Wednesday, August 5, 2015

Bila sera zenye tija Lowassa atakwama Ukawa


Mtikisiko wa aina yake umesikika katika siasa nchini baada ya Waziri Mkuu wa zamani
Edward Lowassa kuhamia Chadema, chama tangulizi katika muungano wa vyama vinne vya siasa vinayounda umoja ambao mwanzo wake ulikuwa ni suala la katiba, yaani Ukawa. 

Kuna mijadala miwili ambayo inasikika, ila wa tatu ambao hausikiki unaweza kuwa muhimu zaidi. Kuna mjadala kwa sababu utambulishaji wa vyama vya siasa kwa itikadi zao umebadilika ghafla. Watu wanaanza kuuliza wengine wako wapi.

Bila kufuatilia kwa kina mijadala ya kiitikadi inayoendelea, labda liulizwe swali kama hali hii ni njema au ni mbaya, na kama kawaida hilo ni swali la kiitikadi. 

Jicho la haraka katika vyombo vya habari linaonyesha kuwa hali hii ni njema kwa upinzani na mbaya kwa chama tawala.

Kinachofuata ni kama walitazamia hilo au la na jibu kwa haraka ni hapana, walidhani Lowassa baada ya kukatwa atanywea tu na pia kutokana na umri wake au afya yake hataweza mikikimikiki upinzani. Ilitazamiwa kuwa atatulia, kumbe atadiriki na amethubutu.

Mwenyekiti Mbowe alikumbushia katika hotuba yake hafla ya kumpa kadi Lowassa na mkewe kuwa 'huku kuna mabomu,' ya polisi ambayo huvuruga mikutano ya chama hicho. 

Wengine wakasikika wakisema kuwa vijana wa jeshi la polisi wanamfahamu na wanamstahi Lowassa - labda tutazamie kuwa itakuwa hivyo, ili jazba na kulazimisha katika chama tawala visije kuharibu amani, au kuvuruga kabisa uchaguzi mkuu. 

Kuna dhamira ya 'goli la mkono' na hata kuotea mchana kweupe, endapo chama tawala kitahisi 'maji marefu.'

Akiwa katika ziara nchini Australia, Rais Jakaya Kikwete alipewa sifa nyingi za kuheshimu vipindi vya uongozi na kuwa na dhamira ya kuondoka madarakani kwa utaratibu unaofahamika. 

Hilo halina shaka ila matazamio ya kukabidhi madaraka kwa mtu anayekubalika kwake na kwa chama tawala kwa jumla. 

Hapo kuna mtihani ambao chama tawala kinaweza kuuzembea, kuzidisha mabomu na wapiga kura kutambua dhamira au kufaulu nia hiyo.

Wakati CCM inajiandaa kuendelea na madaraka ya nchi, upinzani hausisitizi bado uwezekano wa kutwaa madaraka lakini mlingano bora zaidi bungeni kati ya chama tawala na upinzani. 

Ina maana itakuwa vigumu zaidi kwa serikali kuleta miswada bungeni ambayo haikubaliki kwa upinzani, ilazimike kuifanyia ukarabati isikwame. 

Hilo ni jambo jema kama CCM na upinzani watakuwa na sera zinazoeleweka na ugomvi uwe ni kitu halisi, sahihi, siyo fitina za rushwa kwa maslahi ya vikundi tofauti vya Bunge. 

Katika mazingira ambako sera za vyama vya siasa zinaeleweka, na zinalenga uchumi na hivyo kujenga mifumo imara ya jamii ambako matumaini ya kila eneo nchini yanakua na siyo kudidimia, upinzani imara ni jambo jema.

Ni uwezo wa kurekebisha miswada ya sheria tofauti kwani hata Bajeti ya Serikali ni muswada mmojawapo) kuelekea kwenye tija zaidi, au kupunguza upendeleo kisera au kundi la maslahi kwa aina moja au nyingine. Lakini pale Bunge linapokuwa ni makundi tofauti ya maslahi, uboreshaji haupo, ni fitina.

Ndiyo hapo inabidi kuangalia ujio wa Lowassa katika upinzani, na kutafuta nini hasa kinaimarishwa katika upinzani, na uwezekano wa hali hiyo kuwa na tija kwa uchumi wa nchi, utengemano na amani. 

Bado hapo yako maswali mengi, kwani utamnbulishaji wa itikadi sasa unakwama, na haielekei kuwa ziko itikadi mpya, nje ya kaulimbiu, ambazo siyo rahisi kusema zimefanyiwa kazi kiasi cha kutambuliwa kama itikadi. Chadema kwa mfano imeacha sera ya kupambana na ufisadi iingie katika kupambana na umasikini.

Hapo unajiuliza kama mwekeleo huo ni mpya kwa upande wa Chadema, kwani umaskini ulikuwa unaelezewa kuwa unatokana na ufisadi serikalini, hoja ambayo sasa imehamia chama kipya cha ACT-Wazalendo. 

CCM wataendelea kusifu juhudi za Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa (Takukuru) hata za kubuni kesi inayotokana tu na utendaji uliokubaliwa na mamlaka kuu za serikali, iwe ni kosa la jinai na serikali ikae kimya.

Ni katika mazingira hayo ambako fitina hutawala na dira huparaganyika.

Kwa kukubali ujio wa Lowassa ni wazi Chadema haitaendelea kujikita katika hoja rahisi ya ufisadi kuwa ndiyo sababu ya umaskini nchin badala yake walenge nguvu zao katika mfumo.

Inabidi sasa wadiriki na Lowassa pamoja nao kuacha fikra za Mwalimu za kurudia mageuzi. Ubinafsishaji, hasa.

Hapa tulipo hakuna mtu anayeweza kukwepa kutumia bidhaa za umeme zinazozalishwa na Tanesco. 

Ni shirika ambalo linaweza kujipangia faida kwa mwaka kwa kujua tu idadi ya watu wanaotumia umeme kwa wakati huo, tofauti na wenye maduka au wanaouza muda wa simu hawawezi kujipangia faida kwa kujua idadi ya watu, ila kwa makisio tata kihesabu. 

Lakini kutokana na shirika hilo kuwa kaika mikono ya serikali, halina tija yoyote, linaingia mikataba ya gharama kubwa ya fedha za kinga ya matumizi ya mitambo (wanayojifanya ni gharama za uwekezaji wakati sivyo). Ni kuogopa hasara pindi shirika likisusa umeme.

Kuendelea na mageuzi kutaleta katika upinzani lugha mpya kuwaunganisha pamoja, halafu hisia mpya miongoni mwa wananchi kuwa mabadiliko sasa yameanza. 

Nje ya mageuzi ya uchumi dhana kuwa jibu la matatizo ya sasa ya wananchi ni kuiondoa CCM madarakani inakuwa haina tija, kwani haitaji mbinu ni zipi zinakuwa siri ya viongozi wa chama ambao ukweli ni kwamba hawanazo ni watalaamu tu wa kuanika maovu ya CCM.

Kazi hiyo siyo iliyompeleka Lowassa upinzani, lakini kama hataanza kuuelekeza umoja huo katika sera zenye tija atakwama. Bado anafurahia sera za awamu ya tatu kufukuza makampuni, kubinafsisha asilimia 35, 49 au 51, zilizokwama pia.

CHANZO:IMEANDALIWA NA  ANI JOZEN

No comments :

Post a Comment