Ni ukweli usiopingika kwamba siku ya kuzaliwa na kufa ya kila binadamu anaijua Mungu.
Akiamua kukuita kwake, huwezi kupinga kifo kwa namna yoyote. Hata maandiko katika vitabu vitakatifu yanaeleza: “Sisi ni wa kwake na kwake tutarejea.”
Akiamua kukuita kwake, huwezi kupinga kifo kwa namna yoyote. Hata maandiko katika vitabu vitakatifu yanaeleza: “Sisi ni wa kwake na kwake tutarejea.”
Shadrack ni mmoja wa mejeruhi wanne walionusurika kifo wakati watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walipovamia Kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga jijini Dar es Salaam na kuua watu saba, wakiwamo askari wanne na raia watatu ambapo walipora bunduki zaidi ya 20.
Siku chache baada ya tukio hilo, mwandishi wa gazeti la Mwananchi alimtafuta Shadrack ambaye ana cheo cha konstebo, ili kufanya mahojiano naye kuhusu tukio hilo na jinsi alivyonusurika.
Hata hiyvo haikuwa kazi rahisi kukutana naye hasa kutokana na mazingira ya tukio lenyewe ambayo yameacha maswali mengi. Mwandishi alilazimika kupitia kwa viongozi kadhaa wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) alipokuwa amelazwa Shadrack ili kufanikisha kuonana naye kwa mahojiano.
Mwandishi alifika kwenye Wodi ya Kibasila aliyokuwa amelezwa, nikamkuta ameketi kitandani. Nilijimbulisha naye akawa huru kusimulia hali ilivyokuwa siku ya tukio.
Majambazi walivyoingia
Konstebo Shadrack aliyejeruhiwa bega la kulia na kifua, anasimulia kuwa siku hiyo ya tukio alikuwapo kwenye lindo kituoni hapo, kabla ya wanaume wanane kufika na kudai wamedhulumiana.
“Ilikuwa saa 4 kuelekea saa 5 usiku. Lilikuja kundi la wanaume wanane wakiwa wamevaa makoti makubwa, lakini hawakufunika nyuso. Walikuwa wakilalamika, ‘haiwezekani unidhulumu’ huku wakielekea ndani ya kituo"
"Kwa utaratibu wetu, mtu akifika kituoni lazima apite getini kwa mlinzi kwa ajili ya kupewa maelekezo, ili aende ndani. Lakini wao walitaka kwenda moja kwa moja,” anabainisha Konstebo Shadrack.
Walivyoshambulia polisi
Anasimulia kuwa kutokana na kutofuatwa utaratibu huo wa kuanzia getini, aliwaita watu hao kwa ajili ya kuwapa maelekezo ya kwenda ndani. Wakati huo alikuwa na askari wenzake wanne eneo hilo nje ya Kituo cha Polisi Sitakishari.
“…Kitendo cha kuwaita na kuwauliza mnakwenda wapi, jamaa waligeuka na kuvua makoti, kumbe ndani walikuwa na bunduki, ” anasimulia Shadrack.
“Wakaanza kutushambulia mimi na askari wenzangu, ambao walianguka chini huku wengine wakifyatua risasi juu. Nikageuka haraka na kulalia tumbo, lakini wakati nageuka, jambazi mmoja alinipiga risasi iliyonipata kwenye bega la kulia na kifuani,” anasema konstebo huyo huku akionyesha majeraha hayo.
Anabainisha kwamba baada ya hapo, majambazi hao waliingia kituoni na kuendelea kufyatua risasi, lakini mmoja wao alibaki nje ya kituo.
Alivyomchapa jambazi
“Nilitumia mwanya huo nikiwa tayari majeruhi, nikanyanyua bunduki niliyokuwa nayo na kumfyatulia risasi. Akandondoka na mimi nikakimbia,”anasema na kuongeza kuwa wakati majambazi hao walipoingia yeye na askari mwenzake waliokuwa lindo walikuwa na silaha zao mkononi.
“Kwa kuwa nilikuwa nimeumia na sikujua huko mbele ningekutana na nini, sikukimbilia mbali. Nilijificha kwenye shamba la mahindi jirani na kituo,”anaongeza.
Konstebo Shadrack anazidi kusimulia: “Lakini wakati nakimbia, njiani umbali wa kama mita 200 hivi tangu kilipo kituo cha polisi, nilikuta pikipiki kama nane hivi zimeegeshwa. Zilikuwa zimeelekezwa upande wa njiapanda ya kwenda Segerea. Nadhani walikuwa tayari kwa ajili ya kuondoka, baada ya kutimiza lengo lao.”
Anasema alilala katika ya shamba hilo la mahindi kwa muda, hadi aliposikia pikipiki zimepita na kwamba hakukuwa na milio ya risasi tena.
Alivyorudu kituoni
“Nilirudi kituoni kwa kujikongoja taratibu. Nilivyofika nje ya kituo niliwagusa wale askari waliokuwa pale nje wameanguka, mapigo yao ya moyo yalikuwa yamesimama, nikahisi wameshafariki".
Niliingia ndani, pia nikakuta wale wakiokuwa mapokezi wamepigwa risasi. Wakati huo pia wananchi na baadhi ya askari wanaoishi maeneo ya jirani, walianza kufika na kutoa taarifa ili ile miili ije kuchukuliwa,”anasema.
Alivyopelekwa MNH
Anaeleza kwamba, baada ya muda kidogo, alipata msaada wa kupelekwa hospitali kwa ajili ya huduma ya kwanza, kabla ya kupelekwa MNH kwa uchunguzi zaidi.
“Hata hivyo, nashukuru Mungu nilivyoletwa hapa Muhimbili, sikuonekana kuwa na tatizo kubwa sana. Walinichunguza na kuniambia kwamba sijavunjia mfupa, bali nimechanika,” anasema askari huyo.
No comments :
Post a Comment