Tuesday, July 7, 2015

11 wauawa katika shambulio Mandera,Kenya

Shambulio limetokea kaskazini mashariki mwa Kenya ambapo inahofiwa kuwa takriban watu 11 wameuawa. Shambulio hilo linaaminiwa kuwalenga wafanyikazi wa machimbo ya mawe wasiokua wenyeji.
Walioshuhudia wameambia BBC kuwa walisikia mwanzo milipuko miwili kisha ikafuatiwa na milio ya risasi. Shirika la msalaba mwekundu linaongoza oparesheni ya kuwaokoa majeruhi ambao idadi kamili haijulikani bado.

Nani washambuliaji ?

Haijathibitishwa pia ni nani waliofanya shambulio hilo japo wanamgambo wa Al shabaab wamekuwa wakilenga wakaazi wasio wenyeji wa asili katika eneo hilo katika mashambulio yaliyotangulia.
Shambulio kama hilo dhidi ya wachimba migodi lilitokea jijini Mandera mwezi Disemba 2014, ambapo takriban watu 36 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Marudio ya shambulio

Mashambulio kama haya yametishia kudumaza shughuli katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya ambapo wengi wa wafanyikazi wake ni watu kutoka maeneo mingine ya Kenya.
Wafanyikazi hawa wamekuwa wakidai kutishiwa maisha, na wengi wa wafanyikazi kama vile walimu na hata wahudumu wa afya wamesusia kurejea kazini katika eneo hilo wakidai kutishiwa maisha yao.
Chini ya siku kumi zilizopita serikali ya Kenya iliondoa marufuku ya kutoka nje kuanzia magharibi hadi alfajiri, kufuatia wito kutoka kwa viongozi wa kiislamu waliodai kuwa marufuku hiyo inahujumu ibada za waislamu za usiku katika mwezi wa Ramadhani.
Asili mia kubwa ya wakaazi katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya, ni waislamu wa asili ya kisomali.
Source: BBC Swahili

No comments :

Post a Comment