Saturday, July 18, 2015

Eid el Fitr ni siku ya furaha, kufanya ibada

Tokeo la picha la eid al fitr
Waislam dunia nzima wamekamilisha ibada muhimu ya kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Furaha zimetawala kila kona, si kwa sababu sasa wameachiwa huru bali kwa sababu wamefaulu kutekeleza amri ya kufunga. 
Imesuniwa siku ya Eid kula chakula kizuri, kuvaa nguo nzuri na kufanya yote mazuri yanayompendeza Allah (S.W).
Nini maana ya Eid
Maana yake ni sikukuu, shehere au furaha.  Katika Uislam kuna sikukuu kubwa mbili: Eid el fitr (sikukuu ya kufungua swaumu) na Eid el Adhha (sikukuu ya kuchinja).
Eid al-Fitr ni sikukuu ya kumaliza kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhan.  Ni sikukuu ya kidini inayofanywa na Waislamu duniani kote.  Waumini wa dini hiyo kwa muda wa siku 29 au 30 walikuwa wamejinyima kula, kunywa, kukutana na wake/waume zao kimwili tokea jua linapochomoza (alfajiri) mpaka jua linapozama (magharibi). Wakati wa mfungo wa Ramadhan, Waislam walikuwa kwenye mafunzo maalumu (Chuo) kwa ajili ya kuwa wacha-Mungu.  Ni imani ya kiwango cha juu kwa mtu kujinyima kula na kunywa wakati chakula anacho, kujizuia asikutane na mkewe/mumewe wakati anao uwezo wa kufanya hivyo akitaka tena kwa siri ama kwa dhahiri.
Ni wakati wa kujifunza ugumu na uchungu wanaoupata masikini na mafukara kwa kukosa chakula.  Wakati wa Ramadhan Waislamu wote hata wenye fedha wanakuwa sawa na wasionacho wakati wa mchana, wote wanasikia njaa na kiu sawasawa.  Hiyo ni ibada inayomfanya muumini awe mnyenyekevu kwa Mungu wake, amekubali kuwa dhalili na kuhimili njaa na kiu kwa ajili ya Mola wake.
Mafunzo hayo yanayopatikana wakati wa Ramadhan, Waislam wanatakiwa wayachukue katika mfumo wao wa maisha wa mwaka mzima hadi Ramadhan nyingine iwafikie na waingie tena chuoni, wawe wanyenyekevu, wawakumbuke masikini na mafukara kwa kuwaondoshea njaa na kiu zao na hata kuwapa mahitaji yao mengine kama vile mavazi na makazi. 
Ramadhan ikimalizika Waislam hufurahia kufaulu kwao (kuhitimu chuo cha mafunzo ambako walikuwa wakifunga na kujibidiisha kufanya ibada za fardhi na za sunna).  Kwani katika mwezi wa Ramadhan wamehimizwa sana kumkurubia Mwenyezi Mungu na kumuomba msamaha.
Siku ya Eid ni siku ya kwanza ya Mfunguo Mosi (Shawwal). Eid al-Fitr ina swala maalumu ya rakaa mbili inayoswaliwa asubuhi baada ya swala ya alfajiri na baada ya watu kupata istiftahi (kufungua) hivyo huswaliwa kuanzia saa 1.30 hadi saa 3.00. Ni sunnah swala hiyo kuisali katika viwanja vya wazi.
Ni wajibu kwa Muislam kutoa Zakat-ul-Fitr.  Nayo ni zaka ya maumbile ni zaka ya kichwa (kama vile kodi) kwa maana ya kuwa kila mtu katika kaya analazimika kutolewa zaka hiyo hata kama ni mtoto mchanga wa siku moja. 
Zakat-ul-Fitr ni kile chakula au thamani ya chakula anachopaswa kukitoa mtu kabla ya Waislam hawajaswali Swala ya Eid el-Fitr.
Maana ya Zakat-ul-Fitr au Sadaqat-ul-Fitr ni “Sadaqa ya utakaso wa kufungua Swaum. Nacho ni kiwango fulani cha chakula kinachotolewa na Waislamu katika siku chache za mwisho wa Ramadhan au siku ya ‘Eid asubuhi, kabla ya kuswaliwa Swala ya Eid.
