Thursday, August 6, 2015

LIPUMBA: “kila mwanachama ana wajibu wa kujenga chama bila kujali wadhifa wake.”

Dar es Salaam. Sintofahamu imeendelea kukigubika Chama cha Wananchi (CUF), baada ya kauli ya mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kuwaacha wafuasi wa chama hicho katika giza nene juu ya hatima yake kisiasa.

Hali hiyo ilitokea jana baada ya mkutano wa Profesa Lipumba aliouitisha na wanahabari kuahirishwa bila kuelezwa utafanyika lini badala yake akawaambia wafuasi wa chama hicho waliokusanyika makao makuu wa chama hicho, Buguruni kuwa “kila mwanachama ana wajibu wa kujenga chama bila kujali wadhifa wake.”

Makumi ya wafuasi hao walitaka kusikia Profesa Lipumba akieleza mustakabali wake baada ya kuripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa amejiuzulu.

Hata hivyo, wazee wa CUF waliwahi kufika katika ofisi ya mwenyekiti huyo na kumtaka awaeleze alichotaka kuzungumza na wanahabari kwanza, kitendo kilichosababisha kuchelewa kwa mkutano huo na kuvutia idadi kubwa ya wafuasi waliokuwa wakiimba... “Kimyakimya, nguvu ya Lipumba mnaijua.” Wimbo mwingine ulikuwa... “Si si si mnaona!! Nguvu ya Lipumba kuituliza hamuwezi.”

Baada ya kuahirishwa kwa mkutano huo na wafuasi kuendelea kuimba, Profesa Lipumba alitoka ofisini kwake saa 6.25 mchana na baada ya Msemaji wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba kuwatuliza wafuasi hao, Profesa Lipumba alizungumza nao akiwataka waisome na kuielewa katiba ya CUF ambayo imewapa wajibu wa kukijenga chama chao.

Alisema mchakato wa kukijenga chama hautegemei wadhifa alionao kada husika, bali uanachama wake pekee unatosha kuleta maendeleo.


“Mwaka 1995 nilikuwa mwanachama wa kawaida nilipogombea urais kwa tiketi ya CUF na mwaka 1999 nilikuwa mwanachama wa kawaida nilipoongoza kampeni za Jimbo la Temeke na Ubungo ambapo tulishinda lakini wakatuibia kura,” alisema.


Huku akionekana mtulivu tofauti na nyakati nyingine anapozungumza na wafuasi wake, Profesa Lipumba alisema: “Chama ni taasisi na tukijenge kama taasisi, ni wajibu wa kila mwanachama bila kujali nafasi aliyonayo kukijenga,” alisema na kuhitimisha kwa salamu ya; “hakiii” na kujibiwa “kwa wote,” bila kuimalizia.


Baadhi ya wafuasi walionekana kutoridhishwa na kauli yake na kwamba ametumia mafumbo wakati walitaka kusikia habari ya kujiuzulu kwake... “Kiu yangu ilikuwa kumsikiliza baada ya kusikia fununu zilizoandikwa na gazeti jana (juzi) badala yake katuambia tujitahidi kuendeleza chama,” alisema Said Suleiman (58).


Hali ilivyokuwa


Mapema saa nne asubuhi, wafuasi hao walianza kuingia taratibu katika eneo la ofisi hizo na kujaa huku baadhi ya wazee wakiwa wameshaingia ofisini kwa Profesa Lipumba.


Saa 6.05 mchana, Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya akiongozana na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya waliingia ndani ya chumba cha mkutano huku wafuasi wakiwa wamejipanga mstari wakiimba nyimbo za kumsifu Profesa Lipumba na kusema mkutano umeahirishwa hadi utakapotangazwa tena baada ya wazee, wanachama na viongozi mbalimbali kuingia ofisini wakitaka kuelezwa fununu za kujiuzulu.


Kuhusu taarifa za Profesa Lipumba kujiuzulu, Kambaya alidai kwamba wanaosema hivyo wanapiga ramli na kwamba yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ni uzushi na hakuna matatizo yoyote baina ya CUF na Ukawa na kama yangekuwapo, juzi Katibu Mkuu wake ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad asingehudhuria Mkutano Mkuu wa Chadema.


Katika mkutano huo, Maalim Seif alisema hakukuwa na ukweli wowote juu ya kujiuzulu kwa Profesa Lipumba na wanaosema habari hizo wanataka kuwachafua na kuwavuruga Ukawa.


“Kiongozi yeyote anayetaka kujiuzulu lazima barua yake atume kwa katibu mkuu wa chama. Mimi sijapata barua yake na hadi jana saa nne usiku nilikuwa naye wala hakuonyesha dalili za kujiuzulu,” alisema.


Lakini wafuasi waliokuwa wamepiga kambi CUF jana waligawanyika kimawazo juu ya ukweli wa taarifa hizo.


“Hofu ya Profesa Lipumba kujiuzulu ipo, tena kubwa tu ndiyo maana tumekuja kusikiliza lakini kwa sababu amekaa na wazee hakuna kitakachoharibika. Ninaridhika CUF kuendelea kuwa ndani ya Ukawa ili upinzani tushike dola,” alisema Mohamed Njuma kutoka Vingunguti.


Ismail Hamis alisema inaonekana kuna mgogoro hivyo wanataka kujua kilichomkumba kiongozi wao.

No comments :

Post a Comment