Sunday, June 28, 2015

NCCR- Mageuzi Wasema Hawana Mpango wa Kujitoa UKAWA

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema hakitajitoa katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na kuwapo kwa vikwazo vya ugawaji wa madaraka ndani ya umoja huo.

 Akizungumza katika kikao cha Kamati Kuu cha chama hicho kilichoketi jana katika Hoteli ya Travertine jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, alisema lengo la umoja huo lilikuwa ni kuunganisha nguvu ili kuwa na sauti moja ya ushirikiano.

“Yapo maneno mengi yamesemwa na waandishi, wachochezi  wanasema NCCR inataka kuvunja Ukawa, tangu lini mama akakata mkono wa mtoto wake?
 
“Kama kuna wenye wazo la sisi kujitoa kwenye umoja huu ni vizuri watambue kuwa hatuna  mpango huo, na hili ni azimio lililotolewa na wajumbe wa Halmashauri Kuu. Pia itambulike kuwa chama hiki ni zao la Ukawa, hivyo si jambo rahisi kujitoa,” alisema Mbatia.

  Alisema Ukawa si sehemu ya kugawana madaraka na kudai kuwa umoja huo unaangalia zaidi masilahi ya wananchi.

Mbatia alisisitiza pamoja na uchochezi uliopo na changamoto ya ugawaji majimbo, wanaamini watavuka kwa kuwa lengo ni kusaidia wananchi na si vyama husika.

 Alisema umoja huo umejipanga vizuri, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi  kwakuwa wana uwezo wa kutoa rais pamoja na viongozi wengine watakaounda Serikali.

Ajitosa  Sakata  la  Zanzibar

Aidha Mbatia alishagazwa na hatua ya Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kuvunja Baraza la Wawakilishi juzi bila tukio hilo kuhudhuriwa na Makamu  wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad  baada ya wabunge na wawakilishi kumkatalia kuhudhuria.

 “Nimeshangaa sana rais wa Zanzibar anavunja Bunge yupo mwenyewe  bila Maalim Seif. Nini maana ya Serikali ya Umoja wa Kitafa?” alihoji Mbatia.
 
Alisema wanachama wa vyama vya CCM na CUF wanapaswa kutambua kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ni makubaliano  na mali ya Wazanzibari wote na si wanasiasa pekee.

Akizungumzia kuhusu mwenendo wa uandikishaji wa daftari la wapigakura unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (BVR), alisema hakuna dalili za daftari hilo kukamilika kwa wakati kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji.

Alisema kutokana na hali hiyo, kuna viashiria vinavyoonyesha uchaguzi utakaofanyika Oktoba hautakuwa huru na wa haki.

“Uchaguzi hautakuwa huru na haki kwa sababu wameshindwa uandikishaji, kama leo wanasema kuna zaidi ya watu 5,000 wamejiandikisha mara mbili, wanamaanisha nini kwa wananchi?

“Tulishauri tangu mwaka jana kuhusu utaratibu wa uandikishaji na muda wa kuanza, lakini wenzetu wakawa wanabisha. Kwa hapa tulipofikia lolote likitokea  wa kulaumiwa ni Serikali ya CCM,” alisema Mbatia.

Alisema hadi sasa kuna baadhi ya mikoa ikiwamo Dar es Salaam na Pwani bado hawajaandikishwa. Pia NEC inapaswa kuwa na muda wa kuhakiki  majina ambako kutafanywa na wananchi.

Aliongeza kuwa Serikali ya awamu ya nne tangu ilipoingia madarakani mwaka 2005  imekuwa ikipoteza mvuto siku hadi siku kutokana na kutowajibika kwa ufasaha.
 
Alisema hadi sasa kuna mazingira ambayo mtu yeyote makini ni rahisi kuona jinsi Serikali ya CCM ilivyopoteza utashi, mvuto  na mwelekeo wa kuongoza Watanzania.

No comments :

Post a Comment