Friday, July 24, 2015

MADAI YA RUSHWA: UCHAGUZI CHADEMA WAVURUGIKA

Wajumbe wa mkutano maalumu wa uchaguzi wa
Wajumbe wa mkutano maalumu wa uchaguzi wa Chadema Moshi Mjini, wakishangilia baada ya msimamizi wa uchaguzi kumtangaza Jafary Michael kuwa mgombea  ubunge wa jimbo hilo. 
Dar/mikoani. Uchaguzi wa kura za maoni ndani ya Chadema katika Jimbo la Bariadi umeahirishwa baada ya kubainika kwa matukio yanayoashiria vitendo vya rushwa.
Wakizungumza baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo, wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya walisema hawataki kuingiliwa na virusi vya rushwa ndani ya chama hicho, kwa kuwa hali hiyo italeta mpasuko na makundi.
Wajumbe hao wameutaka uongozi Chadema kuwa makini na wanachama mamluki wanaohama kutoka vyama vingine vya upinzani ili wasikivuruge.
“Hatua ya kuahirishwa kwa uchaguzi inaonyesha ni namna gani chama kilivyo makini ili wanaotoa rushwa wajifunze umakini huu na wananchi waelewe kuwa chama kinatetea wanyonge,” alisema Makula Saguda.
Hata hivyo, mjumbe mwingine, Masanja Lujani alipinga hatua hiyo akisema kuahirishwa uchaguzi ni ubadhilifu ambao haufai akisisitiza kuwa kama wamekamata mtu akiwa anagawa rushwa wangemtoa katika uchaguzi na wengine wakaendelea.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Emmanuel Mbise alisema uchaguzi huo umeahirishwa baada ya kukamata watu wakigawa rushwa kwa baadhi ya wagombea.
“Chadema kinaaminiwa na kinapendwa na watu kwa sababu hakikubaliani na rushwa, kwa mujibu wa katiba na mamlaka niliyopewa, nimeamua kuahirisha uchaguzi hadi utakapotangazwa tena kutokana na uchaguzi huu kutawaliwa na rushwa,” alisema Mbise.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Simiyu, Wilson Mshuda ambaye pia ni mgombea katika jimbo hilo alisema: “Hatuwezi kunyamaza kimya, hata katiba ya chama kuanzia ukurasa wa 86 inaongelea mgombea ambaye ataonekana kutoa rushwa kwa wajumbe kuwa atakuwa amejiondoa katika kinyang’anyiro.”
Jimbo la Bariadi lina wagombea 12 ambao ni Godwin Simba, Mshuda, Masanja Madoshi, Seni Silanga, Manyangu Kulemwa, Zacharia Shigukulu, Maendeleo Makoye, Sweya Makungu, Sitta Mulomo, Wilson Limbu, Slivatus Masanja na Ntemi Ndamo.
Ndesa: Jimbo haliondoki
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo  amesema pamoja na kuwa hatagombea nafasi hiyo, CCM isitarajie kulikomboa jimbo hilo.Ndesamburo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa kumpata mgombea ubunge. 
“Wenzetu hawa wa kijani (CCM) wamejipanga walikuwa wanasubiri tu Ndesa ateremke ili wachukue jimbo lakini ng’o. Ndesa niko nyuma yenu na siyo kwamba nitawaacha,” alisema.
“Kwa miaka 10 nimefanya kazi na Basil Lema kama msaidizi wangu, ananielewa na anajua shughuli zangu, namwamini lakini naye anagombea. Basil unaniacha na nani?” Ndesa alimhoji Lema.
Kutokana na kauli hiyo ya Ndesamburo, Lema ambaye pia ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro aliamua kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.
Kujiondoa kwake kulifanya mchuano ubakie kati ya wakili wa kujitegemea Elikunda Kipoko na Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael ambaye anaungwa mkono na Ndesamburo.
Katika uchaguzi huo Meya Michael alipata ushindi wa kishindo wa kura 221 dhidi ya kura tisa za Kipoko. Katika viti maalumu, Mbunge anayemaliza muda wake, Lucy Owenye aliibuka mshindi kwa kura 76 akifuatiwa na Upendo Maforo aliyeambulia 14 huku Rehema Makupa akipata sifuri.
Matokeo mengine
Korogwe Vijijini: Emmanuel Kimea (159) Amina Saguti (50), Augustine Kisaka (40), Damas Damian (2), Sophia Mohamed (2) na Iddi Kanyemka (0).
Viti maalumu, Amina Saguti (28), Sophia Mhando (8) na Monica Mbuva (6).
Handeni Mjini: Viti maalumu; Miriam Ndosi (44) kura 5 za hapana, mbili zimeharibika.
Karagwe: Viti maalumu; Jeni Pesha (34) Reveliana Thadeo (33), Selina Nguma (15), Honoratha Byarushengo (3), Janeth Mjungu (3) na Aneth Bagonza (1).
Bagamoyo: Andrew Kasambala alipata kura zote 56.
Kibaha Vijijini: Editha Bubeiya (79) Kinabo Edward (32), Elly Achahofu (26) na Rose Mkonyi (13).
Chalinze: Chacha Machera (69) Mathayo Torongei (53) na Yahya Mohamed a(18).
Ngara: Peter Bujari ( 230) Lingson Kasomwa (19) na David Kibenza (6).
Muleba Kusini: aliyeshinda ni Kashasira Alistides aliyepata kura 221 akifuatiwa na Lutembeka Loderick 160, Muchunguzi Kabonaki 50 na Aidan Kamushanga kura 2.
Karatu: Willy Kambala (217) Lazaro Maasay (81).
Biharamulo: Dk Anthony Mbasa hakuwa na mpinzani.

No comments :

Post a Comment