vibaka wakishang’ang’ania hawatoki na hata hayati Baba wa Taifa angekuwa hai angekuwa upinzani, hakika nawaeleza,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema anawashangaa viongozi wa CCM ambao wanataka kuongoza nchi wakati walishindwa kuwatetea Watanzania katika Bunge la Katiba ili ipatikane Katiba bora.
“Hawa waliweka masilahi mbele na kulinda nafasi na madaraka ya viongozi, kumbe lengo lao ni kuendelea kuwanyonya wananchi,” alisema.
“Katiba ile ilikuwa inampunguzia madaraka rais na pia ilikuwa inawapa wabunge nguvu ya kuihoji Serikali, ilipinga waziri kuwa wabunge ili Bunge liwe huru kujadili Serikali,” alisema.
Pia alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kujiandikisha kwa wingi na kuhakikisha kipindi cha kupiga kura kitakapofika, wachague wagombea wa Ukawa ili wanaodai kuwa haipo wapate kuijua.
Alisema kama isingekuwa sheria, vyama vyote vya upinzani vingekuwa chama kimoja na kupeperusha bendera ya Ukawa katika kuchagua viongozi kuanzia ngazi za udiwani, ubunge na urais.
“Nimetangaza nia nitagombea urais, lakini nasubiri kwanza Ukawa iamue ni nani anayefaa kugombea kupitia umoja huu, hata kama si mimi, nitahakikisha atakayepitishwa nitampigia kampeni ili nchi isiende kwa mafisadi,” alisema.


No comments :

Post a Comment