Sunday, June 28, 2015

UTUMIAJI WA UNGA WA DONA ISIYOTENGENEZWA VIZURI NI HATARI KWA AFYA YAKO



Na Mtaalamu wa chakula

Utangulizi
Unga wa mahindi ni chanzo kikubwa cha virutubisho kwa watu wengi Barani Afrika. Virutubisho kama vile wanga, protini, madini na vitamin hupatikana kutoka kwenye mahindi au unga wake.
Unga wa dona ni unga unaopatikana kwa kusaga mahindi bila ya kukoboa. Siku za hivi karibuni kumekua na uhimizo mkubwa sana wa matumizi ya unga wa dona na kufanya watu wengi kuanza kupunguza taratibu matumizi ya unga sembe au uliokobolewa.

Faida za unga wa dona
Unga wa dona ulioandaliwa vizuri huwa una faida nyingi sana zaidi ya hata unga ambao umekobolewa. Faida hizo ni za kiuchumi au hata za kiafya. Faida ya kiuchumi ni kwamba Ukisaga mahindi au nafaka zingine bila ya kukoboa unapata unga mwingi kwa kila kilo utakayoisaga. Hii ni kwa sababu ukoboaji wa mahindi kunapoteza kiasi fulani cha unga. Faida zingine kiuchumi ni uandaaji kuwa rahisi zaidi katika ngazi ya familia. Kwa upande mwingine wa faida za kiafya za unga usiokobolewa kuwa na kiasi kikubwa cha mafuta, protini, madini, vitamini, na nyuzinyuzi (fibre). Kwahiyo, unaimarisha zaidi lishe ya mlaji. Kama watu watajenga tabia ya kula mahindi ya kuchoma, kuchemsha au kupika kande pia wanapata faida kubwa ikiwemo kupata choo kikubwa mara kwa mara.

Udhibiti wa ubora katika hatua za utengenezaji wa unga wa dona
Dona yenye ubora na usalama inaweza kupatikana iwapo tu kunaudhibiti wa ubora katikatika mchakato wa utengenezaji. Udhibiti huo unatakia kuanzia mashambani, uvunaji, uhifadhi wa mahindi, hadi usagaji.

Nafaka zisipo vunwa, kukaushwa vizuri na kuhifadhiwa katika hali nzuri huweza kushambuliwa na wadudu waharibifu na vijidudu kama vile "fangasi" ambao mwisho wa siku huweza kusababisha nafaka au zao la nafaka kupungua ubora wake na kupata uambukizo wa "sumu kuvu" au kwa kitaalamu "aflatoxin". Aflatoxin huweza kuleta madhara makubwa kwenye miili ya binadamu kwa kusababisha cancer.

Vile vile iwapo udhibiti wa ubora hautazingatiwa katika hatua za uhifadhi hasa kwenye kuweka dawa za kuhifadhia mahindi "viatilifu" na usagaji wa mahindi. Kunauwezekano mkubwa sana kwa unga wa dona kubakiwa na kiwango kikubwa cha viatilifu au madawa ya kuhifadhia. Madawa hayo yanaweza kuwa ni sumu ambazo zinaweza zikamletea madhara makubwa mtumiaji wa unga huo. Kutokana na hilo basi ni muhimu nafaka zikahifadhiwa kwa mda unaofaa mara baada ya kuwekewa dawa kabla hazijafanyiwa mchakato mwingine wa kusagwa au kukobolewa.
Katika mashine za kusaga unga zilizopo kwenye maeneo yetu tunayoishi, suala la kuosha mahindi huwa halitiliwi maanani sana. Kutokana na ukweli kwamba mahindi mengi huwa yana kuwa na mabaki ya viatilifu suala la kuosha mahindi linatakiwa kuwa ni la lazima ili kuweza kuondoa au kupunguza kiwango cha madawa kilichopo kwenye mahindi.

Suala jingine la kujiuliza ni kwamba mara nyingi pumba za mahindi ndicho chakula kikubwa cha mifugo, lakini kiuhalisia sehemu ya nje ya nafaka/pumba za mahindi ndiyo sehemu ambayo huwa ina kiwango kikubwa zaidi cha dawa ili kuwazuia wadudu waharibifu. Kwahiyo mwisho wa siku sumu hizo huweza kuturudia kupitia mifugo.
Nini cha kufanya?
1. Ili kuweza kuepukana na madhara haya ya sumu za kuhifadhia nafaka na sumu kuvu ni budi kwa watanzania kurudisha utamaduni wetu wa zamani wa kujiandalia vitu vyetu wenyewe. Andaa mahindi yako mwenyewe kwa kuyaosha na kuyakausha vizuri kabla ya kusaga badala ya kwenda dukani na kununua. Dona ambayo hujui imeandaliwaje kabla ya kusagwa inaweza ikakuletea madhara makubwa zaidi ya faida ulizodhani ungezipata. Baada ya kusaga unga hakikisha unaukasha vizuri kabla ya kuhifadhi.

2. Kupunguza matumizi ya pumba kwa mifugo, na kuanza kuipa vyakula muhimu au mbadala kama vile nyasi badala ya kuilisha pumba, kwani pumba hizo huwa zina masalia makubwa ya viatilifu.
Hitimisho

Kutokana na uwezekano mkubwa wa kubakia mabaki ya madawa ya kuhifadhia mahindi yanayokuwemo kwenye unga wa dona ambayo haijatengenezwa vizuri, ni bora kuendelea kutumia unga wa sembe kuliko kuendelea kutumia dona ambayo hatujui imeandaliwaje. Unga wa sembe unaweza kuwa ni salama na ukatuletea faida zaidi kwani ukoboaji husaidia kuondoa gamba la nje la nafaka za mahindi hivyo kusaidia kupunguza kiwango cha mabaki ya sumu au madawa yaliyokuwa yamewekwa wakati wa kuhifadhi mahindi.

No comments :

Post a Comment