Zakat-ul-Fitri ni Fardhi (lazima) mbele ya kundi kubwa la wanazuoni (jopo la wataalamu wa fani ya Fiq-hi). Ufaradhi huu unatokana na hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah amuwiye radhi-kwamba yeye amesema:
“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amefaradhisha Zakat- ul-Fitri. Pishi ya tende au pishi ya shayiri, kwa mtumwa na muungwana, mwanamume na mwanamke, mtoto na mkubwa katika waislamu. Na ameamrisha itolewe kabla ya watu kutoka kwenda kuswali (yaani swala ya Eid)”. Bukhaariy na Muslim
Bwana Mtume ameifaradhisha Zakaatul-Fitri na kuamrisha itolewe katika mwaka ule ule uliofaradhishwa swaumu ya Ramadhani Yaani katika mwezi wa Shaaban, mwaka wa pili wa Hijrah.
Hekima
Zakat-ul-Fitri imefaradhishwa kwa hekima nyingi, miongoni mwake ni:-
Kuwasaidia wenye shida katika siku ya sikukuu ili furaha ienee kwa watu wote.
Kuunga mapungufu na kuziba makosa yanayoweza kuwa yamemtokea mtu katika swaumu yake.
Haya tunayafahamu kupitia hadithi ya Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kwamba yeye amesema:
“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alifaradhisha Zakaatul-Fitri ili kumtwaharisha mfungaji kutokana na maneno na matendo machafu. Na ili iwe chakula kwa masikini, atakayeitoa kabla ya swala basi hiyo ndiyo zaka
yenye kukubaliwa. Na atakayeitoa baada ya swala, basi hiyo ni sadaka kama sadaka nyinginezo,” Abuu Daawoud.
Nini kitolewe
Zimepokewa hadithi nyingi sahihi zinazoweka wazi alichowaamrisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-maswahaba wake kukitoa kwa ajili ya Zakaatul-Fitri. Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Abuu Saaid Al-khudriy-Allah amuwiye radhi-amesema:
“Tulikuwa wakati alipokuwa miongoni mwetu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-tukimtolea Zakat-ul-Fitri kila mkubwa na mdogo. Kibaba cha chakula, au kibaba cha shayiri, au kibaba cha zabibu au kibaba cha maziwa ya unga”- Bukhaariy na Muslim
Na imepokelewa kutoka kwa Abdillah Ibn Tha’alabah-Allah amuwiye radhi-amesema:
“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikhutubu siku moja au mbili kabla ya Eid akasema: Toeni kibaba cha ngano, au kibaba cha tende au cha shayiri. (mtoleeni) kila muungwana au mtumwa, mkubwa au mtoto”. Abuu Daawoud.
Mafaqihi wamesema mazingatio katika kutoa ni kuangalia chakula rasmi cha mahala husika, chakula kitumiwacho katika dhifa na shughuli zao mbali mbali.
Na kibaba kwa kipimo cha kilogramu ni sawa na ¾ ya kilogramu moja. Hiki ndicho kipimo kinachopaswa kutolewa kwa kila kichwa kimoja.
Wakati wa kutoa
Kutokana na riwaya ya Ibn ‘Abbas  (R.A) iliyotangulia, zakat-ul-fitr inatakikana kutolewa siku ya Eid, kabla ya Swala ya Eid.
Ikazidi kupokewa yakuwa Ibn ‘Umar (R.A) alikuwa akitoa siku moja au mbili kabla ya siku ya Eid. Kutokana na hayo imepatikana misingi ya ushahidi wa kutoa kwa siku chache kabla ya Eid. Lakini ni makosa kutoa mapema mno katika mwezi wa Ramadhan na kufanya hivyo itakuwa ni kwenda kinyume na hikima yake ya kuwa kafara ya madhambi wakati wa mwezi (wa Ramadhan), na kuwalisha wanaohitaji siku ya Eid.
Hata hivyo, inaruhusiwa kuwapa mapema wale wanaokusanya, ukiamini ya kwamba hawatozifikisha kwa wanaohitaji kabla ya mwisho wa mwezi (wa Ramadhan). Hivyo ndivyo ilivyokuwa ikifanywa wakati wa maswahaba, ilipokuwa wakusanyaji wakimaliza kukusanya siku moja au mbili kabla ya Eid.
