Wednesday, July 8, 2015

MWANAUME MZEE ZAIDI DUNIANI AAGA DUNIA



Mwanamme mzee zaidi duniani raia wa Japan Sakari Momoi ameaga dunia mjini Tokyo akiwa na umri wa miaka 112.
Mwalimu huyo mkuu wa zamani wa shule ya upili na baba wa watoto watano, aliaga dunia kutoka na ugonjwa wa figo katika kituo kimoja cha kuwahudumia watu wazee siku ya Jumapili.
Alikuwa ametambuliwa na Guinness World Records mwezi Agosti.
Momoi alizaliwa mwaka 1903 mjini Fukushima na alikuwa mwalimu kabla ya kupanda cheo na kuwa mwalimu mkuu kwenye shule kadha nyumbani kwao.
Alikuwa na mazoea ya kusoma hasa mashairi ya Kijapan na pia alipenda kusafiri sehemu mbali mbali nchini Japan na mkewe ambaye sasa pia marehemu.
Wakati alipata cheti kutoka kwa Guinness World Records mwezi Agosti aliwaambia waandishi wa habari alitaka kuishi miaka miwili zaidi. Guinness bado haijatangaza mwanamamme mwenye umri mkubwa zaidi duniani baada ya Momoi.
Mwezi Aprili mtu mzee zaidi na mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi duniani Misao Okawa kutoka Japan aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 117 na sasa rekodi inashikiliwa na mmarekani Susannah Mushatt Jones ambaye ana umri wa miaka 116.
Mtu ambaye aliishi miaka mingi zaidi duniani kulingana na Guinness ni Jeanne Calment kutoka ufaransa ambaye aliishi miaka 122 na siku 164 . Aliaga dunia mwezi Agosti mwaka 1997.
Source: BBC Swahili

No comments :

Post a Comment