Friday, August 7, 2015

BILION 218 ZATUMIKA BVR

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetumia zaidi ya Sh. bilioni 218 kwa uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki wa
Biometric Votes Registration (BVR) pamoja na ununuzi wa mashine na vifaa vya BVR kits.


Mkurugenzi wa Nec, Kailima Ramadhani (Pichani), alisema Sh. bilioni 133 zilitumika kununua mashine za BVR 8,000 zilizotumika kuandikisha wapiga kura.

Alisema Sh. bilioni 85 zilitumika katika uandikishaji kikiwamo kulipa posho waandikishaji, opereta, kutengeneza kadi, karatasi, wino na vifaa muhimu vilivyohitajika kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo 99.5.

Kwa mujibu wa Kailima, lengo lilikuwa kuandikisha wapigakura 23, 913,184 na hadi uandikishaji unakamilika Agosti Jumanne iliyopita, wapigakura 23,782,558 wameandikishwa.

Kailima alisema maandalizi ya msingi yamekamilika, ikiwamo kuwapata wazabuni wa kusambaza vifaa hivyo ambao watajulikana baada ya Agosti 21, mwaka huu.

“Maandalizi yote yamekamilika, hatuwezi kuchapisha karatasi kwa sasa tunasubiri taarifa za wagombea wakaopitishwa kutoma kwenye vyama vya siasa, kwa maana ya chama, jina, picha, eneo na nafasi anayogombea...tunaweza kuweka majina halafu wakiwekewa pingamizi tutatakiwa kuchapisha tena,” alisema.

Kuhusu malalamiko yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu mwaka 2010, Kailima alisema hakuna ukweli wowote wa kuhama kwa tiki iliyowekwa na mpigakura kwenda kwa mgombea ambaye hakumchagua.

Alisema kuna kamati mbalimbali zenye wajumbe kutoka ndani ya vyama ambao hushiriki hatua zote na kwamba hakuna atayekubali kuona chama chake kinahujumiwa.

Aidha, alirejelea kauli ya Nec kuwa watu watapiga kura katika maeneo waliyojiandikishia na ambao watapigia maeneo mengine watakuwa na fursa ya kuchagua Rais pekee.

CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment