Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimejigamba kwamba kimeweza kuzuia ‘mafuriko’ kwa mikono huku kikiwatakia kila la kheri baadhi ya makada wake waliotangaza kutogombea kupitia chama hicho pamoja na wale waliokihama na wanaotaka kukihama.
Mwishoni mwa wiki iliyopita waliokuwa madiwani jimbo la Monduli kupitia CCM mkoani Arusha, walitangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku wabunge wa viti maalum, Ester Bulaya na James Lembeli aliyekuwa Mbunge wa Kahama wakitangaza kutogombea kupitia chama hicho.
Akiungumza na waandishi wa habari jana Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema CCM hakina uwezo wa kuzuia mtu anayetaka kukihama kwa sababu hiyo ndiyo demokrasia.
Aidha, Nape alisema vyombo vya habari vilimnukuu aliyekuwa mgombea urais kupitia CCM, Edward Lowassa akisema kuwa watu hawawezi kuzuia ‘mafuriko’ kwa mikono na kwamba CCM imeweza kufanya hivyo, lakini habari hizo haziandikwi.
Alisema wanachama wanaotaka kuhama hawawezi kuzuiwa kwa namna yoyote na kwamba hilo ni jambo la kawaida kufanyika kwa kada yoyote.
Akizungumzia mchakato wa kumpata mgombea urais, ulivyokuwa ndani ya CCM, alisema ulifuata utaratibu na kanuni zote na kwamba kama maneno mengi yataendelea kusemwa atatoa video inayoonyesha kila kitu kilivyokuwa ndani ya kikao cha Kamati Kuu (CC).
Kuhusu makada waliokihama chama hicho na kujiunga na Chadema, Nnauye alisema baada ya Baraza la Madiwani kuvunjwa hapakuwa tena na wawakilishi wa aina hiyo.
Alisema watu waliojiunga na Chadema huko Monduli mkoani Arusha hawakuwa Madiwani kwa kuwa Baraza la Madiwani likishavunjwa hakuna tena nafasi hizo za uwakilishi.
No comments :
Post a Comment