Ukusanyaji
Inaruhusiwa kuchagua watu kukusanya zakat-ul-fitr miongoni mwao. Vilevile inaruhusiwa kuwapa (hiyo zaka) hao wakusanyaji iwapo wanahitaji na wanastahiki. Ibn ‘Umar (R.A) alikuwa akifanya hivyo. Ikazidi kusisitizwa kumchagua mtu kulinda zakat-ul-fitr iliyokusanywa. Mtume (S.A.W) alimchagua Abu Hurairah (R.A) kwa kazi hii.
Wanaopaswa kupewa Zakat-ul-Fitri ni wale wale wenye sifa ya kupewa Zaka ya faradhi ambao wametajwa katika kauli yake Allah:
“Sadaka hupewa (watu hawa): Mafakiri na masikini na wanaotiwa nguvu nyoyo zao (juu ya Uislamu) na katika kuwapa uungwana watumwa na katika kuwasaidia deni na katika (kutengeneza) mambo aliyoamrisha Allah na katika (kupewa) wasafiri (walioharibikiwa) ni fardhi inayotoka kwa Allah, na Allah ni Mjuzi na Mwenye Hekima.” [9:60]
Lakini masikini na mafakiri ndio walengwa khasa wa Zaakatul-Fitri kuliko mafungu mengine yaliyotajwa.
Zakaatul-Fitri ni wajibu kwa kila muislamu, mwenye uwezo wa kutoa hata kama hamiliki kiwango cha zaka ya fardhi. Mwenye kumiliki chakula chake na familia yake cha siku ya Eid, kinachozidi hapo ni wajibu akitoe kama Zakaatul-Fitri.
Atajitolea yeye mwenyewe na watu wote ambao chakula chao cha kila siku kinamuwajibikia yeye.
Hawa ni pamoja na wanawe ambao bado wanamtegemea yeye, wazazi wake, mkewe na wale wote walio chini ya ulezi wake kwa njia ya wajibu na wala sio kwa njia ya ihsaani/ khiari.
Wakati bora
Wakati bora kabisa wa kutoa Zakat-ul-Fitr ni ule usiku wa kuamkia siku ya Eid. Na ni wajibu itolewe kabla ya kuswaliwa swala ya Eid.
Na wajibu wa kutoa hauondoki kwa sababu ya kuchelewa kutoa. Bali itakuwa ni deni iliyo katika dhima ya aliyewajibikiwa kutoa.
Na itamlazimu kulipa deni hilo hata mwishoni mwa umri wake, kwa sababu aliwajibikiwa na akafanya uzembe kutoa. Na haisihi kuchelewa kutoa bila ya dharura na ni haramu kisheria.
Kwa sababu ucheleweshaji huu unapelekea kupotea kwa lengo la utoaji wake ambalo ni kuondosha uhitaji wa masikini katika siku ile ya furaha. Ambao Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amelizungumzia suala lao kwa kusema: “Waondosheni na udhalili wa kuomba katika siku hii”. Yaani siku ya Eid el Fitr.
Siku ya sikukuu ni siku ya furaha na imekatazwa kufanya machafu.  Mtume Muhammad (S.A.W) anasema:  “Anayeasi (anayefanya machafu) siku ya Eid ni sawa na kuwa amefanya machafu siku ya kuhesabiwa (siku ya kiyama).
Je, kuna mtu ambaye atadiriki kufanya machafu siku atakayohudhurishwa mbele ya Allah (S.W)?  Hivyo Waislam wanatahadharishwa kujikinga na kufanya uchafu wowote ule siku ya Eid eti kwa sababu ni siku ya kufurahi hivyo watu huamua kufurahika hata kwa kumuasi Mwenyezi Mungu.
Siku ya Eid el Fitr ni siku ya kuswali, kula, kunywa, kutembelea ndugu, jamaa na marafiki na wala si siku ambayo mashetani hufunguliwa ili watu wamuasi Mungu.
Imeandaliwa na Na Hawra Shamte, Mwananchi

No comments :

Post a Comment