Wednesday, July 22, 2015

PWANI: JESHI LA POLISI YANASA SILAHA ZA MOTO

                        Kamishna wa Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani, ACP Jafari Ibrahim akionesha silaha zilizokamatwa na jeshi hilo katika mapori ya mkoa huo
JESHI  la Polisi mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na wasamaria wema, limefanikiwa kukamata silaha mbalimbali zinazotumika katika matukio ya kihalifu katika mapori ya mkoa huo.Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake Jafari Ibrahim, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) amesema, 

"Tulifanya opereshani na misako maeneo mbalimbali kati ya 20 Juni hadi 20 Julai mwaka huu. Tulifanikiwa kukamata bunduki aina ya SMG no. 14302621, risasi 30 za SMG ndani ya Magazine na visu 11.”
“Tulikamata bunduki mbili zilizotengenezwa kienyeji, bunduki moja aina ya rifle, risasi 103 za short gun, risasi 20 za SMG, jambia tatu, mapanga manne, bomu mlipuko wa kutengeneza kienyeji matatu, vipande vidogo vya nondo 42, fyuzi zilizotegwa 24, fyuzi zilizo tupu 56, water gel explosive tatu, silcon rubber 100% na nyaya tatu za milipuko,” amesema ACP Ibrahim.
ACP Ibrahim amesema katika tukio la ukamataji silaha hizo pia wamefanikiwa kukamata watuhumiwa 27.
Aidha, amesema 12 julai mwaka huu katika eneo la Misugusugu wilaya ya Kibaha walifanikiwa kumkamata Hassan Justine maarufu kwa jina la Mbwambo (23) mkazi wa Kigogo Feri Dar es Salaam, akiwa na silaha aina ya short gun yenye namba G.74533 wakati akijiandaa kufanya uhalifu kwenye kituo cha mafuta cha Camel.
Justine amekiri kuhusika na matukio mengine ya uporaji kwenye kituo cha mafuta cha Mogas eneo la Mwendapole wilaya ya Kibaha na Mkata wilaya ya Handeni, Tanga.
“Tarehe 10 Mei mwaka huu, majira ya saa nane usiku wilaya ya Kisarawe askari askari walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Mohamed Kitumbi akiwa na vipande 24 vya meno ya tembo vyenye uzito Kg 42 ndani ya mfuko wa sulphate akiwa amepakia kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 660 AGP aina ya boxer vyenye thamani ya Sh. 182.7 milioni,” amesema ACP Ibrahimu.
Mbali na kukamatwa kwa vipande vya meno ya tembo pia, 5 Julai walifanikiwa kuwakamata Jumbe Abdukarim Ngohengo na Omary Yusuph wakiwa na noti bandia 370 za Sh. 10,000 wakiwa na lengo la kuingiza fedha hizo kwenye simu za kupitia kwa wakala wa airtel Money. Watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.
ACP Ibrahim amesema, katika kipindi hicho wamefanikiwa kukamata gunia 18 za bhangi zilizokuwa zinasafirishwa kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam kwa gari namba T. 335 DCX, aina ya Super Custom. Mtuhumiwa ni Maulid Abdalah, mkazi wa Manzese Midizini.
Mbali na kukamata bangi hiyo, pia walikamata kilo 124 za mirungi zilizokuwa zikisafirishwa katika mabasi yenye namba za usajili T. 678 CRT mali ya kampuni ya Burudan na gari namba T.575 BLN mali ya kampuni ya Simba Mtoto.
Pia, walifanikiwa kukamata lita 88 za pombe ya moshi, mitambo mitatu ya kutengeneza pombe hiyo na jumala ya watuhumiwa 47 ambao ni watumiaji na wauzaji wa pombe hiyo walikamatwa na kufikishwa mahakamani.
“Tunawaomba wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono juhudi zetu kwa kutoa taarifa za kiintelijensia juu ya uhalifu ili mafanikio haya yaliyopatikana kwa kipindi cha mwezi mmoja yawe na mafanikio endelevu na jamii iweze kuishi kwa amani na utulivu,” amesisitiza ACP Ibrahim.

No comments :

Post a Comment